Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 Iwe ni Fursa ya Kujenga Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza ilifanyika kunako Mwaka 776 Kabla ya Kristo, huko mjini Olympia, nchini Ugiriki. Haya yalikuwa ni mashindano kwa ajili ya wanamichezo mahalia tu na wala hayakuwa na umaarufu wowote Kimataifa. Lakini kadiri muda ulivyokuwa unazidi kuyoyoma, michezo mingi zaidi iliendelea kuongezwa katika mashindano haya, kiasi kwamba, hata muda wa mashindano yenyewe ukaongezeka maradufu. Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo nchini Ugiriki. Kumbe tangu mwanzo, tunu ya amani na maridhiano imekuwa ni kati ya mambo yanayotiliwa mkazo wakati wa michezo ya Olimpiki. Michezo hii ilianza kupata umaarufu wa pekee mara baada ya utawala wa Kirumi kuanza kushika hatamu za uongozi nchini Ugiriki. Hapa Ukristo ukatambuliwa rasmi kwamba, ndiyo dini iliyokuwa inaongoza kwenye utawala wa Kirumi. Wakati wote huu, michezo hii ilionekana kuwa na sura ya kipagani zaidi na wala hakuna masuala ya kidini yaliyogusiwa wakati huo. Kunako mwaka 393 Baada ya Kristo wakati wa Michezo ya Olimpiki huko Thesalonike, kulitokea maafa makubwa yaliyopelekea Mfalme Theodor wa kwanza kusitisha michezo hiyo! Hapa kukawa ni mwanzo wa kuyumba na kuchechemea kwa historia ya michezo ya Olimpik iliyokuwa imedumu kwa takribani Karne moja Kabla ya Kristo! Mwaka 1894 Bwana Pierre de Coubertin akajitosa kuhamasisha tena michezo hii miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuanzisha mashindano ya michezo mbalimbali, ikiongozwa na kauli mbiu iliyojulikana kwa lugha ya Kilatini kuwa ni "Citius, Altius, Fortius" yaani, Kasi, hapa Waswahili wangesema "Mchomoko", Lenga juu zaidi na kwa nguvu." Lengo kuu likiwa ni mchakato wa ujenzi wa mahusiano na mafungamano miongoni mwa vijana nchini Ufaransa.
Mashindano ya Olimpiki yameendelea kuboreka mwaka hadi mwaka. Lakini pia yamekuwa yakikabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo za ulinzi na usalama wa wanamichezo na watazamaji wanaohudhuria katika mashindano haya. Hii ni dhamana nyeti sana kwa wenyeji wa mashindano haya na kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Ndiyo maana kuna hatua kali sana za kinidhamu zinazochukuliwa ili kuwa na ulinzi makini zaidi hasa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi sehemu mbalimbali za dunia. Baadhi ya wafanyabiashara haramu ya dawa za kulevya wamekuwa wanataka kutumia mwanya wa michezo hii ya Kimataifa kwa ajili ya kueneza biashara haramu ya matumizi ya dawa za kulevya, matukio yanayowahusisha wanamichezo wenyewe, kiasi cha kukiuka malengo na kanuni za michezo. Kashfa hizi zimekuwa ni aibu kwa wanamichezo na nchi wanamotoka pale inapobainika kwamba, ushindi walioupata ni kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Michezo hii imeongeza pia kasi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaowatumbukiza wanawake na wasichana katika utumwa na utalii wa ngono. Mama Kanisa anaona kwamba, matukio kama haya ni mahali muafaka pa kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Ndiyo maana mikakati ya maisha ya kiroho kwa ajili ya wanamichezo na mashabiki wao inapewa kipaumbele cha pekee, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa mwili na roho! Hii ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na upendo wa udugu wa kibinadamu pamoja na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.
Tayari wanamichezo watakaoshiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024 wamekwishakujinoa kikamilifu, huku wakila kiapo cha kushinda! Pale wanaposhindwa, walau waoneshe ujasiri kwamba, wamejaribu. Michezo ni jambo jema: kiroho na kimwili, kwani inawasaidia watu kuboresha hali yao ya maisha. Mazoezi ya kila siku ni sehemu ya sadaka inayomwezesha mwanamichezo kujenga kipaji cha uvumilivu na udumifu; yanampatia mwanamichezo nguvu na ujasiri ili kukuza na kudumisha vipaji ambavyo pengine vingeendelea “kuchapa usingizi.” Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbalimbali za maisha ili kuweza kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Michezo ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu na furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo. Michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbalimbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu wa kibinadamu kati ya watu; kukuza na kudumisha maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo. Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, yamekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.
Ikumbukwe kwamba, kiini cha michezo ni furaha; inayofumbatwa katika mazoezi, kwa kuwa pamoja na kuendelea kushirikishana na kufurahia karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kumkirimia mwanadamu kila kukicha! Kuna tabasamu la kukata na shoka pamoja na nyuso za furaha pale wanamichezo wanaposhinda, lakini furaha ya kweli inajionesha anasema Baba Mtakatifu Francisko, pale wanamichezo wanapovuka hali yao na kutambua kwamba, kweli wanahitaji kufurahia. Watu wengine wanaweza kujifunza kutoka kwao kufurahia pamoja na wengine, hata matukio madogo madogo katika maisha. Hii inatokana na ukweli kwamba, maisha ni matakatifu na kila mtu ni zawadi na kwamba, watu kuingizwa katika jamii ni utajiri mkubwa. Huu ndio ujumbe kwa walimwengu; ulimwengu pasi na mipaka wala mtu awaye yote kutengwa! Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024 itaanza kutimua vumbi Ijumaa tarehe 26 Julai hadi Jumapili tarehe 11 Agosti 2024 na Michezo ya Olimpiki Kwa Ajili ya Walemavu itaanza rasmi tarehe 28 Agosti hadi tarehe 8 Septemba 2024. Jiji la Paris, Ufaransa ndiye mwenyeji wa Michezo ya 33 ya Olimpiki, moja ya matukio makubwa ya michezo ulimwenguni inayotarajiwa kuwashirikisha wanamichezo bora kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo nchini Ugiriki. Kumbe tangu mwanzo, tunu ya amani na maridhiano imekuwa ni kati ya mambo yanayotiliwa mkazo wakati wa michezo ya Olimpiki. Ni katika muktadha wa umuhimu wa kujenga na kudumisha amani na utulivu, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 21 Julai 2024 ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha vita na kuonesha utashi wa kutaka kujikita katika ujenzi wa amani. Michezo ya Olimpiki iwe ni fursa ya kuwakutanisha watu kutoka katika tamaduni mbalimbali, kielelezo cha ujenzi wa ulimwengu shirikishi. Ushuhuda unaotolewa na wanamichezo uwe ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya.