Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2024 anakita mawazo yake kwa viongozi wa siasa. Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2024 anakita mawazo yake kwa viongozi wa siasa. 

Nia za Baba Mtakatifu Kwa Mwezi Agosti 2024: Viongozi wa Siasa

Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2024 anakita mawazo yake kwa viongozi wa siasa, ambao katika ulimwengu mamboleo wengi wao wanaelemewa na: Rushwa, Kashfa na wanapenda kukaa mbali na watu wao. Mtakatifu Paulo wa VI anasema, siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo katika jamii kwani inalenga ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anazungumzia SIASA kwa Herufi kubwa: Mafao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siasa safi ni msingi wa maendeleo endelevu na fungamani; demokrasia shirikishi na uongozi bora unaojikita katika hoja zenye mvuto, mashiko na huduma kwa wananchi. Siasa safi inafumbatwa katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; yanayowashirikisha wadau mbalimbali katika jamii; marika pamoja na tamaduni, daima wakijitahidi kujenga imani kati yao kama sehemu ya kukuza na kudumisha amani.  Siasa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu na kwamba, siasa safi hutekelezwa kwa kufuata katiba, sheria na kanuni maadili; mambo msingi katika kukuza na kudumisha misingi ya: haki. amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Paulo wa VI anasema, siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo katika jamii; ni matunda ya ukomavu yanayojikita katika uongozi bora, maridhiano, utawala wa sheria, uvumilivu, uaminifu na bidii. Kamwe tofauti za kiitikadi kisiwe ni chanzo cha vita, kinzani, vurugu na mipasuko ya kijamii inayowatumbukiza watu kwenye majanga na maafa makubwa! Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2019 ulinogeshwa na kauli mbiu “Siasa safi ni huduma ya amani.” Siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbalimbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo!

Siasa safi ni huduma muhimu sana kwa ujenzi wa amani duniani
Siasa safi ni huduma muhimu sana kwa ujenzi wa amani duniani

Baba Mtakatifu anasema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri! Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vigezo muhimu sana wakati wa kufanya chaguzi mbali mbali, ili kuhakikisha kwamba, haki, dhamana na wajibu vinatekelezwa kikamilifu. Siasa safi ni chombo cha huduma ya amani inayosimikwa katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa vizazi kuheshimiana na kuthaminiana. Vilema vya wanasiasa vinajionesha katika maisha ya hadhara, kwenye taasisi wanazohudumia pamoja na utunzaji bora wa mazingira; mambo yanayoweza kuwafanya watu kumwamini mwanasiasa, katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati yake kama kielelezo cha demokrasia. Vinginevyo, wanasiasa wanaoelemewa na vilema vyao ni hatari sana katika kujenga na kukuza demokrasia jamii.

Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo kwa jamii
Siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo kwa jamii

Ni watu ambao “wamepekenywa” kwa rushwa na ufisadi; watu wasioheshimu wala kujali utawala wa sheria; ni watu wenye uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka; ni wachochezi wa ubaguzi na hofu miongoni mwa jamii; wala utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwao si mali kitu, lakini matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana kwa kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya: Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao, tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Siasa safi inayojikita katika ujenzi wa amani inatambua karama za watu na inaendeleza majadiliano na watu kuaminiana na kuthaminiana badala ya kuangaliana kwa “jicho la kengeza.” Hizi ni dalili za ubinafsi unaofumbatwa katika dhana ya utaifa usiokuwa na tija wala mashiko badala ya kukuza umoja na udugu wa kibinadamu, wao wanakuwa ni sumu ya kusambaratisha watu. Jamii inawahitaji wajenzi wa amani, watakaokuwa ni watangazaji, mashuhuda na vyombo vya wema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake ambaye anawatakia watoto wake furaha.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Baba Mtakatifu Francisko katika Nia zake za jumla kwa Mwezi Agosti 2024 anakita mawazo yake kwa viongozi wa siasa ambao katika ulimwengu mamboleo wengi wao wanaelemewa na: Rushwa, Kashfa na wanapenda kukaa mbali na watu wao. Mtakatifu Paulo wa VI anasema, siasa safi ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huduma ya upendo katika jamii kwani inalenga ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anazungumia “SIASA” kwa herufi kubwa: Siasa inayosimikwa katika utamaduni wa kusikiliza na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Siasa inayoshughulikia ukosefu wa fursa za ajira na mapumziko kwa Dominika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumshukru Mungu kwa kuwakirimia wanasiasa wakweli na waaminifu wanaotekeleza dhamana na wito wao kwa kuusimika katika huduma na wala si katika uchu wa mali na madaraka; wanasiasa wanaochakarika kutafuta na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuungana naye pamoja ili kuwaombea wanasiasa, waweze kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa wananchi wao; tayari kujikita katika maendeleo fungamani; ustawi na mafao ya wengi; kwa kuwaangalia na kuwashughulikia wale waliopoteza fursa za ajira. Nia za Baba Mtakatifu Francisko zinasambazwa sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya Mtandao wa Sala Kimataifa.

Nia Mwezi Agosti 2024
30 July 2024, 15:43