Tunu Msingi za Maisha ya Ndoa na Familia Ni Mbegu za Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Familia ni kitalu cha kupandikiza mbegu za ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Wakati huo huo, Ndoa ya Kikristo ina uzuri wake kwani hii ni Sakramenti inayoadhimishwa ndani ya Kanisa pamoja na kusaidia mchakato wa ujenzi wa Jumuiya mpya, Kanisa dogo kama familia ya Mungu inayowajibika pamoja na jamii. Hili ni fumbo kuu linalonesha uhusiano wa upendo wa dhati kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake; hiki ni kielelezo makini cha upendo na imani ya Kanisa. Ndoa ni sehemu ya mpango wa kazi ya uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu na kwa njia ya neema na baraka za Mwenyezi Mungu, wakristo wameweza kuishi Sakramenti hii katika utimilifu wake.Baba Mtakatifu Francisko anasema ndoa ni tendo la imani mintarafu mpango wa Mungu kwa binadamu na ni kielelezo cha sadaka ya upendo. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa katika nyaraka zake anaoanisha upendo wa Kristo Yesu kwa Kanisa lake kama ulivyo upendo kwa watu wa ndoa wanavyopaswa kupendana kwa dhati, kama Kristo Yesu alivyolipenda Kanisa kiasi cha kujisadaka kwa ajili yake. Pale ambapo mwanaume na mwanamke wanaamua kuoana katika Kristo Bwana, wanashiriki katika umisionari wa Kanisa, kwa kuishi si tu kwa ajili ya familia zao, bali kwa ajili ya wote.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kutokana na ukweli huu, maisha na utume wa Kanisa yanarutubishwa na kila ndoa inayofungwa Kanisani, kwani zinaonesha ule uzuri wa ndoa; Kanisa linadhalilishwa pale ndoa inapobomolewa na kusambaratika. Wanandoa wanaoishi kikamilifu na kwa ujasiri neema ya Sakramenti ya Ndoa, wanalisaidia Kanisa kutoa zawadi ya imani, matumaini na mapendo kwa watu wote sanjari na kuwasaidia watu wengine kuonja zawadi hizi katika maisha ya ndoa na familia zao. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna waamini ambao kweli wanajitahidi kuliishi Fumbo hili kwa ukamilifu wake, kwa kujiaminisha kwa Mungu na tunza kutoka kwa Mama Kanisa. “Équipes Notre-Dame, E.N.D” ni vuguvugu la waamini walei lililoibuliwa na wanandoa kutika kuitikia hitaji la wanandoa kwa kuishi Sakramenti ya Ndoa kikamilifu, kwa kusimama kidete kuangalia matatizo, changamoto na fursa wanazokabiliana nazo wanandoa katika maisha na utume wao. Wazo hili liliibuliwa kunako mwaka 1938 kwa baadhi ya wanandoa wakishirikiana na Padre Henri Caffarel kujenga mazoea ya kukutana walau kila mwezi ili kutafakari kwa kina maana ya Sakramenti ya Ndoa, umuhimu wake kwa waamini na jamii katika ujumla wake. Vuguvugu hili likawa msaada mkubwa kwa wanandoa waliokuwa wanakabiliana na matatizo na changamoto mbalimbali katika maisha ya ndoa na familia. Tarehe 8 Desemba 1947 Équipes Notre-Dame, E.N.D ikazaliwa rasmi. “Équipes Notre-Dame, E.N.D” kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 20 Julai 2024 walikuwa wamekusanyika Jimbo kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia, huku wakiongozwa na kauli mbiu “Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu,...Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate.” Lk 24: 33-35. Huu ni mkutano wa kumi na tatu wa“Équipes Notre-Dame, E.N.D.”
Mkutano huu wa Kimataifa umewashirikisha wajumbe 7, 600 kutoka katika nchi 86 na wanatarajia kukutana tena kunako mwaka 2030. Mada zilizojadiliwa ni pamoja na Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; Umuhimu wa kusikiliza Neno la Mungu ili kuthubutu kuanza hija; amana na utajiri wa Neno la Mungu linaloangazia safari ya imani. Wajumbe wamepembua kwa kina na mapana kuhusu zawadi ya maisha ya ndoa na familia mintarafu mwanga wa Injili ya Kristo Yesu na kwamba, walimtambua katika kuumega mkate. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ili kujenga na kuimarisha ushirika, twende kwa moyo unaowaka! Mama Gabriela Gambino, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika hotuba yake amekazia umuhimu wa wanandoa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani inayopata chimbuko lake katika maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Neno la Mungu. Watambue kwamba, wao kimsingi ni wamisionari wanaotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwashirikisha wengine, furaha ya Injili, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Familia ni chombo madhubuti cha uinjilishaji wa kina, unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.
Kwa upande wake, Sr. Nathalie Becquart, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi, anasema, familia ni shule ya kwanza katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaosimikwa katika safari ya ujenzi wa ushirika wa Kanisa. Wanandoa ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaofumbatwa katika sadaka, upendo na majitoleo ya wanandoa, ili kwa pamoja waweze kushiriki katika ujenzi wa Kanisa linalosimikwa katika umoja, ushiriki na utume. Ikumbukwe kwamba, familia inasimikwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, changamoto kwa wanafamilia kuhakikisha kwamba, wanaishi kwa upendo na umoja; kwa kutambua dhamana na wito wao unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, kumbe wanaitwa kuwahudumia ndugu zao katika Kristo pamoja na Kanisa katika ujumla wake. Matunda ya Mkutano wa Kimataifa wa Équipes Notre-Dame, E.N.D uwasaidie wanandoa kuendelea kupandikiza mbegu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kujikita katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa ndani ya familia, lakini zaidi katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake.