Papa:Trieste ni bandari wazi,msimamo,ukarimu na utambuzi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Misa Takatifu na salamu kutoka kwa Askofu wa Jimbo la Trieste katika Uwanja wa Muungano wa Italia, Dominika tarehe 7 Julai 2024, akiwa huko kwa ajili ya kufunga Juma la toleo la 50 la Mafundisho Jamii ya Kikatoliki nchini Italia na kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, alianza kusema: “Kabla ya baraka ya mwisho ninapenda kuwasalimu ninyi nyote mliokusanyika katika Uwanja huu mzuri. Ninamshukuru Askofu kwa maneno yake na hasa kwa ajili ya maandalizi ya ziara yangu, na wale ambao kwa namna nyingi wameshirikiana hasa kwa ajili ya liturujia na kwa huduma mbalimbali: na kama ilivyo kwa watu wengi walioshiriki kwa sala."Papa Francisko kwa hiyo kwa wote hao amewahakikishia ukaribu wake: “wagonjwa na wafungwa, wahamiaji na kwa wote ambao wanapata ugumu wa maisha."
Papa akiendelea amesema: “Trieste ni moja ya mji ambao una miito ya kufanya waingie watu tofauti: awali ya yote kwa sababu ni bandari na bandari muhimu na kisha kwa sababu inajikuta njia panda kati ya Italia, Ulaya ya Kati na Nchi za Balkan. Katika hali hizo, changamoto kwa jumuiya ya kikanisa na kwa zile za kiraia ni kujua namna ya kuunganisha uwazi na msimamo, makaribisho na utambuzi.”
Papa Francisko kisha amebainisha kuwa imemjia akilini kusema: “mna kadi za kanuni” ili kukubiliana na changamoto hiyo! Kama wakristo tuna Injili ambayo inatoa maana na matumaini katika maisha yetu; na kama raia mnayo Katiba na “dira” inayaoaminika ili kutembea katika demokrasia." Kwa njia hiyo Papa amewatia moyo wa "kuendelea mbele bila kuogopa, wakiwa wazi, na msimamo thabiti katika thamani za kibinadamu na kikristo, huku wakikaribisha lakini bila kuathiri utu wa binadamu."
Na kutoka katika mji huo wa kupyaishwa kwa jitahada zao, ni ombo la Papa ili kusali na kutenda kwa ajili ya amani; hasa kwa ajili ya nchi ya Ukraine inayoteseka, kwa ajili ya Palestina na Israeli, kwa ajili ya Sudan, Myanmar na kila watu ambao wanateseka kwa vita.” Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu amesema “ Tumuombe kwa maombezi ya Bikira Maria anayefanyiwa ibada juu ya Mlima Grisa kama Mama na Malkia.” Na baadaye walisali sala ya Malaika wa Bwana kabla ya kurudi jijini Vatican ambapo ulikuwa ndiyo mwisho wa hitimisho la Toleo la 50 la Mafundisho ya Kijamii Katoliki nchini Italia lililofunguliwa tarehe 3 Julai na mgeni Rasmi Rais wa Nchi Bwana Sergio Mattarella.