2024.07.17 Papa Francisko akiwa mbele ya Picha ya Maria wa Bandari mnamo tarehe 29 Mei 2016 2024.07.17 Papa Francisko akiwa mbele ya Picha ya Maria wa Bandari mnamo tarehe 29 Mei 2016 

Papa Francisko:mjali na kukuza thamani ya kuwakaribisha maskini na wadhaifu!

“ombeni amani,kuweni wajenzi wa amani hasa katika Jumuiya zetu,jipatanishe na kupatanishwa.Mfano wa maisha kidugu yawe ya kiinjili yanayovutia waamini mnaowaelekeza huduma za kichungaji.”Ni Ujumbe wa Papa kwa Padre Piccolo,Mkuu wa Shirika la Watawa wa Mama wa Mungu katika tukio la maadhimisho ya miaka 1500 ya Ibada ya Mtakatifu Maria Bandari salama ya kirumi.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumatano tarehe 17 Julai 2025 ametuma Barua kwa Padre Antonio Piccolo, Mkuu wa Shirika la Watawa wa Kawaida wa Mama wa Mungu katika tukio la maadhimisho ya miaka 1500 ya Ibada kwa heshima ya Mtakatifu Maria Bandari Salama  ya Kirumi(Romanae Portus Securitatis, na Msimamizi wa Mji wa Milele (yaani Roma). Katika barua hiyo anabainisha kwamba ni fursa nzuri ya kuungana katika sala kwa familia yao ya kitawa ambapo tangu 1601 walijikabidhi chini ya Ulinzi wake, shirika lililotaka kuinua sifa kwake, Mama wa upendo na mwororo, taa angavu ambayo iliwafikisha wanae katika bandari salama. Baba Mtakatifu kwa njia hiyo amewalekeza  wazo zuri kwa kila mmoja na wale wote wanaoshiriki tukio kubwa la maana kwa Kanisa zima la Roma. Kwa neema ya Mungu sherehe yao inakwenda sambamba na mwaka 2024 ambao ni wa maandalizi ya Jubilei ya Matumaini. Ni kipindi maalum cha neema ambacho wanaadhimisha pia miaka 450 tangu kuanzishwa kwa shirika lao na Mtakatifu Yohane Leonardi, aliyekuwa na ibada kuu kwa Mama wa Mbingu, kama mlinzi amini wa karama ya Leonardi.

Kuanzishwa kwa ibada ya Maria bandari salama

Papa katika ujumbe huo amekazia kusema kuwa Ibada ya Mtakatifu Maria wa Bandari ilianzishwa baada ya muujiza uliooneshwa na Mama wa Mungu kunako tarehe 15 Julai mwaka 524 katika nyumba ya Mtakatifu Galla, baba wa kiroma, kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Yohane I. Tangu wakati huo  Bandari, mahali ambapo  baba Galla alikuwa anapokea maskini na mahujaji, ikawa Madhabahu ya Maria, na nafasi ya upendo. Kwa njia hiyo wao kama shirika ni warithi wa kiroho wa Mtakatifu Leonardi ambapo Papa anawaalika watunze na kuhamasisha thamani za utunzaji wa maskini na walio wa mwisho ili mahali ambamo tunaishi na makanisa yake yaweze kuwa bandari iliyo wazi duniani, ambamo inatoa faraja na msaada kwa aina nyingi za umaskini ambazo zinahusiana na kuishi kwetu.

Maria alitokea wakati mgumu wa Kanisa 

Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza kuwa Bikira Maria zaidi ya hayo alitokea wakati maalum mgumu kwa Kanisa, kwa kufunika vazi lake juu ya Papa Yohane I ambaye alisafiri na kufa kwa amani bila kukana imani yake, wakati akiwa mateka wa njama za kisiasa na vita vya kindugu. Mbele ya matukio ya sasa, inawezekaje tusipokee dharura kama ya wakati ule ya kusaidia amani, na kusali kwa ajili ya amani? Papa Francisko kwa hiyo amewaomba kuwa: “ombeni amani, fanyeni kuwa wajenzi wa amani hasa katika Jumuiya zetu, jipatanishe na kupatanishwa. Mfano wa maisha kidugu yawe ya kiinjili yanayovutia waamini ambao mnawaelekeza huduma za kichungaji.” Papa pia amewashauri wamtazame Maria kama ishara ya faraja na tumaini salama, mwenye uso wa mama wa Mungu na kimbilio la wakimbizi; kwake Yeye kiukweli anaendelea kutupatia Mwanae kama kisima pekee cha maelewano, matumaini ya wokovu, njia ya amani, na umuhimu kabisa wa utafiti wa binadamu.

Mtakatifu Yohane Leonardi alianzisha shirika

Katika roho hiyo Papa amesema: “Mtakatifu Yohane Leonardi, mwanafamasia, alianzisha Shirika la Mapadre wa Mwenyeheri Bikira Maria, hasa kwa ajili ya kutoa katika Kanisa chombo cha kitume cha asili. Mtakatifu huyo awali ya yote ndiye aliyewahimiza kumweka Kristo katikati ya yote, Kristo awe kipimo cha Yote. “Kristo ni dawa tu yenye uwezo wa kutibu magonjwa ya Kanisa na ya binadamu.” Shughuli hiyo na Maria ambaye anasindikiza kwa upendo safari ya Shirika linajipyaisha tena leo hii na kuwaita wote kuwa na ari kubwa zaidi ya umisionari na maendeleo endelevu katika maisha ya kiroho, kwa kupokea ushauri wa Mtakatifu Mwanzilishi.  Yeye kwa nguvu zote alisema: “mbele ya macho ya akili na moyo tu ni heshima na utukufu wa Kristo na yeye msulubiwa( Mtakati Yohane Leonardi, Wimbo kwa Msalaba).

Bikira Maria katika Jubilei awakumbushe kazi ya Uinjilishaji

Baba Mtakatifu hatimaye katika barua hiyo anabainisha kuwa, maadhimisho ya kijubilei ambazo wao wanajitayarisha kuadhimisha, chini ya mtazamo wa Bikira Bandari, salama awakumbushe kumbu kumbu ya kazi ya Uinjilishaji wa Mtakatifu Yohane Leonardi, ambaye aliandika hata katika Katiba ya kwanza ya Chuo cha Urbano cha Propaganda Fide, ili kufunda Mapadre wenye uwezo wa kupokea changamoto za kimisionari za wakati. Papa amewatia moyo hata wao ili kuwa na moyo wa mafunzo fungamani ya watawa, katika mchakato endelevu wa mafunzo ya Msulibiwa Mfufuka, wa kwanza wa ubinadamu uliokombolewa(rej. 1Kor 15,20) na kwa kutazama Maria mfuasi wa Kristo na Mama wa Kanisa, utume wao uweze kuwa mkondo wa neema na chombo cha tangazo la furaha ya Injili. Katika matashi hayo, amewakabidhi wote kwa maombezi ya Bikira Maria Mtakatifu, mpendwa anayeombwa kama(‘Romanae Portus Securitatis,’ )‘Bandari Salama ya Kirumi’ na Mtakatifu Yohane Leonardi,  kwa utashi amewatumia baraka ya kibaba akiwaomba pia wasali kwa ajili yake.

Barua ya Papa kwa Padre Piccolo
17 July 2024, 12:33