Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linataka kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linataka kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa  (Vatican Media)

Mchakato wa Upatanisho wa Kitaifa Canada Unaosimikwa Katika Toba na Wongofu wa Ndani

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakoleza mchakato wa upatanisho unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; kwa kuzingatia ukweli na uwazi, kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada, miaka miwili baada ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada, limewaandikia waamini barua kuonesha upyaisho katika kukoleza mchakato wa wongofu, uponyaji na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Kitume ya 37 ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa nchini Canada kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 30 Julai 2022 ilinogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo hasa lilikuwa ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; kwa kuzingatia ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Baba Mtakatifu, kwa niaba ya Mama Kanisa aliomba tena msamaha unaopania kuleta mwanga angavu wa hija ya: toba, wongofu wa ndani, matumaini na upatanisho wa Kitaifa. Nia ni kuleta utakaso wa kumbukumbu na hatimaye, kuendelea kujikita katika uinjilishaji wa kina unaosimikwa katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu.  Papa Francisko alikazia kuhusu: Hija ya upatanisho, kumbukumbu ya tamaduni, mila na desturi njema za watu asilia wa Canada, Upatanisho na Uponyaji wa Kitaifa, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini inayosimikwa katika utamadunisho, ili kupyaisha kumbukumbu, unabii, mahusiano na mafungamano ya dhati kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya.

Maaskofu Katoliki Canada: Hija ya upatanisho, toba na wongofu wa ndani
Maaskofu Katoliki Canada: Hija ya upatanisho, toba na wongofu wa ndani

Baba Mtakatifu anasema, alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na watu asilia wa Canada, ili kuonesha uwepo na ukaribu wake; masikitiko na machungu yaliyotanda katika sakafu ya moyo wake kwa nyanyaso, dhuluma na mauaji ya kimbari yaliyotendwa na Wakristo na kati yao wakiwemo Wakatoliki dhidi ya watu asilia wa Canada. Taasisi hizi za kidini zilishirikiana kwa karibu sana na Serikali za kikoloni kuwanyanyasa watu asilia wa Canada. Familia ya Mungu nchini Canada imeanza mchakato wa safari ambayo Mama Kanisa alikwisha ianzisha kitambo pamoja na watu asilia wa Canada, kwa kutembea pamoja, kama kauli mbiu ya hija ya 37 ya Kimataifa nchini Canada ilivyokazia. Hii ni safari ya kutembea pamoja: uponyaji na upatanisho; kwa kutambua madhara yaliyotendeka katika historia; kuwasikiliza wahanga, ili hatimaye, ili kwa kuongozwa na dhamiri adilifu, waweze kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na mwelelekeo mpya wa mawazo. Lakini pamoja na dhuluma na nyanyaso walizowatendea watu asilia wa Canada, ndani ya Kanisa kuna waamini waliosimama kidete, wakaonesha ujasiri wa kutangaza na kushuhudia: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wakajifunza tamaduni, lugha, mila na desturi zao njema kama sehemu ya mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu kati ya watu asilia wa Canada. Inasikitisha kuona kwamba, katika mchakato wa utamadunisho kuna baadhi ya waamini walikwenda kinyume cha tunu msingi za Kiinjili, utu na heshima ya binadamu.

Safari ya upatanisho, toba na wongofu wa ndani
Safari ya upatanisho, toba na wongofu wa ndani

Katika muktadha wa hija yake ya kitume nchini Canada, Baba Mtakatifu alikazia mambo makuu mawili yanayopaswa kuzingatiwa. Waamini watambue kwamba, wao ni watoto wa historia inayopaswa kulindwa na kudumishwa, hatimaye, kuirithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Pili watambue kwamba, wao ni wadau muhimu sana katika kuandika historia ya maisha na utume wao ambayo kimsingi bado haijaandikwa, kwani wao ni chemchemi ya maisha, tayari kumkaribisha Kristo Yesu, ili kutangaza na kushuhudia uwepo wake angavu kati pamoja nao! Sasa ni wakati wa kujizatiti katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa, na kuendelea kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, ndugu zao na historia yao katika ujumla wake. Waendelee kutembea kifua mbele katika mwanga wa maisha unaowawezesha kuwa huru, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano kati ya wazee na vijana wa kizazi kipya sanjari na kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.

Kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu
Kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili ya Kristo Yesu

Baada ya kuomba msamaha, hatua ya pili ilikuwa ni kunogesha mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Dominika, Siku ya kwanza ya Juma, ni njia ya upatanisho, inayotoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu Mfufuka, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini hata katika mazingira ambamo hakuna tena chembe ya matumaini. Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu yake azizi, kiwe ni chanzo na kilele cha maisha ya waamini. Kristo apewe nafasi ya kushirikiana na waja wake: maisha, udhaifu na matumaini yao, ili aweze kuwanyanyua tena; kuwaganga na kuwaponya, hatimaye, kuwapatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Na wao wakisha kupatanishwa na Mungu wageuke na kuanza kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya upatanisho na amani katika jamii inayowazunguka. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye amani, chanzo cha upatanisho na ushirika kati yao, ili waweze kuwa wamoja kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Rej. Efe 2: 14. Kumbe, kuna haja pia ya kusimama kidete kutangaza Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baada ya kuomba msamaha hatua ya pili ni toba na wongofu wa ndani
Baada ya kuomba msamaha hatua ya pili ni toba na wongofu wa ndani

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani, uponyaji na upatanisho wa Kitaifa; kwa kuzingatia ukweli na uwazi, kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada, miaka miwili baada ya Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada, limewaandikia waamini barua kuonesha upyaisho wa Kanisa katika kukoleza mchakato wa wongofu, uponyaji, umoja na upatanisho wa Kitaifa, chemchemi ya matumaini mapya. Maaskofu wa Canada wanaendelea kukusanya kiasi cha dola milioni 30 za Canada kwa ajili ya kugharimia miradi inayolenga uponyaji na upatanisho na watu asilia wa Canada. Hadi sasa kiasi cha dola milioni 15 za Canada zimekwisha kusanywa. Watu mbalimbali wanaweza kufanya tafiti na rejea kwenye mapango hifadhi ya Parokia na Majimbo nchini Canada, kwani ukweli na uwazi lazima vitangulie mchakato wa upatanisho: Ni muhimu pia kujenga utamaduni wa majadiliano na kusikiliza; kwa kuendelea kuthamini tunu msingi za maisha ya watu asilia nchini Canada. Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linawaalika watu wote wa Mungu nchini Canada kujikita katika safari ya umoja na matumaini inayofumbatwa katika: Amani, ukweli na uwazi; Unyenyekevu, huruma na upendo; Uvumilivu, imani na kuheshimiana. Maaskofu Katoliki nchini Canada wanawapongeza na kuwashukuru wale wote wanaojikita katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa Kitaifa.

Upatanisho Canada

 

 

 

29 July 2024, 14:51