Tafuta

Mazishi ya mtawa mkuu wa Buddha aliyeuawa na vikosi vya usalama nchini Myanmar. Mazishi ya mtawa mkuu wa Buddha aliyeuawa na vikosi vya usalama nchini Myanmar.  (ANSA)

Papa atoa wito kwa wasiotaka amani waongoke na kuwa na majadiliano na amani

Papa Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana amesali kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ili uguse mioyo ya wale wanaochochea migogoro na vurugu.Ameomba kutosahau nchi zenye vurugu:Ukraine,Nchi Takatifu na Myanmara na nyingine.Siku ya wafiadini wa kirumi:"Leo hii tunaishi kipindi cha kishahidi zaidi ya hapo awali."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 30 Juni 2024 amewasalimia kuanzia na Waroma wote na mahujaji kutoka Italia na sehemu mbali mbali za Nchi.” Papa amewasalimu  hasa watoto wa Mzunguko wa Wamisionari wa “Misyjna Jutrzenka” kutoka Skoczów, nchini Poland; na waamini kutoka California na Costa Rika, Masista wa Shirika la Mabinti wa Kanisa, ambao siku hizi wamekuwa katika hija wakifuata nyayo za mwanzilishi wao, Mtumishi wa Mungu Maria Oliva Bonaldo, pamoja na kundi la walei. Pia kwa vijana kutoka Gonzaga, karibu na Mantua.

Mahujaji na waamini katika sala ya Malaika wa Bwana 30 Juni 2024
Mahujaji na waamini katika sala ya Malaika wa Bwana 30 Juni 2024

Kumbukumbu ya Wafiadini wa kwanza wa kirumi

Baba Mtakatifu Francisko katika salamu zake amewakumbuka Wafiadini wa kwanza wa Kirumi. “Sisi pia tunaishi katika wakati wa kuuawa kwa sababu ya imani, wakati ambao ni zaidi kuliko katika karne za awali. Wengi kaka na dada zetu katika sehemu mbalimbali za ulimwengu wanakumbana na ubaguzi na mateso kwa sababu ya imani yao; hivyo kuleta matunda mengi kwa Kanisa. Wengine wanakabiliwa na mauaji kwa kile kiitwacho: "white-glove” - glovu nyeupe”. Kwa njia hiyo Papa Francisko ameomba “waungwe mkono na kuhamasishwa na ushuhuda wao wa upendo kwa Kristo.”

Siku ya Mwisho wa Juni:Moyo Mtakatifu wa Yesu

Baba Mtakatifu akiendelea amesema: “Katika siku hii ya mwisho ya Juni, tuuombe Moyo Mtakatifu wa Yesu uguse mioyo ya wale wanaotamani vita, ili waweze kuongoka kuwa na mipango ya mazungumzo na amani.” Papa aidha amewaomba wote ili wasisahau waliouawa kishahidi nchini Ukraine, Palestina, Israel, Myanmar, na maeneo mengine mengi ambako kuna mateso mengi kutokana na vita!” Hatimaye amewatakia Dominika Njema na tafadhali wasisahau kumuombea. “Mlo mwema na kwaheri ya kuonana.

Baada ya Angelus Papa ametoa wito wa amani nchi zenye vita
30 June 2024, 14:14