Tafuta

Fumbo la Ekaristi Takatifu: Akatwaa, Akashukuru na Kuwagawia

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 17 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Mama Kanisa anawawekea waamini wake muujiza uliotendwa na Kristo Yesu kwa kuwashibisha mkutano mkuu. Hii ni alama ambayo, Kristo Yesu ataitumia tena wakati wa Karamu ya Mwisho: Akatwaa, Akashukuru na Kuwagawia; mambo makuu matatu yanayounda maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Rej. Yn 6:1-15. Mwaliko wa kumshukuru Mungu kwa unyenyekevu na furaha kwa zawadi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni zawadi; na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha ushirika, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa kujikita katika utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 28 Julai 2024 amesema kwamba, Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 17 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Mama Kanisa anawawekea waamini wake muujiza uliotendwa na Kristo Yesu kwa kuwashibisha mkutano mkuu. Hii ni alama ambayo, Kristo Yesu ataitumia tena wakati wa Karamu ya Mwisho: Akatwaa, Akashukuru na Kuwagawia; mambo makuu matatu yanayounda maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Rej. Yn 6:1-15.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Mwinjili Yohane anamwonesha mtoto aliyekuwa na mikate mitano na samaki wawili, lakini alikuwa tayari kuwashirikisha wengine kile kidogo alichokuwa nacho. Kitendo hiki kinafafanuliwa na Padre anapotolea sadaka Altareni yaani: Mkate na Divai na kwamba, kila mwamini anajisadaka. Kimsingi, binadamu ana mahitaji makubwa yasiyoweza kutoshelezwa kwa mikate mitano na samaki wawili. Lakini Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anatumia mikate hii mitano na samaki wawili na kutenda muujiza mkubwa kwa kuwashibisha mkutano mkuu, akiwa kati kati ya wafuasi wake na kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kumshukuru Mungu kwa unyenyekevu na furaha kuu kwa kutambua kwamba, kila kitu anachomiliki mwanadamu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kumbe, katika sadaka hii, mwamini anamrudishia tena Mungu zawadi pamoja na sadaka ya Kristo Yesu, kwa mwamini kushirikisha upendo wake dhaifu. Ni katika muktadha wa baraka, mwamini anamtolea Mungu sifa na shukrani kwa wema na ukarimu wake, wakati Mwenyezi Mungu akitakatifuza na kubariki jitihada “za senti mbili.” Rej Lk 21:1-4. Basi Yesu akaitwaa ile mikate na wale samaki wawili, akashukuru, akawagawia walioketi. Rej Yn 6:11. Kitendo hiki katika Ibada ya Misa Takatifu ni kielelezo cha ushirika, pale waamini katika umoja wao, wanajongea Altareni ili kushiriki Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu.

Akatwaa, Akashukuru na Kuwagawia: Ukarimu wa Mungu
Akatwaa, Akashukuru na Kuwagawia: Ukarimu wa Mungu

Haya ni matunda ya kazi ya mikono ya waamini wote yanayogeuzwa kuwa ni chakula kwa ajili ya wengi. Huu ni wakati murua kabisa unaowafundisha waamini kujitahidi kuishi kila wakati katika upendo kama kielelezo cha zawadi ya neema kwa yule anayetoa na kwa yule anapokea. Hii ni fursa anasema Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini kukua kwa pamoja kama ndugu wamoja, daima wakiwa wameungana katika kifungo cha upendo. Baba Mtakatifu anawauliza waamini Je, katika maisha yao kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu wanaamini kwamba, wanacho kitu cha pekee, cha kuweza kuwashirikisha ndugu zao katika Kristo Yesu? Je, wamekuwa ni watu wa shukrani kwa wema na ukarimu wa Mungu katika maisha yao; ukarimu unaoendelea kuonesha upendo wa Mungu? Je, kama mwamini anashirikishana na wengine fursa hii ya kukutana pamoja ili kutajirishana? Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Bikira Maria awasaidie waamini kuishi kwa imani kila adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kutambua na kuonja kila siku “muujiza” wa neema ya Mungu.

Ekaristi Takatifu
28 July 2024, 14:48

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >