Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 11 Julai 2024 amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Antonij wa Jimbo kuu la Volokolamsk, Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi tarehe 11 Julai 2024 amekutana na kuzungumza na Askofu mkuu Antonij wa Jimbo kuu la Volokolamsk,  (Vatican Media)

Majadiliano ya Kiekumene ni Sehemu ya Vinasaba Vya Maisha na Utume wa Kanisa

Ni katika muktadha wa majadiliano ya kiekumene, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 11 Julai 2024 jioni amekutana kwa faragha na kuzungumza na Askofu mkuu Antonij wa Jimbo kuu la Volokolamsk, ambaye pia ni Rais wa Idara ya Mahusiano ya Kikanisa, Upatriaki wa Moscow. Kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Francisko alikutana na Askofu mkuu Antonij wa Jimbo kuu la Volokolamsk tarehe 5 Agosti 2022 mara tu baada ya kuteuliwa kushika nafasi hii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utengano kati ya Wakristo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo Yesu na ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuona kwamba, Kanisa Katoliki linaendeleza majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma. Anasema uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa.

Majadiliano ya kiekumene ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa
Majadiliano ya kiekumene ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume. Ni katika muktadha wa majadiliano ya kiekumene, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 11 Julai 2024 jioni amekutana kwa faragha na kuzungumza na Askofu mkuu Antonij wa Volokolamsk, Rais wa Idara ya Mahusiano ya Kikanisa, Upatriaki wa Moscow. Kwa mara ya kwanza Baba Mtakatifu Francisko alikutana na Askofu mkuu Antonij wa Jimbo kuu la Volokolamsk tarehe 5 Agosti 2022 mara tu baada ya kuteuliwa kushika nafasi hii.

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa
Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa

Tarehe 15 Septemba 2022 wakakutana tena huko Nur-Sultan, wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Saba la Viongozi Wakuu wa Dini Duniani na Dini za Jadi kuanzia tarehe 13-15 Septemba 2022, kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Mchango wa Viongozi wa Dini Duniani na Dini za Jadi katika mchakato wa maendeleo ya kijamii na kiroho baada ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.” Hii ilikuwa ni hija ya 38 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa, lengo likiwa ni kuendelea kuragibisha mchakato wa majadiliano ya kidini kwa ajili ya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Baba Mtakatifu Francisko katika hija hii alikuwa ni hujaji wa majadiliano, amani na matumaini kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Kazakhstan. Tarehe 3 Mei 2023 Askofu mkuu Antonij wa Volokolamsk, Rais wa Idara ya Mahusiano ya Kikanisa, Upatriaki wa Moscow alifika mjini Vatican ili kukutana na kuzungumza na viongozi kadhaa wa Mabaraza ya Kipapa.

Majadiliano ya kiekumene
12 July 2024, 14:36