Vatican imechapisha ratiba ya matukio yajayo ya kipapa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu ana ratiba ya safari zijazo yenye shughuli nyingi itakayoanza na ziara ya kichungaji katika jiji la Trieste nchini Italia mapema mwezi ujao katika fursa ya Juma la Kijamii Katoliki Italia. Katika ziara hiyo tarehe 7 Julai 2024, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na wahamiaji na watu wengine waliotengwa. Baadaye, Papa atafanya ziara mbili za Kitume nje ya Italia. Ya kwanza, kuanzia tarehe 2-13 Septemba 2024 itakayompeleka katika nusu ya dunia, hadi kusini mashariki mwa Asia na Oceania, ambako atatembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor-Leste, na Singapore.
Kuanzia tarehe 26-29 Septemba, Papa Francisko atafanya ziara ya siku moja nchini Luxembourg kabla ya kutembelea miji mitatu ya Ubelgiji, ambako atashiriki katika sherehe za kuadhimisha miaka 600 tangu kuanzishwa kwa vyuo vikuu vya Kikatoliki vya Leuven na Louvain-la-Neuve. Ratiba ya kiliturujia iliyotolewa siku ya Jumatatu tarehe 3 Juni 2024 pia ilibainisha kuwa Papa Francisko ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 29 Juni ambayo inajumuisha baraka za Pallia kwa Maaskofu Wakuu wapya wa Metropolitan. Hatimaye, tarehe 1 Julai Papa Francisko atafanya Mkutano wa Kawaida na Makardinali kwa ajili ya kupiga kura kuhusu sababu mbalimbali za kutangazwa kuwa mtakatifu.
Shughuli za Papa Francisko zinapatikajana hata katika Tovuti ya Vatican bonyeza hapa:website.
Ratiba ya Maadhimisho yatakayoongozwa na Papa Francisko
Tarehe 29 Juni 2024
Maadhimisho ya Watakatifu Petro na Paulo, mitume katika Basilika ya Mtakatifu Petro, saa 3:30 asubuhi kwa Misa Takatifu na baraka za Pallia kwa Maaskofu wakuu wapya wa Majimbo makuu.
Tarehe 1 Julai 2024
Ziara ya kichungaji ya Baba Mtakatifu huko Trieste (Italia).
Tarehe 2-13 Septemba 2024
Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu kwenda Indonesia, Papua New Guinea, Timor Leste, na Singapore.
26-29 Septemba
Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu kwenda Luxembourg na Ubelgiji.