Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linajiandaa kuadhimisha Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa litakalofanyika kwenye Uwanja wa Lucas Oil, Indianapolis. Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linajiandaa kuadhimisha Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa litakalofanyika kwenye Uwanja wa Lucas Oil, Indianapolis.   (Carol Percegona)

Kongamano la 10 la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Marekani 17-21 Julai 2024

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linajiandaa kuadhimisha Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa litakalofanyika kwenye Uwanja wa Lucas Oil, Indianapolis kuanzia tarehe 17-21 Julai 2024. Kongamano hili linatarajiwa kuhudhuriwa na waamini zaidi 83, 000 kwa ajili ya Ibada, Katekesi ya kina, Uponyaji, Toba na Wongofu wa ndani. Ni katika muktadha wa Maadhimisho haya, Papa Francisko amemteua Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle kumwakilisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa ni kipindi cha katekesi ya kina kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, Sala na Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inayofanywa na Jumuiya ya waamini wa Kanisa mahalia mintarafu Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama njia ya kuendelea kuzungumza na Kristo Yesu katika safari ya maisha ya waamini. Ni muda wa kuimarisha katekesi kuhusu Sakramenti ya Upatanisho, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi angavu na endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo makini cha imani tendaji. Lina hitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni zawadi; na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha moto wa mapendo kwa Mungu na jirani. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha ushirika, mshikamano na udugu wa kibinadamu kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa kujikita katika utume kwa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni Katekesi ya Msingi Kuhusu Ekaristi Takatifu
Makongamano ya Ekaristi Takatifu ni Katekesi ya Msingi Kuhusu Ekaristi Takatifu

Maadhimisho ya Kongamano la 53 la Ekaristi Takatifu Kimataifa “53rd International Eucharistic Congress” (IEC) yataadhimishwa katika Jimbo kuu la Quito lililoko nchini Ecuador, kuanzia tarehe 8-15 Septemba 2024. Maadhimisho yananogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8. Ujumbe wa udugu wa kibinadamu unagusa masuala mbalimbali ya kijamii, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu ili apate kuwaganga na kuwaponya. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na maadhimisho ya miaka 150 tangu Ecuador ilipowekwa chini ya ulinzi na mambolezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kisima cha huruma na upendo wa Mungu hapo tarehe 25 Machi 1874. Hii ikawa ni nchi ya kwanza kabisa duniani kujiweka chini ya ulinzi na maombezi ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linajiandaa kuadhimisha Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa litakalofanyika kwenye Uwanja wa Lucas Oil, Indianapolis kuanzia tarehe 17-21 Julai 2024. Kongamano hili linatarajiwa kuhudhuriwa na waamini zaidi 83, 000 kwa ajili ya Ibada, Katekesi ya kina, Uponyaji, Toba na Wongofu wa ndani. Ni katika muktadha wa Maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kuwa mwakilishi wake maalum katika Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Marekani. Kardinali Tagle anaongoza ujumbe wa watu watatu ambao ni: Mheshimiwa Padre Michael Fuller, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB pamoja na Mheshimiwa Padre Jorge Torres, Katibu Mtendaji, Tume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB kwa Ajili ya Wakleri, Watawa na Miito.

Papa Francisko: Pyaisheni ushiriki na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu
Papa Francisko: Pyaisheni ushiriki na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu

Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake ya uteuzi anakazia kuhusu umuhimu wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu; Mkate wa Malaika, chemchemi ya maisha ya kiroho, uzima wa milele na wingi wa baraka na neema kutoka mbinguni. Hii ni Karamu inayowaimarisha waamini kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza nyajibu zao za kila siku kwa uaminifu mkubwa. Kardinali Tagle anatumwa, kutimiza huduma hii takatifu kwa mafao ya Kanisa zima. Kongamano hili ni chemchemi ya neema na baraka, wawe tayari kuwamegea na kuwashirikisha jirani zao. Baba Mtakatifu anamtaka Kardinali Tagle kuhimiza Ibada ya nguvu katika kuabudu Ekaristi Takatifu; Ushiriki mkamilifu kwa watu wa Mungu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili iweze kuwaburudisha nyoyoni mwao na kuwapatia ufanisi wa maisha ya kiroho.Itakumbukwa kwamba, Kamati ya Maadhimisho ya Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Marekani, Jumanne tarehe 19 Juni 2023 ilikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake alikazia kuhusu: Ekaristi Takatifu chakula kinachozima njaa ya maisha ya kiroho, Umuhimu wa Kongamano hili katika maisha ya waamini na Kanisa Katoliki nchini Marekani katika ujumla wake. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu utekelezaji wa ukuhani wa waamini wote katika Sakramenti wanasema, waamini wakishiriki sadaka ya Ekaristi Takatifu, iliyo chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo, wanamtolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya kimungu na kujitoa wenyewe pamoja nayo. LG 11. Baba Mtakatifu amewashirikisha wanakamati hawa juu ya ishara iliyofanywa na Kristo Yesu ya kuwalisha watu elfu tano kwa mikate mitano ya shayiri na samaki wawili na hatimaye kuwatangazia kwamba Yeye ndiye chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Rej. Yn 6:51.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Ekaristi Takatifu ni chakula kinachozima njaa ya maisha ya kiroho, ni Kristo mwenyewe kati ya waja wake, anayekuja kuwafariji na kuwaenzi katika hija ya maisha yao ya kiroho. Inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya Wakatoliki wanaiona Ekaristi Takatifu kuwa ni alama na wala si tena uwepo wa Kristo Yesu kwa nguvu ya Neno lake na Roho Mtakatifu; uwepo wake wa upendo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya kongamano la kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Marekani yatasaidia kupyaisha tena mshangao kwa Ekaristi Takatifu, zawadi na sadaka ya Kristo Yesu pamoja na kuchochea tena ile hamu ya waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Hii pia ni njia ya kuragibisha sala kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwani Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Daraja Takatifu ni chanda na pete. Ni fursa kwa waamini kujizatiti kikamilifu na kukoleza ari na mwamko wa kuwa ni Mitume wamisionari tayari kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu waamini wanakutana na Kristo Yesu aliyejisadaka ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumshirikisha maisha na uzima wa milele. Waamini wanakuwa mashuhuda amini wa Kristo Yesu katika furaha na wanapotangaza ukuu na wema wa Kristo Yesu kwa kuwashirikisha na kuwaonjesha upendo majirani. Waamini wanaweza kupata maana ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuonesha huruma, upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu ni fursa nyeti kwa maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Marekani. Hiki ni kipindi cha neema kinachopaswa kuzaa matunda mema, kwa kupyaisha tena imani na matumaini ya watu wa Mungu nchini Marekani. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wajumbe wa Tume ya Kongamano la Kumi la Ekaristi Takatifu Kitaifa chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria pamoja na kuwahakikishia sala na sadaka yake ya maisha.

Kongamano USA

 

 

10 July 2024, 15:19