Tafuta

Kristo Yesu Aliguswa na Uchovu wa Mitume Wake: Mapumziko, Huruma na Huduma

Baba Mtakatifu Francisko:Injili inawafundisha waamini kuzingatia mapumziko, muda wa faragha pamoja na kukuza ndani mwao fadhila ya huruma. Ili kwa kupumzika, waamini waweze kujichotea ari, moyo na nguvu mpya, tayari kuhudumia. Waamini wajifunze kuwa na jicho la huruma litakalowawezesha kujenga utamaduni wa huruma, kwa kujitenga na kutafuta muda wa ukimya, ili waweze kumwabudi Mwenyezi Mungu na hatimaye, kujichotea neema na baraka katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 16 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, Mwinjili Marko kwa namna ya pekee, anapenda kukazia mambo makuu mawili; umuhimu wa wanafunzi wa Kristo Yesu kupata faragha na kupumzika. Pili, ni huruma ya Kristo Yesu kwa umati mkubwa wa watu kwa sababu walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji! Rej. Mk 6:30-34. Mwenyezi Mungu baada ya kukamilisha kazi yake ya uumbaji alijipatia siku ya mapumziko, changamoto kwa binadamu kufurahia siku za likizo na mapumziko ili kupata nafasi ya kutafakari na kujiwekea sera na mikakati kwa siku za usoni. Lakini kutokana na uchu wa mali na faida ya haraka haraka, leo hii binadamu amegeuzwa kuwa ni mtumwa wa kazi na wala hana hata wakati wa kujipumzisha. Ikumbukwe kwamba, Kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, inapaswa kuwa na uhusiano na sehemu nyingine za maisha ya binadamu. Likizo iwe ni fursa ya kuendeleza utamaduni, ari na moyo wa sala katika maisha. Kiwe ni kipindi cha kupyaisha na kunogesha maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili! Likizo ni nafasi muafaka ya kujenga, kukuza na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu, kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, lakini zaidi kwa kuongozwa na Amri Kumi za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha. Ni nafasi ya kutafakari kuhusu Fumbo la maisha ya binadamu, ili kubainisha ikiwa kama maisha yana alama na chapa ya uwepo endelevu na angavu wa Mungu, ambaye kamwe hachoki kuwaongoza waja wake katika mapito ya maisha.

Kristo Yesu alitambua uchovu wa wanafunzi wake akawataka wapumzike
Kristo Yesu alitambua uchovu wa wanafunzi wake akawataka wapumzike

Likizo ni kipindi cha kukuza, kujenga na kudumisha urafiki; umoja na mafungamano ya kifamilia, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika familia ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Wanafamilia watambue kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Likizo ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha katika maisha na vipaumbele vyao, tayari kumfuasa Kristo Yesu bila woga! Waamini wajifunze kutoka kwa Bikira Maria, kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Likizo ni muda muafaka wa kukaa pamoja na wanafamilia wote pale inapowezekana, ili kukazia: makuzi, malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana alama muhimu za ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Likizo ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia nzima. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu ili aweze kuwafunda na kuwapyaisha katika maisha yao ya ndoa na familia. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Likizo ni muda wa: Sala, Neno la Mungu na Matendo ya huruma
Likizo ni muda wa: Sala, Neno la Mungu na Matendo ya huruma

Likizo si wakati wa kumtundika Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vya maisha ya mwanadamu kwani hii, ni hatari kubwa sana! Ni katika muktadha wa likizo au mapumziko, Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 21 Julai 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amekita tafakari yake, kwa kuonesha kwamba, Kristo Yesu alikuwa ameguswa na uchovu wa wanafunzi wake. Kuna hatari kubwa kwa waamini kuzama zaidi katika kazi ili kupata matokeo ya haraka, hali ambayo wakati mwingine inawapelekea kushindwa kuona mambo msingi na hivyo kujichosha bure: kiroho na kimwili. Kumbe, ushauri wa Kristo Yesu kwa wanafunzi wake ni muhimu sana hata kwa maisha na utume sanjari na shughuli za kichungaji. Waamini wanakumbushwa kwamba, wasizame zaidi katika kutenda, kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha. Ushauri unaotolewa na Kristo Yesu kwa wanafunzi wake kupata fursa ya mapumziko, si kwamba, anawaambia kuukimbia ulimwengu, bali ni kujipanga vyema zaidi ili kutoa huduma kwa Kondoo waliotawanyika kana kwamba, hawana Mchungaji mwema, kama Kristo Yesu alivyotenda kwa kuwafundisha mambo mengi. Injili inawafundisha waamini kuzingatia mapumziko, muda wa faragha pamoja na kukuza ndani mwao fadhila ya huruma. Ili kwa kupumzika, waamini waweze kujichotea ari, moyo na nguvu mpya, tayari kuhudumia. Waamini wajifunze kuwa na jicho la huruma litakalowawezesha kujenga utamaduni wa huruma, kwa kujitenga na kutafuta muda wa ukimya, ili waweze kumwabudi Mwenyezi Mungu na hatimaye, kujichotea neema na baraka katika maisha.

Likizo ni muda muafaka wa kujenga mahusiano na Mwenyezi Mungu
Likizo ni muda muafaka wa kujenga mahusiano na Mwenyezi Mungu

Baba Mtakatifu anawauliza waamini ikiwa kama katika harakati za siku, wanatafuta na hatimaye kujipatia muda wa faragha? Je, wanajibidiisha kutafuta muda wa kukaa pamoja na Kristo Yesu? Au daima wamekuwa ni watu wenye pilika pilika kibao? Je? katika siku wamejenga utamaduni wa kutengeneza “Jangwa” nyoyoni mwao katika makelele pamoja na shughuli za siku na hasa katika kipindi hiki cha likizo ya kiangazi. Je, wanajipatia nafasi ya kutafakari matendo makuu ya Mungu katika kazi ya Uumbaji. Wajitahidi kuwashirikisha jirani zao wenye shida na mhangaiko; wajenge na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika sala na Mwenyezi Mungu. Mambo haya yanahitaji watu makiini na waangalifu tayari kuwahurumia watu wengine. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Bikira Maria awasaidie waamini “kupumzika katika Roho” hata “katika pilika pilika nguo kuchanika” katika shughuli za kila siku kwa kuwajibika pamoja na kuonesha huruma kwa watu wengine.

Mapumziko na Huruma
21 July 2024, 14:31

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >