Tafuta

Baba Mtakatifu anasema siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbalimbali za maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbalimbali za maisha ya binadamu.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Siasa Safi Ni Kwa Ajili ya Ustawi, Maendeleo na Mafao ya Wengi

Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, siasa inayohitajika katika kujenga udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii, inapania pamoja na mambo mengine kukuza na kudumisha amani ulimwenguni sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa kidigitali, yamesaidia maboresho makubwa katika matumizi ya “akili mnemba” katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu, iwe kwa mtu binafsi au jamii katika ujumla wake. Mapinduzi haya makubwa ya teknolijia yanawawezesha watu kujifahamu sanjari na kuufahamu ulimwengu unaowazunguka, kiasi hata cha kuathiri maamuzi, uwezo wa kufiki na kutenda katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Leo hii utashi wa mwanadamu unaathiriwa kwa namna ya pekee na matumizi ya teknolojia ya akili mnemba kutokana na mchango wake mkubwa! Siasa inayojihusisha na matokeo ya haraka ikisaidiwa na sekta ya manunuzi husukumwa na uzalishaji wa muda mfupi na kwa masilahi ya watu wachache ndani ya jamii. Kumbe, ujuzi halisi wa uongozi unajionesha pale ambapo mkazo zaidi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na ujenzi wa taifa na ujenzi wa familia ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuweka uhusiano mwema baina ya siasa na uchumi kwa ajili ya mustakabali wa binadamu. Na hii ndiyo hali halisi ya teknolojia ya akili mnemba. Ni wajibu wa binadamu kuweza kuitumia vyema na kwamba, lazima ziwepo sera bora zaidi za matumizi bora ya teknolojia ya akili mnemba. Rej. Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Wakuu wa G7 14 Juni 2024.

Siasa safi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Siasa safi ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Baba Mtakatifu anasema siasa safi inafumbatwa katika unyenyekevu, kielelezo makini cha huduma katika ngazi mbalimbali za maisha ya binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha dhamana, utu, heshima na tunu msingi za maisha zinazoiwezesha jamii kutekeleza mafao ya wengi. Kumbe, utekelezaji makini wa siasa safi ni changamoto endelevu kwa viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza, kwani wanapaswa kuwalinda raia wao; kwa kushirikiana kikamilifu ili kuboresha maisha ya wananchi wao katika misingi ya haki, uhuru, utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, siasa safi inakuwa ni chombo cha upendo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo na fadhila za kiutu ziwe ni kwa ajili ya siasa safi inayohudumia haki msingi na amani, kila mtu akijitahidi kujikita katika mafao ya wengi, kama sehemu ya ujenzi wa mji wa Mungu hapa duniani, ili kuendeleza historia ya maisha ya familia ya binadamu. Haki na usawa; tabia ya kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu; ukweli, uwazi na uaminifu ni tunu msingi zinazoboresha siasa safi na kwamba, mwanasiasa bora ni yule anayetambua dhamana na wajibu wake kwa jamii; anayeaminika na kuthaminiwa na jamii; ni kiongozi anayejitaabisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mwaminifu katika ahadi zake kwa wananchi waliomchagua, daima akijitahidi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano, tayari kuchochea mageuzi katika maisha ya watu; kwa kuwasikiliza na kutenda kwa ujasiri!

Wakatoliki wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa
Wakatoliki wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa

Baba Mtakatifu anasema, hivi ni vigezo muhimu sana wakati wa kufanya chaguzi mbalimbali, ili kuhakikisha kwamba, haki, dhamana na wajibu vinatekelezwa kikamilifu. Siasa safi ni chombo cha huduma ya amani inayosimikwa katika kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa vizazi kuheshimiana na kuthaminiana. Vilema vya wanasiasa vinajionesha katika maisha ya hadhara, kwenye taasisi wanazohudumia pamoja na utunzaji bora wa mazingira; mambo yanayoweza kuwafanya watu kumwamini mwanasiasa, katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati yake kama kielelezo cha demokrasia. Vinginevyo, wanasiasa wanaoelemewa na vilema vyao ni hatari sana katika kujenga na kukuza demokrasia jamii. Hawa ni watu ambao “wamepekenywa” kwa rushwa na ufisadi; watu wasioheshimu wala kujali utawala wa sheria; ni watu wenye uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka; ni wachochezi wa ubaguzi na hofu miongoni mwa jamii wala utunzaji bora wa mazingira kwao si kipaumbele, lakini matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza umuhimu wa kudumisha siasa safi inayowashirikisha vijana na kujengeana imani, kiasi kwamba, hata vijana wa kizazi kipya wanajisikia kuwa ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii yao na kwamba, wanaweza kushirikisha karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Hawa ni vijana ambao dhamana ya amani inapenyeza katika akili na nyoyo zao, tayari kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Demokrasi safi ni ile inayowashirikisha watu wote wa Mungu
Demokrasi safi ni ile inayowashirikisha watu wote wa Mungu

Ni katika muktadha wa siasa safi, Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii, katika tahariri yake baada ya Baba Mtakatifu Francisko kushiriki katika maadhimisho ya Juma la Wakatoliki wa Italia Kijamii kuanzia tarehe 3-hadi 7 Julai 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Demokrasia Inahitaji Ujirani anauliza swali msingi, Je? Siasa ni nini? Kinzani katika demokrasia inayopelekea kudhani kwamba, siasa inakita mizizi yake katika uchu wa madaraka na kusahau kwamba, siasa safi haina budi kujielekeza katika kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anawachangamotisha waamini na wanasiasa katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanajikita katika siasa na demokrasia shirikishi inayosimikwa katika upendo, mshikamano, uwajibikaji pamoja na kanuni ya auni. Lengo ni kuwawezesha wanasiasa kuwa ni vyombo vya matumaini, kwa kuwashirikisha watu wengi zaidi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si katika azma ya kujijengea umaarufu kisiasa. Jambo la msingi ni ushiriki mkamilifu wa Wakristo katika masuala ya kisiasa, ili kuleta mabadiliko. Baba Mtakatifu Francisko anasema, imani ya kweli inapania kuleta mabadiliko, kurithisha tunu msingi na kuacha mambo ya kudumu baada ya kuitupa mkono dunia. Huu ni mwaliko kwa watu wateule wa Mungu kuwajibika kikamilifu katika maisha ya kisiasa na kuachana na mtindo wa Pontio Pilato aliyekwepa kuwajibika kwa kunawa mikono! Watu wasimame kidete kulinda na kutetea haki, kwa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu. Kumbe, wanasiasa wanaitwa kushikamana na kutembea pamoja na watu wao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kuzima kiu na njaa ya haki!

Dr. Paolo Ruffini

 

09 July 2024, 14:10