Tafuta

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 28 Juni 2024, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 28 Juni 2024, Baba Mtakatifu amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza   (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 1700 Tangu Kuadhimishwa Kwa Mtaguso Wa Kwanza wa Nicea

Patriaki amekazia kuhusu: Kifungo cha upendo; taalimungu katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na dhana ya Sinodi katika ujenzi wa Kanisa; na kama chombo cha majadiliano, amani na upatanisho; Roma ni mji uliopambwa kwa damu ya mashuhuda wa imani; Mtakatifu Petro na Paulo, Mitume. Sherehe hii ni fursa inayosaidia kujenga na kuimarisha mafungamano ya upendo katika hija ya majadiliano ya kiekumene kuelekea kwenye umoja kamili wa Kanisa. Umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ni katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, tarehe 28 Juni 2024, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amegusia kuhusu: Ushuhuda wa Makanisa haya pacha, Kumbukizi ya Miaka takribani 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Anathagoras, Tamko la Amani Kuhusu Yerulusalem, Waamini waungane ili kuombea amani; Jubilei ya Miaka 1700 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso wa kwanza wa Nicea. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli kwa kutuma ujumbe katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, kielelezo cha mafungamano ya dhati kati ya Makanisa haya pacha, yaani Kanisa la Roma na lile la Costantinopoli, ambayo yamedhamiria kujikita katika hija ya kutafuta na hatimaye, kuambata umoja wa Wakristo, dhamana inayotekelezwa kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, atakayewawezesha Wakristo kufikia ushirika kamili katika tofauti zao msingi.

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ukishiriki katika Ibada ya Misa.
Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza ukishiriki katika Ibada ya Misa.

Mtakatifu Petro, Mtume alikuwa ni mvuvi kutoka Galilaya aliyechaguliwa kuwa ni mvuvi wa watu na Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa alilidhulumu Kanisa la Kristo, lakini kwa mwanga wa Neno la Mungu wameweza kushiriki kikamilifu mang’amuzi ya Fumbo la Pasaka, hawa wamekombolewa na Kristo Yesu na mlango ukawafungukia wenyewe katika mwelekeo wa maisha mapya. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia kielelezo cha mlango mintarafu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Ukombozi wa Mtakatifu Petro kutoka Gerezani na Mtakatifu Paulo akakutana uso kwa uso na Kristo Yesu Mfufuka, wakati akiwa njiani kuelekea Dameski, akienda kuwadhulumu Wakristo. Wote hawa wakapewa fursa ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto kwa Wakristo kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha yao; watakatifu Petro na Paulo Mitume ni walinzi na waombezi wa mji wa Roma; Maaskofu wakuu waliopewa Pallia Takatifu wanaitwa na kutumwa kuwa ni wachungaji wenye ari na moyo mkuu, wanaofungua lango la Injili, tayari kushiriki katika ujenzi wa Kanisa na jamii yenye malango yaliyo wazi.

Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa kwanza wa NICEA
Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa kwanza wa NICEA

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume na Miamba wa Imani, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli alimtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe mzito kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 tangu kuadhimishwa kwa Mtaguso wa kwanza wa Nicea uliowasilishwa kwa Baba Mtakatifu na Askofu mkuu Emmanuel di Calcedonia. Katika ujumbe huu, amekazia kuhusu kifungo cha upendo; taalimungu katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na dhana ya Sinodi katika ujenzi wa Kanisa; na kama chombo cha majadiliano, amani na upatanisho; Roma ni mji uliopambwa kwa damu ya mashuhuda wa imani; Mtakatifu Petro na Paulo, Mitume.  Maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume ni fursa inayosaidia kujenga na kuimarisha mafungamano ya upendo katika hija ya majadiliano ya kiekumene kuelekea kwenye umoja kamili wa Kanisa. Kwa hakika, Mitume Petro na Paulo kwa neema ya Mungu walikuwa wameungana: kiroho na kiakili, kielelezo na mfano bora kwa wafuasi wa Kristo Yesu; Mitume hawa waliupamba mji wa Roma kwa ushuhuda wa maisha yao. Huu ni mfano bora wa kuigwa na Wakristo katika mchakato wa kutafuta na kujenga umoja wa Wakristo. Lengo kuu ni kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Rej. Efe 4:3 sanjari na maadhimisho ya pamoja ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaombea mafanikio katika Jubilei ya 1700
Patriaki Bartolomeo wa kwanza anaombea mafanikio katika Jubilei ya 1700

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuimarisha majadiliano ya kitaalimungu na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kurahisisha ukaribu wa Makanisa haya mawili, unaofumbatwa katika dhana ya Sinodi, kwa kutambua kwamba, Kanisa, kimsingi tayari ni Sinodi, kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na linaongozwa na Roho Mtakatifu na kwamba, mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni muhimu sana. Hizi ni juhudi pia zinazoendelea kutekelezwa katika majadiliano ya kitaalimungu kiekumene mintarafu ukulu wa Mtakatifu Petro na Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ile sentensi “Atokaye kwa Baba na Mwana: Filoque na Mafundisho kuhusu kutokukosea kwa Papa anapofundisha akiwa ameungana na Maaskofu wengine, “Infallibility” yamefikia mahali pazuri, kwani huu ni mchakato ambao umesimikwa katika unyenyekevu, upendo na uponyaji na ukweli, ili Wakristo wote kwa pamoja waweze kuufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufikia kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo. Rej. Efe 4: 13.

Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza tarehe 29 Juni 2024
Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza tarehe 29 Juni 2024

Kwa hakika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi umekuwa ni chombo cha majadiliano ya kiekumene, amani na upatanissho na kwamba, Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli linaungana na Baba Mtakatifu kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, ili vita ikome, na hatimaye, Mwenyezi Mungu aweze kuiongoza “miguu yetu kwenye njia ya amani.” Lk 1: 49. Madhara ya vita ni makubwa kamwe hayawezi kubebwa na mtu mmoja. Mji wa Roma umepambwa kwa damu ya mashuhuda wa imani: Mtakatifu Petro na Paulo, Mitume, mwaliko wa Kanisa kujikita katika kutafuta, kujenga na hatimaye kudumisha amani. Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka 2025 wakristo wote wataadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima. Watu wanamtafuta Kristo Yesu hata bila ya kutambua. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anamwomba Mwenyezi Mungu ili awakirimie waja wake afya na nguvu, ili kwa pamoja waweze kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 ya Mtaguso wa kwanza wa Nicea.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza
02 July 2024, 15:20