Siku ya Nne ya Babu Bibi na Wazee 2024: Mshikamano wa Upendo na Wazee!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 inanogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Sala ya mkongwe “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 anasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanagundua wakiwa wamechelewa kwamba, walishindwa kuwatendea vyema wazee na kwamba haya ni mazoea mabaya sana kwa wazee na hasa katika kipindi hiki cha likizo ya kiangazi. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Dominika tarehe 28 Julai 2024 amesema, huu ni wakati wa kusikiliza na kujibu kilio cha wazee wanaoelemewa na upweke hasi; kwa kuendelea kujenga mtandao wa mshikamano wa umoja, udugu na upendo miongoni mwa ndugu na jamaa. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutambua kwamba, ustawi na maendeleo kwa siku za usoni unategemea hasa jinsi watu wanavyoishi kwa umoja na upendo. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawaonea huruma wazee, kwa kuwatembelea mara kwa mara na kuwatia moyo, wale waliovunjika na kupondeka moyo na hivyo kujikatia tamaa ya maisha; tayari kuwarejeshea tena matumaini katika safari ya maisha yao!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu kamwe hawatelekezi watoto wake, wala haangalii kama binadamu aangaliavyo na kwamba, kimsingi Maandiko Matakatifu ni simulizi la uaminifu wa upendo wa Mungu unaofumbatwa katika huruma katika kila hatua ya maisha hata katika uzee na kwamba, uzee kadiri ya Maandiko Matakatifu ni alama ya baraka. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 kielelezo cha ukatili wa hali ya juu sana kutoka kwa mwanadamu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu pale Mlimani Kalvari, kiasi cha Kristo Yesu kulia kwa sauti “Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Mt 27:46. Katika Maandiko Matakatifu, kumesheheni viashiria vya ukaribu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu katika uzee, mateso na mahangaiko ya maisha bila kusahau upweke hasi unaowaandama hasa maskini, wazee na wazazi pweke. Upweke huu unaweza kusababishwa na vijana kuhama familia zao ili kutafuta maisha bora zaidi, vita, mila na desturi zilizopitwa na wakati. Hii inachangiwa pia na vijana kukwepa kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa wazazi na walezi wao, mwaliko kwa vijana kupenda na kuthamini zawadi ya maisha. Kauli mbiu: “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati mwingine, hii ni sera inayokita mizizi yake katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kibinafsi ambayo kamwe haitambui “dignita infinita” yaani “heshima isiyokuwa na ukomo.” Badala yake sera na mikakati kama hii inaunga mkono mchakato wa kudhibiti gharama ya maisha na wale wanaogharamia ni wazee, wanaoshutumiwa kwa kuwa ni mzigo usiobebeka na hivyo kutengwa. Kuna baadhi ya watu katika Jamii wanaamua kuishi katika hali ya upweke na inawawia vigumu kuishi na wengine. Wazee ni tabaka linalotaka kujitegemea kwa kudhani kwamba, wamekuwa mzigo kwa jamii na hivyo kutaka kujitegemea na hivyo kuwapatia vijana nafasi ya kufurahia maisha. Lakini kama inavyojionesha kwenye Maandiko Matakatifu hasa katika kitabu cha Ruthu, ambapo Naomi anaamua kubaki na Ruthu kwani kama mwanamke mjane, aliona hana tena thamani mbele ya jamii, lakini Ruthu anamwonesha upendo na anahidi kutokumwacha kamwe katika uzee wake. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa Kristo Yesu, Bwana na Masiha, Imanueli, Mungu pamoja na waja wake katika hali zote. Hiki ni kielelezo cha uhuru na ujasiri unaoweza kubadili hatima ya wazee wengi, kwa kujikita katika uwepo wa karibu hata kama itabidi kutoa sadaka kubwa. Ruthu ni mfano bora wa kuigwa katika ulinzi na tunza bora kwa wazee. Ruth aliamua kukaa karibu na Naomi na kitendo hiki kikawa ni chemchemi ya baraka na neema ya kupata ndoa yenye furaha, uzao pamoja na ardhi.
Kumbe, waamini kwa kukaa karibu na wazee, kwa kutambua dhamana na wajibu wao katika familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake, wataweza kupata neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 iwe ni fursa ya kuwafariji: babu, bibi na wazee walioko kwenye familia; iwe ni nafasi ya kuwatembelea na kuwasalimia wale wote waliovunjika na kupondeka moyo, kiasi cha kujikatia tamaa. Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi unaopelekea watu kumezwa na utamaduni wa kutupa na hivyo kuwatumbukiza watu wengi katika upweke hasi. Huu ni wito wa kuonesha moyo wa ujasiri na upendo kwa kushikamana na kutembea na babu, bibi na wazee, bila kuwageuzia kisogo hata kidogo!