Tafuta

Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii kuanzia tarehe 3-hadi 7 Julai 2024 linanogeshwa na kauli mbiu: “Demokrasia Inahitaji Ujirani. Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii kuanzia tarehe 3-hadi 7 Julai 2024 linanogeshwa na kauli mbiu: “Demokrasia Inahitaji Ujirani.   (ANSA)

Juma la 50 la Wakatoliki wa Italia Kijamii: Mafundisho Jamii ya Kanisa

Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu maadili ambayo ni dira ya maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwenyeheri Professa Giuseppe Toniolo, Baba wa Familia, Jaalimu wa siasa za kiuchumi toka Chuo kikuu cha Pisa, mwamini makini aliyeacha harufu ya utakatifu katika maisha ya kijamii nchini Italia ndiye Muasisi wa Maadhimisho ya Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii, ambalo kwa Mwaka 2024 limeingia katika awamu yake ya 50 tangu kuanzishwa kwake: Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii kuanzia tarehe 3-hadi 7 Julai 2024 linanogeshwa na kauli mbiu: “Demokrasia Inahitaji Ujirani. Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; Rerum Novarum.

Mafundisho Jamii ya Kanisa: Mazingira Nyumba ya Wote
Mafundisho Jamii ya Kanisa: Mazingira Nyumba ya Wote

Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, katika Waraka wake kuhusu Masuala ya Kijamii Centesimus Annus, alifafanua kwa kina kuhusu asili ya haki msingi za binadamu; umuhimu wa kukuza na kudumisha upendo na mshikamano miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, kama inavyojidhihirisha katika Waraka wake wa “Sollicitudo Rei Socialis” cheche ya uanzishaji wa vyama vya kitume kijamii vilivyokuwa vinapania kulinda na kutetea uhuru, utu na haki msingi za binadamu. Itakumbukwa kwamba, uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu ni muhtasari wa haki zote za binadamu. Dini zisaidie kujenga amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na vita. Kanuni maadili na utu wema ni sehemu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu zinazopaswa kulindwa ili amani na utulivu viweze kushika kasi, bila kusahau nafasi na dhamana ya uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kufahamu vyema kweli za imani yao ili wasiyumbishwe, bali wasimame kidete kuilinda na kuitetea kwa ajili ya ustawi, mafao ya maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 anasema amani ni sawa na matumaini yanayosongwa na changamoto pamoja na magumu yanayowaandama walimwengu, hasa kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka na matokeo yake ni matumizi mabaya ya madaraka na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Siasa safi ni nyenzo inayosaidia ujenzi wa huduma kwa binadamu, lakini ikitumiwa vibaya inaweza kuwa ni chombo cha dhuluma, mipasuko na hatimaye kusababisha madhara makubwa kwa jamii. Baba Mtakatifu anasema siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbali mbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi.

Maadhimisho ya Juma la 50 la Wakatoliki wa Italia Kijamii
Maadhimisho ya Juma la 50 la Wakatoliki wa Italia Kijamii

Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri!

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia

Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vigezo muhimu sana wakati wa kufanya chaguzi mbali mbali, ili kuhakikisha kwamba, haki, dhamana na wajibu vinatekelezwa kikamilifu. Siasa safi ni chombo cha huduma ya amani inayosimikwa katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa vizazi kuheshimiana na kuthaminiana. Vilema vya wanasiasa vinajionesha katika maisha ya hadhara, kwenye taasisi wanazohudumia pamoja na utunzaji bora wa mazingira; mambo yanayoweza kuwafanya watu kumwamini mwanasiasa, katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati yake kama kielelezo cha demokrasia. Vinginevyo, wanasiasa wanaoelemewa na vilema vyao ni hatari sana katika kujenga na kukuza demokrasia jamii. Hawa ni watu ambao “wamepekenywa” kwa rushwa na ufisadi; watu wasioheshimu wala kujali utawala wa sheria; ni watu wenye uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka; ni wachochezi wa ubaguzi na hofu miongoni mwa jamii wala utunzaji bora wa mazingira kwao si kipaumbele, lakini matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao ya wengi. Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao, tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Amani ni sawa na matumaini yanasongwa na changamoto nyingi
Amani ni sawa na matumaini yanasongwa na changamoto nyingi

Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza.” Hizi ni dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija wala mashiko badala ya kukuza umoja na udugu, wao wanakuwa ni sumu ya kusambaratisha watu. Jamii inawahitaji wajenzi wa amani, watakaokuwa ni watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuna haja ya kukataa kishawishi cha vita na mbinu mkakati wa vitisho; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Matumizi ya nguvu ni kinyume cha kanuni maadili inayopania suluhu ya amani na utulivu. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaotumia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kuwa ni mbinu mkakati wa kujijenga kisiasa kwa kuwashutumu wakimbizi na wahamiaji kuwa ni sababu ya umaskini na majanga yanayowaandama watu wao. Ikumbukwe kwamba, amani ya kweli inafumbatwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni ushuhuda wa urithi wa utajiri wa kimaadili kizazi baada ya kizazi! Watoto wanaoishi katika maeneo ya vita, vurugu na kinzani wanapaswa kulindwa na haki zao msingi na utu wao kuheshimiwa na kamwe wasipelekwe mstari wa mbele kama chambo cha vita kwani wao ndio leo na kesho ya binadamu.

Juma la Wakatoliki wa Italia
04 July 2024, 14:41