Papa,Trieste:Mungu amefichwa katika pembe za giza za maisha na miji yetu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika misa iliyoongozwa na Baba Mtakatifufu kwa usaidizi wa Kardinali Matteo Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Italia, Askofu Enrico Trevisi ,Rais wa Tume ya Maandalizi ya Tukio la Kijamii pamoja na Askofu Mkuu Luigi Renna, wa Jimbo Kuu la Trieste, iliudhuriwa na washiriki wa Toleo la 50 la Mafundisho Jamii ya Kanisa nchini Italia na waamini wote wa jimbo hilo, Dominika tarehe 7 Julai 2024. Baba Mtakatifu Francisko akianza mahubiri yake kwa kuongoza na masomo ya Siku amesema “Ili kufufua matumaini katika mioyo iliyovunjika na kusaidia mizigo ya safari, Mungu daima amewaibua manabii kati ya watu wake. Lakini, kama vile Somo la Kwanza lilivyosimulia katika historia ya Ezekieli, mara nyingi walikutana na watu waasi, “watoto wakaidi wenye mioyo migumu”( Eze 2:4 ), nao wakakataliwa. Yesu, pia, alipata uzoefu sawa na manabii. Alirudi Nazareti, nchi yake, kati ya watu wake alipokulia, lakini hakutambuliwa, na hata akataliwa: "Alikwenda kwake, na watu wake mwenyewe hawakumpokea" (Yh 1:11).
Injili inatuambia kwamba Yesu “alikuwa sababu ya kashfa kwao” (Mk 6:3 ), lakini neno “kashfa” halirejei kitu kibaya au kisichofaa kama tunavyo kitumia leo hii; kashfa ina maana ya "kikwazo," kitu ambacho kinazuia na kukwaza kuendelea zaidi. Hebu tujiulize: ni kikwazo gani kinachozuia kumwamini Yesu? Tukisikiliza majadiliano ya wenyeji wenzake, tunaona kwamba yanaishia tu kwenye historia Yake ya duniani, katika asili ya familia yake, na hivyo hawawezi kuelewa jinsi hekima hiyo, na hata uwezo wa kufanya miujiza, ungewezekanakwa mwana wa Yosefu seremala; yaani kutoka kwa mtu wa kawaida. Kashfa, basi, ni ubinadamu wa Yesu. Kizuizi kinachowazuia watu hawa kutambua uwepo wa Mungu ndani ya Yesu ni ukweli kwamba Yeye ni mwanadamu, kwa urahisi Yosefu mwana wa seremala: Mungu na Mwenyezi, anawezaje kujidhihirisha katika udhaifu wa mwili wa mwanadamu? Je, Mungu muweza wa yote na mwenye nguvu, aliyeiumba dunia na kuwakomboa watu wake kutoka utumwani, anawezaje kuwa dhaifu kiasi cha kuja katika mwili na kujishusha ili kuosha miguu ya wanafunzi?
Baba Mtakatifu Francisko amesema, hii ndiyo kashfa: imani iliyojengwa juu ya Mungu wa kibinadamu, anayejishusha chini kwa wanadamu, ambaye anajali, ambaye anachochewa na majeraha yetu, anayechukua uchovu wetu, ambaye kwa ajili yetu amemegwa kama mkate. Mungu mwenye nguvu na uweza ambaye yuko upande wangu na kuniridhisha kwa kila kitu anavutia; Mungu dhaifu, ambaye hufa msalabani kwa sababu ya upendo na Ananiomba nishinde ubinafsi wote na kutoa maisha yangu kwa wokovu wa ulimwengu, ni Mungu asiye na raha. Hata hivyo, tunaposimama mbele ya Bwana Yesu na kutazama changamoto zinazotukabili, masuala mengi ya kijamii na kisiasa yaliyojadiliwa hata katika Juma hii la Kijamii, Papa amesema maisha halisi ya watu wetu na mapambano yao, tunaweza kusema kwamba tunachohitaji leo hii ni kwa hakika hii: kashfa ya imani.
Baba Mtakatifu amebainisha: "Si dini iliyojifungia yenyewe, inayotazama mbinguni bila kujali kinachotokea duniani na kusherehekea ibada hekaluni lakini kusahau vumbi linalovuma katika mitaa yetu. Badala yake, tunahitaji kashfa ya imani, imani iliyosimikwa katika Mungu aliyefanyika mwanadamu na, kwa hiyo, imani ya kibinadamu, imani ya mwili, inayoingia katika historia, inayogusa maisha ya watu, inayoponya mioyo iliyovunjika, ambayo inakuwa chachu ya tumaini na mbegu ya ulimwengu mpya." Ni imani inayoamsha dhamiri kutokana na ulegevu, inayoweka kidole chake katika madonda ya jamii, inayoibua maswali kuhusu mustakabali wa ubinadamu na historia; ni imani isiyotulia ambayo inatusaidia kushinda unyonge na uvivu wa moyo, ambayo inakuwa mwiba katika mwili wa jamii ambayo mara nyingi hupigwa na kulaluliwa.
Zaidi ya yote, imani inayovuruga mahesabu ya ubinafsi wa kibinadamu, inayokemea maovu, inayoonesha udhalimu, inayovuruga mipango ya wale ambao, kwa kivuli cha uwezo, wanacheza na maisha ya wanyonge. "Mshairi wa jiji hili, akielezea katika wimbo wa kawaida kurudi nyumbani kwake jioni, alisema anavuka barabara yenye giza, mahali pa kuoza ambapo watu na bidhaa za bandari ni "detritus," ambayo ni, mabaki ya ubinadamu, bado hapa, anaandika, “nikipita hapo, naona wasio na mwisho katika unyenyekevu,” kwa sababu yule kahaba na baharia, mwanamke mgomvi na askari, “wote ni viumbe vya maisha na maumivu; ndani yao, kama ndani yangu, Bwana husisimua.” (U. SABA, “Città vecchia,” in Il canzoniere (1900-1954) Edizione definitiva, Torino, Einaudi, 1961).
Papa Francisko ameomba wasisahau kuwa: “Mungu amefichwa katika pembe za giza za maisha na miji yetu, uwepo wake unajidhihirisha kwa usahihi katika nyuso zilizo na mateso na ambapo uharibifu unaonekana kuwa wa ushindi. Utovu wa Mungu umefichwa katika taabu ya mwanadamu, Bwana huchochea na kuwa uwepo wa kirafiki kwa usahihi katika nyama iliyojeruhiwa ya angalau, iliyosahauliwa, na kutupwa. Na sisi, ambao nyakati fulani tunakashifiwa bila ya lazima na mambo madogo madogo, badala yake tungefanya vyema kujiuliza: Kwa nini hatukatizwi kashfa katika uso wa uovu uliokithiri, maisha ya kudhalilishwa, masuala ya kazi, mateso ya wahamiaji? Kwa nini tunabaki kutojali na sintofahamu, na dhuluma za ulimwengu? Kwa nini hatuzingatii hali ya wafungwa, ambayo hata kutoka katika jiji hili la Trieste huinua kama kilio cha uchungu?
Papa amesititiza tena kuwa: "Yesu aliishi katika mwili Wake unabii wa maisha ya kila siku, akiingia katika maisha ya kila siku na historia za watu, akidhihirisha huruma ya Mungu ndani ya mambo ya kibinadamu na tete ya wanadamu waliojeruhiwa. Na kwa sababu hiyo, baadhi ya watu walikashifiwa Naye, Akawa kikwazo, Alikataliwa tukio hadi kufikia hatua ya kuhukumiwa; hata hivyo, Alibaki mwaminifu kwa utume Wake, Hakujificha nyuma ya utata, hakuafikiana na mantiki ya mamlaka ya kisiasa na kidini. Alifanya maisha yake kuwa sadaka ya upendo kwa Baba. Vivyo hivyo, sisi Wakristo tumeitwa kuwa manabii na mashahidi wa Ufalme wa Mungu, katika hali zote tunazoishi, katika kila mahali tunapoishi.
"Kutoka mji huu wa Trieste, unaoelekea Ulaya, njia panda ya watu na tamaduni, nchi ya mpakani, Papa amesema - tuimarishe ndoto ya ustaarabu mpya unaosimikwa kwenye amani na udugu; tusiwe na kashfa na Yesu bali, kinyume chake, tuchukie hali hizo zote ambapo maisha yanashushwa hadhi, kujeruhiwa, na kuuawa; tulete unabii wa Injili katika miili yetu, pamoja na chaguzi zetu hata kabla ya maneno yetu. Na kwa Kanisa hili la Trieste, ningependa kusema: Endeleeni mbele” Kwa kuwatia moyo ameongeza kuwa waendelea kuwa mstari wa mbele kueneza Injili ya matumaini, hasa kwa wale wanaowasili kutoka njia ya Balkan na kwa wale wote ambao, kwa mwili au roho, wanahitaji kutiwa moyo na kufarijiwa. Hebu tujitoe pamoja: kwa sababu kwa kugundua kwamba tunapendwa na Baba, tunaweza kuishi kama ndugu.