Tafuta

Hija ya 13 ya Chama cha Watumishi wa Altareni Kimataifa: Coetus Internationalis Ministrantium 2024 Hija ya 13 ya Chama cha Watumishi wa Altareni Kimataifa: Coetus Internationalis Ministrantium 2024  (Vatican Media)

Chama cha Kimataifa Cha Watumishi Altareni: Ekaristi Takatifu

Hija ya kumi na tatu ya Chama cha Watumishi wa Altareni Kimataifa kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Pamoja nawe. Papa Katika hotuba yake, amekazia: Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanaonja na kushiriki uwepo angavu wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi na kwamba, upendo wa dhati kutoka kwa Kristo Yesu ndicho kipimo cha upendo kwa Mungu jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ni mahali pa kwanza kabisa pa kuwafunda watoto misinngi ya imani, maadili, nidhamu na utu wema. Wazazi wanapaswa kuwaangalia watoto wao kama zawadi kutoka kwa Mungu na kuwaheshimu kama binadamu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wawafundishe kushika Amri za Mungu zinazomwilishwa katika upendo kwa Mungu na jirani. Wazazi wawe ni mashuhuda na vyombo vya: utu wema, heshima, uaminifu, msamaha, upendo na mshikamano wa dhati. Nyumbani pawe ni mahali ambapo watoto wanafundwa fadhila njema, ili waweze kukua na kukomaa: kiakili, kiimani, kimaadili na kiutu! Mama Kanisa anaendelea kuwekeza katika malezi, makuzi na majiundo ya watoto, ambao kimsingi ni matumaini ya Kanisa na Jamii ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Vijana 70elfu wamehudhuria hija ya watumishi wa Altareni kwa mwaka 2024
Vijana 70elfu wamehudhuria hija ya watumishi wa Altareni kwa mwaka 2024

Kuanzia tarehe 29 Julai hadi tarehe 3 Agosti 2024, Mji wa Roma umefunikwa na watumishi wa Altareni zaidi ya sabini elfu, kutoka sehemu mbalimbali za dunia, walioitikia mwaliko wa “Coetus Internationalis Ministrantium; Associazione Internationalis Ministrantium", CIM, yaani Chama cha Kimataifa cha Watumishi Altareni. Hija ya “XIII” kumi na tatu ya Watumishi wa Altareni kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Pamoja nawe.” Vijana hawa kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanataka kujiaminisha tena kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwamba, wanataka kumtumikia bila ya kujibakiza, huku wakichuchumilia amani na utulivu wa ndani; kwa hakika wanataka kujikita na hivyo kuwa ni mashuhuda maalum wa Kristo Yesu pamoja na Injili yake, ili kutangaza na kushuhudia maisha ya sala yanayobubujika kutoka katika furaha ya Injili, ili kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii.

Kauli mbiu: Pamoja Nawe
Kauli mbiu: Pamoja Nawe

Huu ni muda wa hija kuzunguka maeneo ya kihistoria, kipindi cha sala na tafakari pamoja na vijana kufurahia maisha ya ujana wao kwa kukutana na vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia kama njia ya ujenzi wa madaraja na utamaduni wa watu kukutana. Huu ni ushuhuda kwamba, vijana ni jeuri ya Kanisa. Hawa ni vijana kutoka Australia, Hungaria, Ubelgiji, Uswisi Croatia, Ufaransa, Lithuania, Ureno, Luxemborg, Jamhuri ya Watu wa Czech, Romania, Serbia na Ukraine. Ujerumani ina idadi kubwa ya vijana wapatao 35, 000, na wanasindikizwa na Askofu Msaidizi Johannes Wubbe, Rais wa Tume ya Vijana, Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani.

Vijana 35 elfu kutoka Ujerumani wameshiriki
Vijana 35 elfu kutoka Ujerumani wameshiriki

Hija ya kumi na tatu ya Watumishi wa Altareni Kimataifa kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Pamoja nawe” na imefikia kilele chake kwa vijana hawa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne jioni tarehe 30 Julai 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika hotuba yake, amekazia kuhusu adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Waamini wanaonja na kushiriki uwepo angavu wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi na kwamba, upendo wa dhati kutoka kwa Kristo Yesu ndicho kipimo cha upendo kwa jirani, changamoto na mwaliko kwa vijana hawa kushirikishana ile furaha ya kuwa ni watumishi wake waaminifu Altareni. Baba Mtakatifu anasema kauli mbiu ya “Pamoja Nawe” ni maneno yanayotoa mwanya na mwaliko kwa waamini kufanya upembuzi yakinifu, ili hatimaye, kupata maana inayokusudiwa.

Vijana ni mashuhudia wa Injili ya Kristo katika maisha na utume wao
Vijana ni mashuhudia wa Injili ya Kristo katika maisha na utume wao

Ni maneno yanayofumbata na kuambata fumbo la maisha ya mwanadamu na upendo wa Mungu, tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake na kwamba, mtoto hana kitu cha kuogopa kwani Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye na ndivyo ilivyo hata kwa wazazi pia. Lakini maneno haya kwa Watumishi wa Altare yanapata maana mpya. Hii inatokana na ukweli kwamba, wao kama watumishi Altareni, wanao uzoefu na mang’amuzi ya Liturujia ya Kanisa na kwamba, katika maadhimisho hayo mhusika mkuu ni Mwenyezi Mungu, kwani kama Maandiko Matakatifu yanavyoshuhudia: “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.” Mt 18:20. Na uwepo huu wa Mungu kati pamoja na waja wake, unafikia kilele chake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Papa Francisko anawashukuru vijana kwa ushuhuda wao wa imani
Papa Francisko anawashukuru vijana kwa ushuhuda wao wa imani

Uwamo wa Kristo Yesu kwenye maumbo ya Mkate na Divai unajidhihirisha kwa Ibada ya Misa Takatifu, ambayo kwayo watumishi wa Altareni wanashiriki kikamilifu. Na kwa namna ya pekee, wanaonja na kugusa uwepo wake wakati wanapokomunika, kielelezo cha upendo wake unaojidhihirisha katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kristo Yesu amewahakikishia wafuasi wake kwamba, atakakuwa pamoja nao na huu ndio ukweli pia kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuwa ndani mwake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watumishi wa Altareni kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo kwa waja wake, upendo unaopaswa kushirikishwa kwa wengine na hivyo kuwa ni viumbe wapya katika Kristo Yesu. Kumbe, huu ni mwaliko kwa watumishi wa Altare kumwimbia Kristo Yesu utenzi wa sifa na shukrani kwa uwepo wake wa karibu.

Vijana ni kielelezo cha furaha na matumaini ya Kanisa
Vijana ni kielelezo cha furaha na matumaini ya Kanisa

Kumbe, watumishi wa Altareni wanapaswa kujenga ndani mwao: huruma na mapendo yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, tayari kuomboleza na wale wanaoomboleza; kufurahi na wale wanaofurahi bila ya kuathirika na maamuzi mbele wala ubaguzi kwa misingi ya rangi yam tu, tamaduni au mahali anapotoka mtu. Kauli mbiu “Pamoja Nawe” inabeba ndani mwake Fumbo kubwa na kwamba, wanaheri wale wote waliobahatika kufanya hija ya maisha ya kiroho kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni fursa na kushirikishana ile furaha ya kuwa ni Mtumishi wa Kristo Yesu; Wahudumu wa upendo wake mkuu usiokuwa na mawaa; Wahudumu wa Moyo wake Mtakatifu uliotobolewa, ili kuganga na kutibu madonda ya mwanadamu; na kuwaokoa kutoka katika mauti na kifo na hivyo kuwakirimia maisha ya uzima milele.

Watumishi Altareni
31 July 2024, 15:09