Sikukuu ya Mtakatifu Maria Magdalena Mtume wa Mitume: Shuhuda wa Ufufuko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko alipenda kuonesha ukuu na mchango wa Mtakatifu Maria Magdalena unaofumbatwa katika upendo aliouonesha kwa Kristo Yesu pale alipompaka mafuta ya gharama kubwa, alipokuwa nyumbani kwa Simoni Mfarisayo. Huyu ni kati ya wanawake watatu wanaotajwa kuwa ni kati ya wafuasi wa karibu wa Kristo Yesu, aliyefuata Njia ya Msalaba hata akadiriki kusimama chini ya Msalaba. Siku ya kwanza ya Juma, asubuhi na mapema, Kristo Yesu akamtokea Maria Magdalena na kumshuhudia kuwa ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu, kiasi cha kudondosha chozi la furaha ya Pasaka. Mtakatifu Maria Madgalena alipata heshima ya kuwa ni mfuasi wa kwanza kushuhudia kufufuka kwa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, "testis divinae misericordiae", kama Papa Gregory Mkuu anavyofafanua. Yesu Mfufuka akamwonjesha huruma na upendo wake; chemchemi ya maisha mapya, dhidi ya Eva aliyesababisha kifo. Yesu akamwambia Maria Magdalena “Non me tangere”, yaani “Yesu akamwambia. Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.” Yn 20:17. Huu ni wito pia kwa Kanisa kuambata imani na kuendelea kuamini ubinadamu unaojionesha katika Fumbo la Mungu. Mama Kanisa kuanzia tarehe 22 Julai 2016 anaadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Maria Magdalena, yaani wa Magdala (Kwa lugha ya Kigiriki Μαρία ἡ Μαγδαληνή) ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi maarufu zaidi wa Yesu wa Nazareti, hasa kutokana na sifa ya kuwa wa kwanza kukutana mubashara na Kristo Yesu Mfufuka. Rej. Mk 16:9 na Yn 20:16. Baba Mtakatifu Francisko anasema, lengo la kuipandisha kumbukumbu ya Mtakatifu Maria Magdalena kuwa ni Sikukuu ya lazima kwenye Kalenda ya Kanisa Katoliki ni kuendelea kutafakari kuhusu: wito, utu, heshima, hadhi na haki msingi za wanawake.
Kanisa linapenda kutambua ushiriki wao katika uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake kwenye ushuhuda sanjari na ukuu wa Fumbo la huruma ya Mungu kwa mwanadamu. Wanawake wamekuwa ni wadau wakuu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni dhamana endelevu na fungamani inayojionesha kwa namna ya pekee, katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaowaambata watu wote pasi na ubaguzi, ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, inayowasindikiza waamini katika safari yao hapa duniani sanjari na kuwaonjesha maajabu ya Wokovu unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Maria Magdalena ni mfano bora na Mwinjilishaji, aliyewashirikisha wengine ile furaha ya Ufufuko wa Kristo, kiini cha Fumbo la Pasaka. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kudumisha maisha na utume wa Kanisa katika ngazi mbalimbali za maisha. Hii ni siku ambayo Mama Kanisa anapenda kuwashukuru wanawake wote kwa moyo na upendo wao wa kimama, katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake wanaalikwa kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Wanawake waendelee kuwa ni mfano bora na kikolezo cha utakatifu wa maisha katika sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, utakatifu ni jambo linalowezekana, kila mtu ajitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na katika majukumu ya kifamilia na kijamii.
Maria Magdalena ni Mtakatifu aliyesikia na kupewa dhamana ya kuwapasha ndugu zake Kristo Yesu kwamba: kweli Yesu amefufuka kwa wafu! Maria Magdalena ni shuhuda na mtangazaji wa Ufufuko wa Kristo Yesu kama walivyokuwa Mitume wengine ndiyo maana Mtakatifu Thoma wa Akwino anamwita kuwa ni “Mtume wa Mitume” kwani alitangaza kile ambacho Mitume watapaswa kukitangaza na kukishuhudia hadi miisho ya dunia. Maria Magdalena ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaoganga, na kuponya; upendo unaomwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ndiyo maana Kumbukumbu ya Mtakatifu Maria Magdalena imepandishwa hadhi sasa na kuwa ni Sikukuu kwa Kanisa zima. Tarehe 22 Julai ya kila mwaka sasa Kanisa linasali na kuwaombea wanawake wote walioonesha ujasiri wa pekee katika kumwamini, kumpenda na kumtangaza Kristo Yesu kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu kwa watu wa nyakati mbalimbali duniani. Kweli ni vyema na haki kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na utukufu wake ulioshuhudiwa na Kristo Yesu na kutangazwa na Mtakatifu Maria Magdalena. Akabahatika kuwa Mtume kwa Mitume wa Yesu waliokimbia mbio kwenda kushuhudia kaburi wazi, Kristo Yesu akiwa amefufuka kwa wafu! Maria Magdalena alibahatika kumwona Kristo Yesu, “mubashara” yule aliyekuwa amempenda wakati wa uhai wake, akashuhudia akiteswa, kufa na kuzikwa. Akabahatika kumwabudu akiwa amefufuka kwa wafu kama anavyosimulia Mwinjili Yohane 20:1-18. Mtakatifu Maria Magdalena akawa ni shuhuda wa Injili hai, yaani Kristo Yesu, Bustani iliyokuwa chanzo cha kifo wakati wa Eva na Adamu, sasa inakuwa ni chemchemi ya maisha mapya na furaha ya Injili.