Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2024 imeadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2024 imeadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo.   (Siam Pukkato)

Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu Kwa Mwaka 2024

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2024 imeadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Kaulimbiu ya mwaka huu wa 2024 ni "Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katika vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu." Papa Francisko anasema, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo ni donda ndugu katika mwili wa binadamu katika ulimwengu mamboleo: Utu na Haki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 30 Julai 2024 imeadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Kaulimbiu ya mwaka huu wa 2024 ni "Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katika vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu." Hii siku iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2013 ili kusaidia juhudi za kimataifa za kuragibisha athari za biashara hii katika maisha ya binadamu, haki msingi, utu na heshima yake. Kila mwaka kuna mamilioni ya watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na mifumo ya utumwa mamboleo, hususan katika kazi za suluba, utalii wa ngono na biashara haramu ya viungo vya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni donda ndugu katika mwili wa binadamu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii, kuwashukuru wale wote wanaoendelea kusimama kidete ili kuwasaidia na kuwahudumia wahanga wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Kuna hatua kubwa ambazo zimekwisha kufikiwa na Jumuiya ya Kimataifa, lakini, bado kuna haja ya kuendelea kupambana ili hatimaye, kashfa hii dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu iweze kufutika machoni pa uso wa dunia! Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2015 alipokuwa anahutubia kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati katika kupambana na biashara haramu ya binadamu na viungo vyake sanjari na utumwa mamboleo unaodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mapambano haya lazima kwanza kabisa yalinde na kuheshimu: utu na haki msingi za binadamu.

Vita dhidi ya usafirishaji wa binadamu: kipaumbele mwaka 2024: Watoto
Vita dhidi ya usafirishaji wa binadamu: kipaumbele mwaka 2024: Watoto

Baba Mtakatifu anasema, Pili, ni kwa kusimama kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato na tatu ni kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vatican daima imekuwa mstari wa mbele kupambana na biashara haramu ya binadamu ili kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kuridhia Itifaki ya Umoja wa Mataifa katika mchakato wa kupambana na biashara haramu ya binadamu, kwani ni biashara inayowanyanyasa watu wengi zaidi. Ndiyo maana Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa aliwataka viongozi wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha utashi wa kisiasa katika mapambano haya. Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake mbalimbali limeendelea kujipambanua kuwa ni kati ya wadau wakuu wanaopambana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na kuwasaidia waathirika ili waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida. Utumwa mamboleo unaendelea kukua na kukomaa, kumbe, unahitaji watu kulitambua hilo na kuchukua hatua madhubuti, hii ikiwa ni pamoja na kubadili mtindo wa maisha. Ikumbukwe kwamba, mafanikio katika maisha yanapatikana kwa juhudi na maarifa, kwa kujinyima na kujiwekea malengo thabiti. Serikali mbalimbali zinapaswa pia kujizatiti katika kuboresha hali ya maisha ya wananchi wake kwa kuwapatia mahitaji msingi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, ndiyo maana kunako mwaka 2015 alipokuwa anazungumza na mabalozi pamoja na wawakilishi wa nchi na mashirika mbali mbali mjini Vatican aliwataka kuhakikisha kwamba, wanasaidia katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni katika muktadha huu, Kikundi cha Mtakatifu Martha kilianzishwa katika jitihada hizi za Baba Mtakatifu Francisko kuwahusisha wadau mbali mbali katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo!

Kupambana na umaskini kiwe ni kipaumbele cha Jumuiya ya Kimataifa
Kupambana na umaskini kiwe ni kipaumbele cha Jumuiya ya Kimataifa

Kaulimbiu ya mwaka huu wa 2024 ni "Hakuna mtoto anayepaswa kuachwa nyuma katika vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu." Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa na Uhalifu (UNODC) imeandaa nyenzo za utafiti kuhusu utumikishwaji wa watoto ili kuongeza uelewa wa tatizo hili la kimataifa na kutoa wito wa kuchukua hatua za kukomesha usafirishaji haramu wa binadamu. Usafirishaji haramu wa watoto unahusisha matumizi ya watoto yanayofanywa na wahalifu kwa lengo la utumikishwaji. Huu ni uhalifu mkubwa na ukiukwaji wa haki msingi za binadamu, hata kama inaonekana kwamba mtoto amekubali kwa namna fulani "kutumikishwa." Mara nyingi, hii hufanyika kwa: kutumia nguvu, udanganyifu, kulazimishwa, matumizi mabaya ya mamlaka, au mazingira magumu. Watoto wanaweza kutumikishwa katika njia mbalimbali. Miongoni mwao ni: Utumikishwaii wa kingono, ambao unaweza kujumuisha dhuluma dhidi ya watoto ili kuwatumikisha kingono kwa malengo ya biashara au utengenezaji wa nyenzo za ukatili wa kijinsia kwa watoto. Aidha, kazi za shuruti ambapo watoto hufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kwenye sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, viwanda, migodi au kama wafanyakazi wa majumbani. Njia nyingine ya utumikishwaji ni kuwalazimisha watoto kuombaomba mitaani au kufanya uhalifu kama vile wizi. Watoto katika migogoro ya silaha hutumikishwa kwa kuchukuliwa kama wapiganaji, kutumiwa kingono au kuwekwa katika utumwa wa majumbani.

Mazingira magumu ya maisha yanawafanya wasichana wengi  kurubuniwa
Mazingira magumu ya maisha yanawafanya wasichana wengi kurubuniwa

Ndoa za utotoni ni njia nyingine ya utumikishwaji unaowaathiri zaidi wasichana. Wasichana hawa wanaozeshwa kwa malipo au ili kuboresha hali ya kijamii, mara nyingi kama sehemu ya mila na desturi za kitamaduni zenye madhara na zilizopitwa na wakati. Kuasili watoto kinyume cha sheria ni utumikishwaji unaojumuisha usafirishaji wa watoto kwa ajili ya kuwaasili kwa lengo la kuwatumikisha, mara nyingi kwa kuwalaghai au kuwalazimisha wazazi au walezi wao. Wakati mwingine waathirika wa usafirishaji haramu wa watoto wanaweza kutumikishwa katika njia kadhaa. Kwa mfano, mtoto anayelazimishwa kuombaomba mitaani anaweza pia kutumikishwa kingono. Wasichana na wavulana wanaathirika na usafirishaji haramu wa binadamu, lakini inaweza kuathiri watoto kwa njia tofauti kulingana na jinsia na eneo. Wasichana wanasafirishwa zaidi kwa utumikishwaji wa kingono, wakati wavulana wanasafirishwa kwa ajira za shuruti. Usafirishaji haramu wa watoto hufanyika duniani kote, lakini kwa utofauti wa maeneo. Kaskazini mwa Afrika na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa mfano, watoto wanachangia sehemu kubwa ya waathirika wa usafirishaji haramu wa binadamu, na ajira ya kulazimishwa ndio imekithiri Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Vita inachochea biashara haramu binadamu
Vita inachochea biashara haramu binadamu

Hata hivyo, katika Amerika ya Kati na Karibea, waathirika wengi waliotambuliwa ni wasichana, hasa vijana wanaoanza kubalehe, ambao wamesafirishwa kwa utumikishwaji wa kingono. Kusini mwa Asia, karibu nusu ya waathirika ni watoto waliotumikishwa kama wafanyakazi au kulazimishwa kuolewa. Usafirishaji haramu wa watoto unastawi katika hali ya matatizo kwenye familia, umaskini, ukosefu wa usawa, ulinzi usiotosha na ukosefu wa malezi bora ya wazazi. Wahalifu mara nyingi hulenga watoto kutoka familia maskini sana au wale walioachwa na wazazi na walezi wao. Migogoro, matatizo ya kiuchumi na majanga asilia yanawafanya watoto, hasa wale wasio na walezi na waliotengana na familia zao, kuwa katika mazingira hatarishi zaidi. Wakati wasafirishaji wengi wa binadamu ni wahalifu sugu, wanaweza pia kuwa wajasiriamali wa ndani, wapenzi wa karibu, na wanafamilia. Wasafirishaji haramu wa binadamu hutumia majukwaa ya mtandaoni, mitandao ya kijamii, na wavuti za siri kuwasiliana, kutumikisha na kudumisha mamlaka mabaya dhidi ya watoto. Kwa msaada wa teknolojia ya kisasa, wanakwepa kugunduliwa na kuendelea kusambaza maudhui ya kikatili. Matumizi ya watoto ya mtandao na mitandao ya kijamii bila uangalizi, mara nyingi bila hatua sahihi za usalama, yanaweza kuwaweka watoto katika hatari zaidi ya kutumikishwa. Uhalifu huu una madhara makubwa kwa ukuaji wa kimwili, kiakili na kijamii wa watoto. Waathiriwa mara nyingi wanapata matatizo ya kiafya ya muda mrefu, matatizo ya kiwewe, wasiwasi, msongo wa mawazo, na matatizo ya kujumuika kijamii. Watoto wana uwezekano wa kukumbwa na ukatili mkubwa na wasafirishaji haramu wa binadamu mara mbili zaidi ikilinganishwa na waathiriwa watu wazima. Idadi hii ni kubwa zaidi miongoni mwa wasichana.

Utumwa Mamboleo

 

 

 

31 July 2024, 15:39