Papa:Padre Allamano atakuwa mtakatifu Oktoba wakati Carlo Acutis tarehe ni baadaye!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baraza la Makardinali lilikutana na Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumatatu asubuhi tarehe Mosi Julai 2024 katika Jumba la Kitume la Vatican kwa ajili ya Baraza la Kawaida la Umma. Katika fursa hiyo, Papa aliwaongoza Makardinali wanaoishi Roma na wale ambao walikuwapo katika fursa mbalimbali mjini Vatican kama ilivyokuwa imeombwa kwa kusali Sala ya Masifu ya katikati ya Asubuhi ya Liturujia ya Vipindi vya Kawaida vya mwaka kabla hawajaendelea kupitia upya mchakato wa kutangazwa kuwa watakatifu kwa baadhi ya Wenyeheri. Kardinali Marcelo Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu aliwasilisha ripoti fupi mbele ya Papa inayojulikana kwa Kilatini Peroratio, kuhusu maisha na miujiza ya watu 15 waliokuwa wakichunguzwa, na kisha Baraza hilo likapiga kura na kuidhinisha kutangazwa kwao kuwa watakatifu.
Kundi kubwa zaidi la Watakatifu wapya ni lile la waliouawa kishahidi huko Damasco, nchini Siria, mnamo mwaka 1860 na wanaojulikana kama: “Mashahidi wa Damasco.” Hao wanajumuisha Padre Manuel Ruiz López, (OFM), na wenzake 7, na Ndugu Abdel Moati, Francis, na Raphael Massabki, walei watatu wa Wamaroniti. Wote hawa 11 waliuawa kwa sababu ya chuki ya imani yao wakati wa Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivytokea huko Siria, ambavyo vilishuhudia maelfu ya Wakristo wakiuawa huko Ottoman nchini Siria na wanamgambo wa Kiislamu. Kulingana na ripoti hiyo ya Peroratio, Ndugu wa Massabki na Wafransiskani 8 waliuawa usiku wa tarehe 9 Julai 1860, walipokuwa wakisali ndani ya Kanisa la Wafransiskani huko Damasco.
Waitaliani wawili ambao ni Padre Giuseppe Allamano na Sr. Elena Guerra—pia waliidhinishwa kutangazwa kuwa watakatifu. Padre Allamano alianzisha Shirika la Wamisionari wa Consolata katika miaka ya mapema ya karne ya 20. Pia alipendezwa na matatizo ya wafanyakazi na akawa kiongozi wa Kikatoliki. Akiwa amevutiwa tangu alipokuwa mvulana na utume wa kimisionari, kwa ufasaha wa hali ya juu aliona utume wa ad gentes kama utimilifu wa upeo wa wito wa kipadre na kwa sababu hiyo alianzisha Taasisi ya Wamisionari ya Consolata mwaka 1901. Baada ya kuona hitaji la dharura la wanawake walio na wakfu kwa muda wote kwa ajili ya kazi ya uinjilishaji, miaka tisa baadaye, alianzisha, Taasisi ya Kimisionari ya Consolata ambayo, pamoja na tawi la wanaume, ikawa ndiyo shabaha ya uangalizi wa Mwenyeheri Allamano katika kipindi cha mwisho cha maisha yake. Alifariki tarehe 16 Februari 1926. Alitangazwa mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II mnamo tarehe 7 Oktoba 1990.
Wakati Sr. Elena Guerra alijitolea maisha yake kwa elimu ya wasichana na akaanzisha Shirika la Waoblate wa Roho Mtakatifu mwishoni mwa karne ya 19. Akiwa amepokea Kipaimara siku chache kabla ya kutimiza miaka minane mwaka wa 1843, alihisi kujitolea kwa ajabu kwa Roho Mtakatifu kukitokea ndani yake, kwa hiari na bila mtu yeyote kumfundisha. Ilikuwa ni mwanzo wa safari ya kukomaa kiroho na ukamilifu wa Kikristo, iliyojikita katika mada za kujinyima moyo na zaidi ya yote juu ya Roho Mtakatifu, Karamu kuu na Pentekoste. Akiwa amekubaliwa na Watawa wa upendo, alitembelea maskini na wagonjwa nyumbani na, kwa idhini ya familia yake, alifanya hivyo pia wakati kipindupindu kilipopambazuka huko Lucca. Alijitolea katika utengenezaji na uchapishaji wa maandishi juu ya hali ya wanawake na, pamoja na kikundi cha wazalendo, aliunda shule ya jiji. Kwa hivyo Taasisi ya Mtakatifu Zita ilizaliwa, kwa ajili ya elimu ya wasichana.
Baadaye watawa walianza maisha ya kawaida na walichukua jina la Waoblate wa Roho Mtakatifu. Papa Leo XIII, mwandishi pamoja na mambo mengine mnamo mwaka 1897 wa waraka wa Divinum illud Munus kuhusu uwepo na fadhila za Roho Mtakatifu, binafsi aliwahimiza Mwenyeheri kueneza ibada kwa Roho Mtakatifu. Baada ya miaka mitatu ya kuwa na afya mbaya, Elena Guerra alifariki tarehe 11 Aprili 1914. Papa Mtakatifu Yohane XXIII alimwinua hadhi kwa heshima katika madhabahu kutangazwa mwenyeheri, tarehe 26 Aprili 1959. Baraza hilo la Makardinali pia liliidhinisha kutangazwa kuwa mtakatifu kwa Mtawa mzaliwa wa Canada, Sr. Marie-Léonie Paradis (aliyezaliwa Virginie-Alodie Paradis), ambaye alianzisha Shirika la Masista Wadogo wa Familia Takatifu mwanzoni mwa karne ya 20. Majina ya Watakatifu hawa 14 wapya yataandikwa katika Orodha ya Watakatifu siku ya Dominika tarehe 20 Oktoba 2024.
Papa Francisko na Baraza la Makardinali kisha walipiga kura kuidhinisha kutangazwa Mtakatifu wa kwanza kutoka katika kizazi kipya, waliozaliwa kati ya 1981 na 1996 wanaojulikana kama wa milenia. Mwenyeheri Carlo Acutis atafanywa kuwa Mtakatifu katika tarehe ambayo bado haijaamuliwa, kulingana na Taarifa za Vyombo vaya habari . Kulingana na wasifu wake, ilisomwa kuwa Mwenyeheri Carlo Acutis, ambaye umaarufu wake wa utakatifu na ishara umeenea, katika muda mfupi sana tangu kifo chake, si tu katika Italia na Ulaya, lakini katika mabara yote. Mzaliwa wa London, kwa wazazi wa kiitalia, mnamo tarehe 3 Mei 1991, Carlo aliishi Milano. Aliomba kupokea Komunyo yake ya Kwanza mapema kuliko wakati wa kawaida, mbegu ya utume wa Ekaristi, ambayo ilikuwa na sifa ya maisha yake yote mafupi. Alipokuwa na umri wa miaka 14 alianza shule ya Sekondari katika Taasisi ya Leone XIII huko Milano, iliyoongozwa na Mapadre Wajesuit, ambapo alipata fursa ya kukuza na kuelezea vyema utu wake kama mvulana aliyejitolea na mwenye bidii, mzuri sana kwa kila mtu. Alifundisha katekisimu kwa watoto wa parokia yake ya Maria Segreta. Akiwa na shauku ya zana za kisasa zaidi za mawasiliano, alitunza tovuti ya parokia na kisha shule yake, na hatimaye Chuo cha Kipapa Cultorum Martyrum yaani cha Elimu ya Mashahidi.
Alianzisha maonesho ya kimataifa, yenye maonesho ya picha na maelezo ya kihistoria, juu ya miujiza 136 ya Ekaristi. Akiwakaribisha na kuwajali maskini zaidi, aliwasaidia wasio na makazi, wenye uhitaji na raia wasio wa Umoja wa Ulaya pesa zilizookolewa kutoka kwa “pesa zake za mfukoni” za kila Juma. Aina mbaya ya Saratani ya damu ilimaliza maisha yake ya kidunia. Siku chache kabla ya kifo chake alitoa maisha yake kwa Bwana kwa ajili ya Papa, kwa ajili ya Kanisa na kwenda Mbinguni. Kifo cha ubongo kilitangazwa mnamo Oktoba 11, 2006 na moyo wake ukaacha kudunda asubuhi iliyofuata. Kardinali Semeraro amebainisha kuwa Baba Mtakatifu alimtangaza Carlo Acutis kuwa Mwenyeheri tarehe 10 Oktoba 2020. Kwa njia hiyo “Wakiwa wamezungukwa na sifa ya kudumu ya utakatifu, Wenyeheri hawa kumi na watano walitambuliwa pia na Watu wa Mungu kuwa ni waombezi wa neema na upendeleo.” Na zaidi hivi karibuni Baba aliidhinisha maoni ya Kikao cha Kawaida cha Makardinali na Maaskofu Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu na wafiadini Wenyeheri wa Damasco. Pia aliidhinisha Baraza hili kutangaza amri kuhusu miujiza inayohusishwa na maombezi ya Wenyeheri wengine wanne.