Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 anashiriki katika mkutano wa wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7 Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 anashiriki katika mkutano wa wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7 

Ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko Katika Mkutano wa G7: Amani na Akili Mnemba

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 anashiriki katika mkutano wa wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7, ili kutoa wito wa kutafuta, kujenga na kudumisha amani sanjari na ubinadamu katika enzi ya akili mnemba. Huu ni mwaliko kutoka kwa Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni, mwenyeji wa mkutano wa G7. Baba Mtakatifu anatarajia kukutana na kuzungumza na baadhi ya viongozi waliomba kukutana naye!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 14 Juni 2024 anashiriki katika mkutano wa wa Viongozi Wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani, G7, ili kutoa wito wa kutafuta, kujenga na kudumisha amani sanjari na ubinadamu katika enzi ya akili mnemba. Huu ni mwaliko kutoka kwa Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni. Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu atatoa maoni yake kuhusu baadhi ya mada kama vile vita vya sasa vinavyoendelea kupiganwa sehemu mbalimbali za dunia na madhara yake, Bahari ya Mediterania, Afrika, mahusiano na China sanjari na changamoto za teknolojia ya akili mnemba. Baba Mtakatifu Francisko anashiriki kwa mara ya kwanza katika mkutano wa wakuu wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda ishara ya wazi kabisa kwa ulimwengu mzima ambao kwa sasa unajikita katika majadiliano kuhusu ubinadamu katika enzi ya teknolojia ya akili mnemba sanjari na amani duniani. Baba Mtakatifu anatarajia kukutana na viongozi kadhaa walioomba kukutana na kuzungumza naye. Uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko katika mkutano huu ni muhimu sana kama kielelezo cha mamlaka ya kimaadili, mwaliko kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifra kutilia maanani utu, heshima na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 ilinogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Mnemba na Amani”: Artificial Intelligence and Peace: Au “Akili Mnemba na Amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema mifumo yote ya akili mnemba itumike kupunguza mateso ya binadamu, kukuza maendeleo shirikishi na kusaidia kumaliza vita, kinzani na migogoro; na wala si kuongeza ukosefu wa usawa na haki za binadamu duniani.

Kudumisha amani na ubinadamu katika enzi ya akili mnemba
Kudumisha amani na ubinadamu katika enzi ya akili mnemba

Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia kuhusu: Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuelekea ujenzi wa amani; Wakati ujao wa akili mnemba: kati ya ahadi na hatari; Teknolojia ya siku zijazo: mashine ambazo "hujifunza" peke yake; Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia; Masuala motomoto kwa maadili; Je, tugeuze panga ziwe majembe? Changamoto za kielimu na hatimaye ni changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema akili ni kati ya zawadi ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu kwa kumuumba kwa sura na mfano wake, akampatia akili ya kuweza kujibu upendo wa Mungu kwa uhuru zaidi na kwamba, kwa njia ya kazi na maarifa yake, binadamu daima amefanya bidii ili kuyaendeleza maisha yake. Huu ni mwaliko wa kushirikiana na mpango wa Mungu ili kujenga na kudumisha amani miongoni mwa watu wa Mataifa; kukuza uhuru, ushirika wa kidugu ili kuboresha maisha ya binadamu na hatimaye ulimwengu. Mama Kanisa anatambua maendeleo makubwa ya sayansi ambayo yameboresha maisha ya watu wengi, mwaliko ni kuwajibika barabara na matumizi haya makubwa ya sayansi na teknolojia, ili kuepuka hatari sanjari na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo haya makubwa yanajionesa katika ulimwengu wa kidigitali na wasi wasi wake kwa siku za mbeleni.

Ushiriki wa Papa Francisko katika Mkutano wa G7 Italia: Amani na Akili mnemba
Ushiriki wa Papa Francisko katika Mkutano wa G7 Italia: Amani na Akili mnemba

Teknolojia ya siku zijazo: Kumekuwepo na maboresho makubwa katika maisha ya watu kutokana na kuboreka kwa njia za mawasiliano, huduma kwa umma, elimu pamoja na ongezeko la ulaji; mwingiliano na mafunagamano ya kijamii, mambo yanayojionesha katika uhalisia wa kila siku ya maisha ya watu. Kuna haja ya kufahamu kwa kina maana ya sayansi na teknolojia pamoja na athari zake kwa binadamu. Kumbe, teknolojia ya akili mnemba lazima izingatie mambo yafuatayo: Iwe ni shirikishi, inayotekelezeka kwa misingi ya ukweli na uwazi; usalama, usawa, pamoja na kulinda siri za wat una kwamba, teknolojia ya akili bandia iwe inategemewa. Kuwepo na chombo kitakachodhibiti masuala ya maadili, haki msingi za watumiaji na waathirika. Teknolojia ya akili mnemba itumie pia tafiti za kitekolojia na kisayansi, ili kulinda na kudumisha amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, ili haki iweze kuchangia katika mchakato wa kutafuta na kudumisha amani duniani. Teknolojia ya akili mnemba ni teknolojia ya siku zijazo na kwamba, itakuwa na athari kubwa katika medani mbalimbali za maisha ya binadamu, kwa kuweka msingi wa ufahamu hadi kufikia ukweli na kamwe teknolojia hii isitumike kwa ajili ya kusambaza habari za kughushi na hivyo kusababisha njia za mawasiliano ya jamii kutoaminika, kwa kujikita katika masuala ya ubaguzi; kuingilia katika michakato ya uchaguzi, kwenda kinyume cha utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kukomaza ubinafsi; mambo ambayo yanaweza kuwa ni kikwazo kikubwa cha kutafuta na kudumisha amani.

Papa Francisko: Amani na Akili Mnemba.
Papa Francisko: Amani na Akili Mnemba.

Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia kwani kuna hatari kushindwa kuchakata takwimu nyingi na hivyo kusababisha ukosefu wa haki na maamuzi mbele katika mazingira zilimotoka takwimu hizi, kumbe, binadamu anapaswa kufanya tathmini na hatimaye kutoa uamuzi wa mwisho. Hapa, kuna haja ya kufikiria ukomo katika teknolojia kamwe teknolojia isitumike kuzalisha utajiri kwa watu wachache ndani ya jamii na hivyo kuhatarisha demokrasia na amani katika ujumla wake. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia pia masuala motomoto kwa maadili kwani hapa watu na haki zao msingi, utu na heshima yao vinahusishwa kwa ukaribu na hivyo mifumo hii ya teknolojia ya akili mnemba inaweza kusababisha ubaguzi, ukosefu wa haki na usawa katika jamii na hata wakati mwingine, kuathiri fikra na utendaji wa watu. Kumbe utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, sanjari na fadhila ya huruma, upendo na msamaha. Hapa haki za wafanyakazi na fursa za ajira zinapaswa kuzingatiwa, ili kwamba, matumizi ya teknolojia ya akili mnemba isiwe ni sababu ya wafanyakazi kukosa ajira. Je, tugeuze panga ziwe majembe? Kwa sasa matumizi ya teknolojia ya akili mnemba kijeshi ni jambo la hatari sana kimaadili na kwamba, wajanja wachache wasije kuibuka na kuanza kuwekeza kwenye biashara ya silaha na hivyo kusababisha maafa makubwa ya vita, bali matumizi ya teknolojia ya akili mnemba yasaidie kukoleza amani duniani; yaboreshe sekta ya kilimo, sekta ya elimu na maisha ya watu kwa kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na mafungamano ya kijamii; pamoja na majadiliano katika ukweli na uwazi.

Italia ni mwenyeji wa mkutano wa G7 kwa Mwaka 2024
Italia ni mwenyeji wa mkutano wa G7 kwa Mwaka 2024

Huu ndio mwelekeo wa kimaadili wa matumizi sahihi ya teknolojia ya akili mnemba. Kwa hakika teknolojia ya akili mnemba imeleta changamoto za kielimu katika mfumo wa kufundishia na majiundo ya wanafunzi. Wanafunzi wanapaswa kufundishwa kujikita katika upembuzi yakinifu, weledi na kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema; kwa kujenga madaraja ya watu kukutana, ili kuishi kidugu na kwa amani. Na hatimaye Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa zinazopaswa kukazia pamoja na mambo mengine ni umoja, mwongozo utakaoratibu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali; kwa kuheshimu na kulinda haki msingi za binadamu, ili kudumisha misingi ya haki na amani sanjari na kusikiliza na kuzingatia maoni ya watu mbalibali mintarafu teknolojia ya akili mnemba. Baba Mtakatifu anahitimisha Ujumbe wa Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani” kwa kusema, amani ni matunda mafungamano yanayotambua utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kushirikiana na wengine kwa ajili ya ustawi wa wengine. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba ili mifumo yote ya akili mnemba itumike kupunguza mateso ya binadamu, kukuza maendeleo shirikishi na kusaidia kumaliza vita, kinzani na migogoro; na wala si kuongeza ukosefu wa usawa pamoja na uvunjaji wa haki msingi za binadamu duniani.

Akili Mnemba
13 June 2024, 15:17