Papa Francisko kwa watoto wa kituo cha kiangazi,Vatican:amani ni jambo zuri!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Alhamisi tarehe 18 Julai 2024, Baba Francisko akizungumza na watoto walioko kwenye kituo cha kiangazi cha mjini Vatican, ambao ni watoto wa wafanyakazi alizungumzia juu ya thamani ya familia, ya wazazi, ya uhusiano na babu na bibi, huku aliwahimiza kufanya kazi kwa ajili ya amani, kwa sababu “kufanya amani ni jambo zuri zaidi maishani, na kujiandaa kwa Jubile ijayo kwa roho ya furaha.”
Akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari, Msemaji wa Ofisi ya Vyombo vya Habari Vatica Dk. Matteo Bruni, kuhusu ziara hiyo ya Papa Francisko katika Kituo cha Kiangazi alisema kuwa: “Leo asubuhi Baba Mtakatifu Francisko ametembelea kituo cha kiangazi cha watoto, mjini Vatican akiambatana na Padre Franco Fontana, S.D.B., mwenye jukumu la kuandaa Juma za kituo hicho za shughuli za kimwili, kielimu na kiroho. Baada ya salamu fupi na shukrani kwa wafadhili wa Nyumba ya Mtakatifu Marta, Papa alihamia eneo la kituo kidogo cha michezo, kilichojengwa hivi karibuni na kilichokusudiwa kwa watoto wa wafanyakazi, kilichowekwa jina la Mtakatifu Joseph.”
Na baada ya kuwasili, mkutano mfupi ulifanyika na wahuishaji na baadaye Papa Francisko alifanya mazungumzo na watoto na vijana walioshiriki katika kituo cha majira ya joto.” Msemaji wa Vyombo vya habari aidha alibanisha kuwa: “Katika kujibu maswali yao aliyoulizwa kwa kuchochewa na njia ya tafakari na shughuli wanazozifuata siku hizi, Papa Francisko alizungumzia juu ya thamani ya familia, ya wazazi, ya uhusiano na babu na bibi, aliwahimiza “kufanya kazi kwa ajili ya amani, kwa sababu kufanya amani ni jambo zuri zaidi maishani, na kujiandaa kwa ajili ya Jubile ijayo kwa roho ya furaha.”
Hatimaye, baada ya muda wa sala, watoto na vijana wote kwa pamoja walitupa maputo yenye rangi zilizotengenezwa kwa mpira wa asili angani, maputoa ambayo yanaweza kuoza, kila moja likiwa na maneno ya Papa yaliyoandikwa: “Kwa, mvulana mpendwa, kwa, msichana mpendwa, wewe ni mwenye thamani machoni pa Mungu,” kwa kutumaini kwamba ujumbe huo unaweza “kuwafikia watu wengi iwezekanavyo.” Mkutano ulimalizika kwa shukrani za Papa kwa watoto, kwa furaha yao na kwa wale wote waliohusika katika utekelezaji wa mpango huo.