Jubilei ya Miaka 400 Tangu Kupatikana Kwa Masalia ya Mtakatifu Rosalia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Rosalia Sinibaldi alizaliwa Jimbo kuu la Palermo kati ya Mwaka 1130 na kufariki dunia tarehe 4 Septemba 1170. Ibada yake imeenea sana Kusini mwa Italia na ni mlinzi na mwombezi wa Jimbo kuu la Palermo na anasherehekewa kila mwaka kati ya tarehe 14 hadi tarehe 15 ya Mwezi Julai. Mwaka huu 2024, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 400 tangu walipovumbua Masalia ya Mwili wa Mtakatifu Rosalia, mwaliko kwa watu wa Mungu kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, chemchemi ya neema na baraka zote alizomkirimia “Mtume wake Mtakatifu Rosalia Sinibaldi.” Ni Mtakatifu aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na mwaminifu kwa Habari Njema ya Wokovu. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka 4000, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuungana na watu wa Mungu Jimbo kuu la Palermo, kumshukuru Mungu kwa zwadi ya Mtakatifu Rosalia. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Corrado Lorefice, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Palermo, anagusia kuhusu upendo wa Mungu kwa Mtakatifu Rosalia; mwaliko kwa waamini kumwilisha ndani mwao mtindo wa maisha na ushuhuda wake wa Kiinjili.
Mtakatifu Rosalia alikuwa ni mwanamke wa matumaini, asaidie kupyaisha tena miongoni mwa waamini maisha mapya ya kiroho, kwa kuonesha unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili awawezeshe kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukarimu na huruma; awawezeshe waamini kuwa ni Mitume hodari wa Kristo Yesu na wajenzi wa matumaini. Mtakatifu Rosalia aliyaacha malimwengu akaambata tunu msingi za maisha ya Kikristo, akajitenga na malimwengu, akajitahidi kuwa ni Mtawa wa ndani na hivyo kuukumbatia Msalaba wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa wafuasi wa Kristo kufuata tunu msingi za Kiinjili zinazosimikwa katika Injili ya matumaini; chemchemi ya mapendo yanayomegwa kwa ajili ya wengine, ili kushirikishana uzoefu na mang’amuzi haya dhidi ya magonjwa yanayoendelea kumwandama mwanadamu katika historia ya maisha yake.
Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu, kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha mtindo wa maisha ya Kiinjili wa Mtakatifu Rosalia ili kutolea ushuhuda wa imani na mapendo kwa maskini. Palermo ni tajiri wa utamaduni na historia, iliyowachangamotisha watu wa Mungu jimboni humo kuwa na nguvu kiasi hata cha kujisadaka na kujitoa kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Katika shule ya Mtakatifu Rosalia, wamejifunza kuwa ni watu wanaotosheka kwa kiasi, mwaliko na changamoto ya kusimama kidete kupambana na changamoto mamboleo. Huu ni ujasiri unaokita mizizi yake katika Injili ya huduma kutokana na mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, lakini anawakumbusha kwamba, Baba yao wa mbinguni anawatambua fika “kwani hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.” Mt 10:30. Mtakatifu Rosalia anatambua fika shida na mahangaiko ya watu wa Mungu na kwamba, yuko tayari kuwapaka mafuta ya faraja na kupyaisha ari na mwelekeo wao wa maisha. Kwa maombezi na tunza ya Mtakatifu Rosalia, Mwanamke wa Matumaini, Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu Jimbo kuu la Palermo kusimama kidete, tayari kupyaisha Injili ya matumaini kati yao; Jumuiya zao ziendelee kupyaishwa kwa ushuhuda wa damu ya mashuhuda wa imani, ili waweze kuwa ni mwanga angavu wa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu.
Baba Mtakatifu anawahimiza watu wa Mungu Jimbo kuu la Palermo kamwe wasikate wala kujikatia tamaa na matumaini ya maisha. Waendelee kutambua furaha ya faraja inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anayewaita kwake, ili kufurahia matunda ya maridhiano na amani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 400 tangu kuvumbuliwa kwa Masalia ya Mtakatifu Rosalia, itakuwa ni fursa makini kwa maisha ya kiroho kuchanua upya, kwa kuwa wanyenyekevu na wasikivu kwa Roho Mtakatifu, ili kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, tayari kujikita katika Injili ya upendo, ukarimu na huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumtolea Mlinzi na Mwombezi wao yale yote yanayofichika nyoyoni mwao, Mwanamke mwenye kimyaa kikuu, atawasikiliza na kuwaombea nguvu na ujasiri wa kushinda woga na wasiwasi zao, hali ya kukata na kujikatia tamaa, ili waweze kuwa kweli Mitume wenye ari na mwamko na wajenzi wa matumaini. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka watu wote wa Mungu Jimbo kuu la Palermo, chini ya ulinzi na tunza ya Watakatifu wote wanaopamba Kisiwa cha Sicilia! Sancta Rosalia! Ora Pro Nobis.