Tafuta

Kongamano la kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Marekani 17-21 Julai 2024. Kongamano la kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Marekani 17-21 Julai 2024. 

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa USA: Utume, Zawadi Na Umisionari

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 Julai 2024 limeadhimisha Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa lililofanyika kwenye Uwanja wa Lucas Oil. Huu umekuwa ni muda muafaka wa kuchochea moyo wa Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kuabudu Ekaristi Takatifu. Kimekuwa ni kipindi cha uponyaji wa ndani; toba na wongofu wa ndani. Wongofu wa Kiekaristi na Wongofu wa kimisionari ni mambo muhimu kwa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni zawadi; na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha ushirika, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa kujikita katika utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Kumbe, Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayofanywa na Jumuiya ya waamini wa Kanisa mahalia mintarafu Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia ya kuendelea kuzungumza na Kristo Yesu katika safari ya maisha ya waamini. Ni muda wa kuimarisha katekesi kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi angavu na endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu.

Kardinali Lui Antonio Golkim Tagle, akifunga Kongamano la Ekaristi USA
Kardinali Lui Antonio Golkim Tagle, akifunga Kongamano la Ekaristi USA

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, kuanzia tarehe 17 hadi tarehe 21 Julai 2024 limeadhimisha Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa lililofanyika kwenye Uwanja wa Lucas Oil. Huu umekuwa ni muda muafaka wa kuchochea moyo wa Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kuabudu Ekaristi Takatifu. Kimekuwa ni kipindi cha uponyaji wa ndani; toba na wongofu wa ndani. Katika maadhimisho haya Baba Mtakatifu Francisko aliwakilishwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Kardinali Tagle ameongoza ujumbe wa watu wawili ambao ni: Mheshimiwa Padre Michael Fuller, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB pamoja na Mheshimiwa Padre Jorge Torres, Katibu Mtendaji, Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB kwa Ajili ya Wakleri, Watawa na Miito. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, baada ya kuwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, katika mahubiri yake ajilikita katika: Utume na zawadi; Uwepo hai wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai na mwisho ni Ekaristi na Umisionari. Baba Mtakatifu katika salam zake, amewataka watu wa Mungu nchini Marekani kujikita katika wongofu wa kiekaristi na wongofu wa kimisionari, kwa sababu wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu alitumwa na Baba wa milele kuyafanya mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na kwamba Yeye ni Mkate ulioshuka kutoka mbinguni.

Kongamano la 10 la Ekaristi Takatifu Kitaifa
Kongamano la 10 la Ekaristi Takatifu Kitaifa

Ni katika muktadha huu, anasema Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle kwamba, umisionari ni zawadi na sadaka binafsi kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu: Kristo mwenyewe anasema, huu ni “Mwili wangu na hii ni Damu yangu” kwa ajili yenu. Kumbe, Ekaristi Takatifu ni mahali muafaka pa kuonja utume wa Kristo Yesu kama zawadi binafsi, mwaliko na changamoto kwa waamini kupata uzoefu na mang’amuzi haya ya kumwona Kristo Yesu kama kikolezo cha ujenzi wa umoja na mafungamano kati yao na hasa pale wanaposhiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya jirani zao! Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi mang’amuzi ya uwepo angavu wa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai. Tangu mwanzo, hata wanafunzi wake walikuwa na mashaka ya kumwamini, kwani wengi wao walimtambua kuwa ni Mwana wa Yosefu na Maria, kiasi kwamba, wakaamua kumgeuzia kisogo na kurejea kwenye njia zao za awali, badala ya kumsindikiza Kristo Yesu! Walishindwa kukubali zawadi ya Kristo Yes una hivyo kuwa tayari kutumwa kwenda sehemu mbalimbali za dunia kumtangaza na kumshuhudia. Jambo la kujiuliza, ni kwanini baadhi ya waamini wanamkataa Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai? Je, familia zimeendelea kuwa ni kitovu cha kurithisha imani; Je, vijana bado wana kiu ya kumtafuta Kristo Yesu? Kuna watu kutokana na hali na maisha yao wanashindwa kujongea kwa Kristo Yesu. Hawa ni maskini, wakimbizi na wahamiaji, ambao hawana budi kusimama kidete na kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko hai katika maumbo ya Mkate na Divai, hata pale ambapo amejeruhiwa!

Kongamano la Ekaristi Takatifu: Kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa
Kongamano la Ekaristi Takatifu: Kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa

Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, anakaza kusema, kuna uhusiano wa dhati kabisa kati ya Ekaristi Takatifu na Umisionari, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu, Mkate wa uzima ni Mwana wa Mungu aliye hai na nndiye aliyetiwa muhuri na Mwenyezi Mungu. Yn 6: 27-29. Huu ni mwaliko wa kukaa pamoja na Kristo yesu, huku wakiwa huru kutoka katika undani wa maisha yao: Imani na uhakika wa mambo ni zawadi maalum kutoka kwa Kristo Yesu anayewataka wafuasi wake kuishi pamoja naye, huku wakiwa tayari kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumshirikisha Kristo Yesu: magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao, huku Bondeni kwenye machozi na kwa njia hii, wataweza kuonja huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu; atawakirimia upatanisho na amani ya kweli, wote waliovunjika na kupondeka moyo. Waamini wa Kiekaristi ni wale wanaoinjilisha na wako tayari kuinjilishwa. Wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapohitimishwa, waamini wawe tayari kurejea majumbani mwao, ili kuwashirikisha wengine yale waliyosikia, yale yaliyowagusa na yale waliyoonja. Waamini watambue kwamba kwa kushiriki Ibada ya Misa Takatifu, wanampokea Kristo Yesu kama zawadi wanayopaswa kuitangaza na kuishuhudia, kwa furaha na bashasha!

Ekaristi Takatifu USA
22 July 2024, 15:31