Maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu 11 Julai 2024: Watu Bilioni 1.8
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika Azimio Na.45/216 la Desemba 1990 liliamua kuendelea kuadhimisha Siku ya Idadi ya Watu Duniani, ili kuongeza uelewa wa masuala ya idadi ya watu, ikiwa ni pamoja na mahusiano yao ya mazingira na maendeleo fungamani ya binadamu. Inapania pamoja na mambo mengine kujenga uelewa zaidi wa masuala ya idadi ya watu katika mipango ya nchi zao. Hii inatokana na ukweli kwamba, Idadi ya watu ina athari kubwa katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiuchumi, kimazingira na hata katika maisha ya mtu binafsi. Ni vyema kutambua madhara yake na kuamua kuchukua hatua stahiki. Kwa mara ya kwanza siku hii iliadhimishwa tarehe 11 Julai 1990, miaka thelathini iliyopita katika nchi 90 wanachama wa Umoja wa Mataifa. Maadhimisho haya kwa mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Tumia Nguvu ya Takwimu Jumuishi Kujenga Mustakabali Madhubuti na Wenye Usawa Kwa Wote.” Takwimu za Idadi ya watu hadi kufikia tarehe 10 Julai 2024 ni watu 8,120,508,228 kwa ufupi ni watu bilioni 8.1
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani kwa Mwaka 2024 anasikitika kusema kwamba, shida ya ulimwengu mamboleo sio idadi ya watoto wanaozaliwa ndani yake. Tatizo kubwa ni ubinafsi, uchoyo na ulaji wa kupindukia; unaowafanya watu washibe sana, wawe wapweke na watu wasiokuwa na furaha hata kidogo. #Siku ya Idadi ya Watu Duniani. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres anasema, Mwaka 2024 Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbukizi ya miaka thelathini ya Mpango wa Utendaji wa Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD). Huu ni mwaka wa kuazimia kuharakisha juhudi za uwekezaji ili kugeuza ahadi zake kuwa kweli.
Jambo la msingi katika Mpango wa Utendaji wa Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD) ni utambuzi kwamba afya ya wanawake ya kujamiiana na uzazi na haki za uzazi ni msingi wa maendeleo endelevu. Katika miongo kadhaa tangu kupitishwa, kwa Azimio hili kumepatikana maendeleo makubwa. Wanawake wengi zaidi kuliko hapo awali wanaweza kupata uzazi wa mpango wa kisasa. Vifo vya wajawazito vimepungua kwa asilimia thelathini na nne tangu mwaka wa 2000. Harakati za wanawake na jumuiya za kiraia zimekuwa muhimu katika kuleta mabadiliko haya. Lakini maendeleo yamekuwa hayako sawa na wala si thabiti. Inasikitisha kuona kwamba katika karne ya ishirini na moja, takribani wanawake 800 wanafariki dunia kila siku bila sababu kutokana na ujauzito au wakati wanapojifungua. Idadi hii ni kubwa zaidi katika Nchi Zinazoendelea Dunian.
Sheria bado hazijashika mkondo wake barabara katika muktadha wa kukabiliana na changamoto ya masuala ya ukeketaji ambao kimsingi ni kinyume cha haki msingi za binadamu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres anasema, kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Idadi ya Watu Duniani: “Tumia Nguvu ya Takwimu Jumuishi Kujenga Mustakabali Madhubuti na Wenye Usawa Kwa Wote” inaikumbusha Jumuiya ya Kimataifa kuwekeza zaidi katika mchakato wa ukusanyaji wa takwimu muhimu za idadi ya watu duniani, ili kuelewa matatizo, urekebishaji wake; suluhu na hatimaye, kupata mchakato wa maendeleo ya haraka. Kumbe, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa hazina budi kutenga fedha ya kutosha kwa ajili ya kukusanya takwimu. Anaendelea kutoa wito kwa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutumia kikamilifu Mkutano wa Kilele, baadaye Mwaka huu wa 2024 ili kupata mitaji nafuu kwa ajili ya maendeleo fungamani ya binadamu.