Viongozi wa dini Kimataifa, tarehe 10 Julai 2024 wametia saini wito wa Roma kuhusu Teknolojia ya Akili Mnemba kwa Maadili, mjini Hiroshima. Viongozi wa dini Kimataifa, tarehe 10 Julai 2024 wametia saini wito wa Roma kuhusu Teknolojia ya Akili Mnemba kwa Maadili, mjini Hiroshima. 

Teknolojia ya Akili Mnemba Kwa Ajili ya Kudumisha Amani Na Mafao ya Wengi

Papa Francisko amekazia: Umuhimu wa binadamu katika kuchagua na kuamua kutenda, kwa kuzingatia utu na heshima na kwamba amani haina budi kupewa kipaumbele cha kwanza, teknolojia ya akili mnemba katika vita ni hatari sana, kumbe mchango wa viongozi wa dini ni muhimu sana katika kuratibu ukuaji wa maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba. Teknolojia ya akili mnemba inatumia hali ya binadamu, changamoto kwa binadamu kuwa wazi kwa Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na kanuni maadili ili kujibu changamoto za kijamii zinazoendelea kuibuliwa na maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba kiasi cha kuathiri utu wa binadamu. Teknolojia huzaliwa kwa kusudi na, katika athari zake kwa jamii ya wanadamu, daima huwakilisha aina ya utaratibu katika mahusiano ya kijamii na mpangilio wa mamlaka, hivyo kuwawezesha watu fulani kufanya vitendo maalum huku wakiwazuia wengine kufanya tofauti.  Kwa njia iliyo wazi zaidi au kidogo, mwelekeo huu wa nguvu wa teknolojia daima unajumuisha mtazamo wa ulimwengu wa wale walioivumbua tekenolojia hii na kuiendeleza. Teknolojia ya akili mnemba isaidie kujenga leo na kesho iliyo njema na bora zaidi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, msukumo wa kimaadili ni muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, tarehe 28 Februari 2020 ni kumbukumbu ya kutiwa saini kwa Mkataba wa Ushirikiano unaojulikana kama “Rome Call For Artificial Intelligence” umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili uliowekwa saini kati ya Taasisi ya Kipapa ya Maisha, Kampuni ya Microsoft, Kampuni ya IBM pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organzation of the United Nations"; kifupi: FAO.) Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba watu wote wenye mapenzi mema wataendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na kwamba, maendeleo ni kwa ajili ya wote!

Mji wa Hiroshima: Changamoto ya kujizatiti katika kutafuta na kulinda amani
Mji wa Hiroshima: Changamoto ya kujizatiti katika kutafuta na kulinda amani

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha, tarehe 9 Julai 2024 amefungua Mkutano wa Majadiliano ya Kidini huko Hiroshima, unaowashirikisha wajumbe 150 kutoka Japan, Umoja wa Falme za Kiarabu “United Arab Emirates”, na Israeli na kwamba mkutano huu unafungwa rasmi tarehe 10 Julai 2024. Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Maadili ya Teknolojia ya Akili Mnemba Kwa Amani: Dini za Ulimwengu zinajitolea kwa Wito wa Roma” Artificial Intelligency For Peace: World Religions Commit to the Rome Call.” Katika hotuba yake ya ufunguzi Askofu mkuu Vincenzo Paglia, amekazia umuhimu wa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Teknolojia ya akili mnemba inaendelea kushika kasi ya ajabu katika maendeleo ya binadamu. Mkutano huu umefanyika mjini Hiroshima, nchini Japan mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika kutafuta na kudumisha: haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa. Viongozi wa dini mbalimbali duniani wanahimizwa kushikamana kama ndugu, ili kutoa msukumo wa pekee katika ujenzi wa haki, amani na udugu wa kibinadamu. Viongozi wa kidini wanasema, ni dhamana na wajibu wa viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanashikamana kwa dhati ili kukabiliana na changamoto za maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba; kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema na kwamba, kuna haja ya kuwa na uongozi utakaosimamia kanuni maadili ya teknolojia ya akili mnemba.

Viongozi wa kidini wanao mchango katika kudhibiti akili mnemba
Viongozi wa kidini wanao mchango katika kudhibiti akili mnemba

Viongozi wa dini Kimataifa, tarehe 10 Julai 2024 wametia saini wito wa Roma kuhusu Teknolojia ya Akili Mnemba kwa Maadili, mjini Hiroshima. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa pamoja walimwengu wanaweza kujenga amani, huku wakisaidiwa na teknolojia inayotumika kuwahudumia wanadamu huku wakiendelea kuheshimu utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu unaonogeshwa na kauli mbiu “Maadili ya Teknolojia ya Akili Mnemba Kwa Amani: Dini za Ulimwengu zinajitolea kwa Wito wa Roma” Artificial Intelligency For Peace: World Religions Commit to the Rome Call” amekazia umuhimu wa binadamu katika kuchagua na kuamua kutenda, kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu; amani haina budi kupewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, teknolojia ya akili mnemba katika vita ni hatari sana, kumbe mchango wa viongozi wa dini ni muhimu sana katika kuratibu ukuaji wa maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba. Teknolojia ya akili mnemba inatumia hali ya binadamu, changamoto kwa binadamu wenyewe ni kuwa wazi kwa Mwenyezi Mungu pamoja na binadamu wenzao na kwamba, teknolojia hii inawaelekeza binadamu kwa maendeleo ya siku zijazo. Dhamiri ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu na hekalu la Mungu, ambamo sauti yake inasikika na utimilifu wa sheria hii ni upendo kwa Mungu na jirani.

Mji wa Hiroshima: Changamoto ya ujenzi wa haki, amani na mshikamano
Mji wa Hiroshima: Changamoto ya ujenzi wa haki, amani na mshikamano

Kumbe, teknolojia ya akili mnemba inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma kwa binadamu; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zake msingi; kwa kukazia uhuru na uwajibikaji wake na kwa namna ya pekee ni kujihusisha na kanuni maadili na utu wema. Baba Mtakatifu anawahimiza wajumbe kuwatangazia walimwengu kwamba, viongozi wa kidini wataka kuona kwamba, utu, heshima, haki msingi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanaheshimiwa katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba. Ni hatari sana ikiwa kama teknolojia ya akili mnemba itatumika katika vita, kumbe, haki na amani vinapaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Kwa hakika mji wa Hiroshima unawakumbusha walimwengu madhara makubwa ya vita na kwamba, teknolojia ya akili mnemba inapaswa kudhibitiwa na binadamu. Teknolojia ya akili mnemba ni tete sana, kumbe, kunahitajika utajiri wa mchango kutoka kwa watu mbalimbali pamoja na viongozi wa dini, ili kuratibu maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba, kwa kushirikiana sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Wajumbe wa mkutano huu wametia saini mktaba wa Akili Mnemba kwa Ajili ya Amani. Dini za Ulimwengu zinajitolea kwa Wito wa Roma” Artificial Intelligency For Peace: World Religions Commit to the Rome Call.”

Akili Mnemba
10 July 2024, 14:48