Tafuta

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Mapadre waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre kuanzia Mwaka 2014-2014. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Mapadre waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre kuanzia Mwaka 2014-2014.  (Vatican Media)

Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mapadre Wapya 2014 - 2024

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Mapadre waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre kuanzia Mwaka 2014-2024. Huu ni mkutano uliofanyika kwa faragha. Kati ya mada zilizojadiliwa kati ya Mapadre hawa na Baba Mtakatifu ni pamoja na: uzoefu na mang’amuzi yao katika huduma kwa wagonjwa na wazee; changamoto za maisha na utume wa Kipadre; mang’amuzi yao kwa huduma kwa watu wa Mungu; Upweke hasi na hofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wito na maisha ya Kipadre ni zawadi na sadaka kubwa inayotolewa kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Huu ni utimilifu wa wito unaowawezesha Mapadre kuwa ni Kristo mwingine kwa kutenda kama Kristo Yesu “In persona Christi.” Maisha na utume wa kipadre unatekelezwa kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa pamoja na kuhudumia kwa upendo watu wa Mungu. Kwa ufupi kabisa, Mapadre wanashiriki katika huduma ya: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kristo Yesu katika maisha na utume wake wa hadhara alijitambulisha kuwa ni Mchungaji mwema, hali ambayo ilijidhihirisha katika ushuhuda wa maisha yake ya kila siku kiasi cha kusema kwamba, Yeye ndiye mchungaji mwema anayeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Kristo Yesu ni mlango salama wa kondoo na kondoo humsikia sauti yake kwa sababu huwaita kwa majina na kuwapeleka nje kwa kuwatangulia nao humfuata nyuma. Anawajua walio wake na walio wake wanamjua fika. Rej. Yn. 10: 1-18. Huu ni mwendelezo wa kazi ya ukombozi ambayo Kristo Yesu amekuja kuitekeleza hapa duniani, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Mapadre wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili baada ya kukutana na Kristo Yesu Mfufuka. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha; ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni.

Papa Francisko amekutana na Mapadre wapya: 2014-2024
Papa Francisko amekutana na Mapadre wapya: 2014-2024

Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! Huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa wagonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kutoa mkazo wa pekee katika Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha.  Mapadre wanakumbushwa kwamba, utume wao wa Kipadre unajikita katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho zinazofumbatwa katika ukarimu, ushuhuda, huruma; ukweli na uwazi katika kanuni maadili. Mapadre wawe tayari kuwasindikiza waamini katika hija ya toba na wongofu wa ndani, kwa kuonesha uvumilivu; kwa kuwa na mawazo mapana na wakarimu katika kutoa msamaha wa Mungu. Mapadre pia wanapaswa kuwa ni kielelezo cha toba na wongofu wa ndani na kwamba, Sakramenti ya Upatanisho inapaswa kuwa ni kiini cha maisha ya Kikristo kwani Mapadre ni vyombo vya Upatanisho. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Mapadre waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre kuanzia Mwaka 2014-2024. Huu ni mkutano uliofanyika kwa faragha. Kati ya mada zilizojadiliwa kati ya Mapadre hawa na Baba Mtakatifu ni pamoja na: uzoefu na mang’amuzi yao katika huduma kwa wagonjwa na wazee; changamoto za maisha na utume wa Kipadre; mang’amuzi yao kwa huduma kwa watu wa Mungu; Upweke hasi, hofu na wasiwasi.

Mapadre wapya na changamoto za maisha na utume wao
Mapadre wapya na changamoto za maisha na utume wao

Mkutano huu ulifanyika kwenye Nyumba ya Masista wa “Divin Maestro” wanaoishi Jimboni Roma. Hii ni awamu ya pili kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na Mapadre wanaofanya utume wao Jimbo kuu la Roma. Itakumbukwa kwamba, mara ya mwisho Baba Mtakatifu alikutana na kuzungumza na Mapadre waliokuwa wanaadhimisha kumbukizi ya Miaka 40 tangu walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mapadre waliopadrishwa kati ya Mwaka 2014 hadi Mwaka 2024 wameonesha furaha ya maisha na wito wao wa Kipadre; Imani ya watu wa Mungu sanjari na changamoto za huduma. Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, wanapaswa kuonesha ukaribu wa Mungu kwa kujitosa kimaso maso katika huduma ya upendo kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema, ili waweze kuona, kusikiliza na kujibu kwa vitendo kilio na mhangaiko ya watu wa Mungu kama alivyofanya yule Msamaria mwema: Alipomwona, alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai na hatimaye, akamtunza. Mapadre wawe na ujasiri wa kutekeleza dhamana, wajibu na utume wao bila ya kuogopa. Parokia zao iwe ni alama na utambulisho wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Kipimo cha ukaribu wa Mungu kwa waja wake ni pamoja na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, bila kumezwa na malimwengu. Mapadre waguswe na umaskini pamoja na mahangaiko ya watu wao, ili kuinua na kusimamia utu, heshima na haki zao msingi. Mapadre wajenge utamaduni wa kuwasikiliza waamini wao kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Mkutano huu, imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kuwatia shime Mapadre wapya, kwani majiundo ya awali Seminarini hayatoshi na kwamba, kwa kutekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, wanaendelea kukomaa katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu amewataka Mapadre kujenga utamaduni wa ukaribu na Mungu kwa njia ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu; Ukribu na Askofu mahalia ili kujenga na kudumisha urafiki na udugu wa kibinadamu katika huduma kwa watu wa Mungu; Ukaribu kati ya Mapadre katika maisha na shughuli za kichungaji; Ukaribu na watu wa Mungu kwa njia ya huduma makini.

Mapadre Wapya

 

03 June 2024, 14:14