TANZIA: Rais Mstaafu wa Vietnam Nguyễn Phú Trọng: Papa Francisko Atuma Salam!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amepokea taarifa za kifo cha Rais Mstaafu wa Vietnam Nguyễn Phú Trọng, ambaye pia alikuwa ni Katibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam kilichotokea tarehe 19 Julai 2024 akiwa na umri wa miaka 80. Alikuwa ni Katibu mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2024 na Rais wa Vietnam kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2024. Itakumbukwa kwamba, Rais Mstaafu Nguyễn Phú Trọng alizaliwa tarehe 14 Aprili 1944 huko Hanoi.
Baba Mtakatifu katika salam za rambirambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Jenerali To Lam, Rais wa Vietnam, Baba Mtakatifu anapenda kuungana na wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito kwa sala, faraja na amani. Baba Mtakatifu anamkumbuka Hayati Nguyễn Phú Trọng kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Vietnam sanjari na kujenga na kukuza mahusiano ya kidiplomasia na Vatican. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha uwepo wake wa karibu kwa Rais To Lam na wananchi wote wa Vietnam katika kipindi hiki cha masikitiko pamoja na maombolezo.