Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana uzoefu na mang’amuzi ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana uzoefu na mang’amuzi ya maisha.  (Vatican Media)

Waheshimuni na Kuwatunza Wazee, Kamwe Msiwatelekeze Kama Daladala Mbovu!

Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana uzoefu na mang’amuzi ya maisha. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani inakuwa ni fursa ya kuboresha mahusiano kati ya kizazi kipya na kile cha zamani kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wazee! Uzee ni Amana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, tarehe 28 Julai 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Sala ya mkongwe “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 anasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanagundua wakiwa wamechelewa kwamba, walishindwa kuwatendea vyema wazee. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawaonea huruma wazee, kwa kuwatembelea mara kwa mara na kuwatia moyo, wale waliovunjika na kupondeka moyo na hivyo kujikatia tamaa ya maisha; tayari kuwarejeshea tena matumaini katika safari ya maisha yao!

Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya babu, bibi na wazee
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya babu, bibi na wazee

Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo misingi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana uzoefu na mang’amuzi ya maisha. Katika kipindi hiki ambacho mahusiano na mafungamano ya kifamilia yanalegalega, Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ambayo kwa Mwaka 2024 inaadhimishwa tarehe 28 Julai, inakuwa ni fursa ya kuboresha mahusiano kati ya kizazi kipya na kile cha zamani kwa kujenga na kudumisha upendo kati ya vijana wa kizazi kipya pamoja na wazee kwani wazee ni urithi unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa ili kujenga na kudumisha maisha ya kidugu! “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja. Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko BWANA alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele.” Zab 133:1-3.

Wazee ni amana na utajiri wa jamii
Wazee ni amana na utajiri wa jamii

Upendo kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee ni amana na utajiri mkubwa, unaowawezesha kuwa na hekima na busara, tayari kurithishana imani inayobubujika kutoka katika sala na ushuhuda wa maisha, unaofutilia mbali tabia ya uchoyo, ubinafsi na baadhi ya watu kutaka kujimwambafai, hali inayoonesha ule umaskini wa mtu kutoka katika undani wake. Ulimwengu umeumbwa na Mwenyezi Mungu na unawakusanya watu wa rika mbalimbali; mafungamano muhimu ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu. Hii inaonesha kwamba, ulimwenguni, watu wanategemeana ili kukamilishana. Vijana wa kizazi kipya wajifunze kuwaheshimu, kuliwanda na kuwatunza wazee wao badala ya kuwatelekeza katika nyumba za wazee, ambao kimsingi wanapaswa kuishi ndani ya familia, ili waweze kuhitimisha siku za kuishi hyapa ulimwenguni kwa furaha na amani moyoni na hivyo kuwafanya wawe na hekima zaidi.

Upendo kati ya vijana na wazee ni amana na utajiri mkubwa kwa jamii
Upendo kati ya vijana na wazee ni amana na utajiri mkubwa kwa jamii

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 27 Aprili 2024 alipokutana na babu, bibi, wazee pamoja na wajukuu wao mjini Vatican. Wazee ni kumbukumbu hai katika ulimwengu usiokuwa na kumbukumbu. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kujenga utamaduni wa kuwasikiliza kwa makini wazee, kama walivyofanya Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu pale Mtoto Yesu alipopelekwa Hekaluni na kukutana na Mzee Simeoni na Nabii Ana, Binti ya Fanueli waliobahatika kufunuliwa kuhusu Fumbo la Umwilisho. Lk 2: 22-28. Wazee wanao uwezo wa kuangalia mbali kwa sababu “wamekula chumvi nyingi.” Baba Mtakatifu anawahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga mahusiano mema na mafungamano ya urafiki wa kijamii na wazee. Vijana wajifunze kutoka kwa wazee upendo wa dhati, hekima na utashi mwema; wajenge utamaduni wa kuwatembelea na kuwasalimia wazee wao, ili kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Kristo Yesu alipokuwa Msalabani aliwakabidhi wanafunzi wake kwa Bikira Maria na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake. Rej. Yn 19: 26-27.

Vijana wajifunze kuwaheshimu na kuwathamini wazee
Vijana wajifunze kuwaheshimu na kuwathamini wazee

Hii ni changamoto ya watu wote kupendana na kuheshimiana kama familia kubwa ya binanamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutekeleza kwa dhati wajibu na haki msingi za wazee katika ulimwengu mamboleo. Wazee wasaidiwe kupata huduma bora za kijamii sanjari na matibabu makini; Haki msingi, heshima na utu wao vidumishwe. Kamwe wazee wasiachwe waelemewe na upweke hasi, washirikishwe kikamilifu maisha ya kifamilia.

Wazee Duniani
24 July 2024, 14:52