Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 15 Juni 2024 amekutana na kuzungumza na Wakurugenzi na washirika wa Makampuni makuu na Benki maarufu. Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 15 Juni 2024 amekutana na kuzungumza na Wakurugenzi na washirika wa Makampuni makuu na Benki maarufu.   (Vatican Media)

Wakurugenzi wa Mashirika na Benki Maarufu: Vipaumbele: Mazingira, Maskini na Vijana

Katika hotuba yake amejikita katika changamoto kuu tatu wanazopaswa kuzivalia njuga: Mazingira; Utunzaji wa maskini pamoja na kuwajali vijana wa kizazi kipya. Utekelezaji wa majukumu na maamuzi yao yanagusa masuala ya kiuchumi, maisha ya kijamii na kisiasa na athari zake ni kwa maelfu ya watu, hawa ni wafanyakazi na wawekezaji na zaidi ikiwa kama wanafanya kazi kwa kiwango cha Kimataifa. Nguvu ya uchumi imeunganishwa katika nguvu ya kisiasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 15 Juni 2024 amekutana na kuzungumza na Wakurugenzi na washirika wa Makampuni makuu na Benki maarufu. Katika hotuba yake amejikita katika changamoto kuu tatu wanazopaswa kuzivalia njuga: Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Utunzaji wa watu maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa vipaumbele vya kijamii pamoja na kuwajali vijana wa kizazi kipya. Utekelezaji wa majukumu na maamuzi yao yanagusa masuala ya kiuchumi, maisha ya kijamii na kisiasa na athari zake ni kwa maelfu ya watu, hawa ni wafanyakazi na wawekezaji na zaidi ikiwa kama wanafanya kazi kwa kiwango cha Kimataifa. Nguvu ya kiuchumi imeunganishwa na nguvu ya kisiasa. Kwa kweli, makampuni makubwa, pamoja na uchaguzi wa matumizi, kuokoa na uzalishaji, pia huathiri hatima ya serikali, sera za kitaifa na kimataifa za umma sanjari na maendeleo endelevu. Viongozi hawa wanaufahamu ukweli huu kwa sababu wanaoishi ndani mwake na ukweli huu ni sehemu ya maeneo yao ya kujidai.

Vipaumbele: Mazingira, Maskini na Vijana
Vipaumbele: Mazingira, Maskini na Vijana

Hii ni changamoto kwa viongozi hawa wakuu kujibidiisha kuufahamu na kuuangalia kwa umakini mkubwa na utambuzi ili hatimaye, kung’amua athari za moja kwa moja mintarafu maamuzi yao. Kwa sababu leo hii, kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mwanadamu uchumi ni mkubwa. Baba Mtakatifu amewapatia angalisho kuhusu hali ya mazingira ya dunia, ili waweze kuchukua taadhari mapema, mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuna shida na changamoto kubwa ya kimazingira inayotegemea mambo mengi, hii ikiwa pamoja na chaguzi za kiuchumi na ujasiriamali zilizopita pamoja na hali halisi kwa sasa. Haitoshi kuheshimu sheria za nchi, au kanda ambazo kimsingi zinakwenda kwa kusua sua, kuna haja ya kuvumbua kwa kutazamiaq uchaguzi wa ujasiri na wa kuona mbali zaidi mambo yanayoweza kuigwa. Ubunifu wa mjasiriamali katika ulimwengu mamboleo lazima kwanza kabisa uwe uvumbuzi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Makampuni yawakaribishe na kuwakirimia vijana nafasi za kazi
Makampuni yawakaribishe na kuwakirimia vijana nafasi za kazi

Baba Mtakatifu anawataka wakurugenzi hawa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini, kwa kuwashirikisha katika uchumi shirikishi na kamwe maskini wasitengwe katika mchakato huu, kwa kudharaulika, kiasi cha umaskini wenyewe kuwa kama hatia. Maskini wawe ni rasilimali watu na wapewe kipaumbele cha pekee, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wawe ni wahusika wakuu katika mchakato wa maendeleo ya kiuchumi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, vijana mara nyingi ni miongoni mwa maskini wa nyakati hizi. Hawa ni maskini wa rasilimali, fursa na siku zijazo. Idadi kubwa ya wazee nchini Italia inatokana na idadi ya watoto wanaozaliwa kuwa ni wachache na kwamba, hakuna kazi anayo weza kujifunza bila "ukarimu wa ushirika", yaani huu ni mwaliko wa kuwaribisha vijana kwa ukarimu hata kama wakati mwingine hawana uzoefu na ujuzi unaohitajika, kwa sababu kila kazi mtu anaweza kujifunza tu kwa kufanya kazi. Baba Mtakatifu anawahimiza ili waweze kuwa karibu kwa kuwakaribisha vijana katika kazi na biashara zao, kwa kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu anawaombea ili waweze kufanya maamuzi ya ujasiri, kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya mazingira, ukarimu kwa maskini na vijana. Hii ni dhamana na jukumu zito sana katika maisha, lakini kwa kufanya hivi, huu ni uwekezaji wenye kuzaa matunda zaidi na hata kiuchumi, kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa, waendelee kupania na kunia makubwa. Baba Mtakatifu amewabariki na kuwatakia mema yote ya mbinguni.

Wakurugenzi wa Benki
15 June 2024, 14:33