Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2024,  ni mwaliko kwa waamini kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanaochakarika usiku na mchana katika Utume wa Bahari, yaani mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2024, ni mwaliko kwa waamini kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanaochakarika usiku na mchana katika Utume wa Bahari, yaani mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. 

Ujumbe wa Dominika ya Utume wa Bahari Kwa Mwaka 2024

Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 14 Julai 2024. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa uwepo na utendaji wa Mapadre washauri wa maisha ya kiroho, watu wa kujitolea pamoja na waamini wa Makanisa mahalia wanaojisadaka ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za mabaharia na wavuvi zinaheshimiwa na kulindwa, ili kwa pamoja kuweza kujikita katika ujenzi wa umoja, ushirikiano na udugu wa kibinadamu kwa msaada wa B. Maria Nyota ya Bahari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utume wa Bahari, “Apostolatus Maris” unaojulikana na wengi kama “Stella Maris” ulianzishwa tarehe 4 Oktoba 1920 na waamini walei wanaoshiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu unaopata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo. Ni jukumu na wito wa waamini walei kuutafuta Ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia, na kuyaelekeza kadiri ya mpango wa Mungu. Wanaitwa kuyatimiza majukumu yao wenyewe wakiongozwa na roho ya Kiinjili, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo thabiti! Ili kuonesha na kushuhudia ukaribu wa Kanisa kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, Papa Pio XI tarehe 17 Aprili 1922 aliridhia kuanzishwa kwa Utume wa Bahari “Apostolatus Maris.” Leo hii kuna jeshi kubwa la watu wanaojisadaka zaidi kuwadumia mabaharia na wavuvi katika bandari 300 kwa kutembelea meli zisizopungua 70,000 kwa mwaka. Mama Kanisa anawashukuru kwa dhati Mitume hawa wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Wadau wa Utume wa Bahari wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji wa kina kwa kuwafunulia watu wa Mungu, ile sura pendelevu ya Mama Kanisa: kwa kuonesha ukaribu wake kwa watu watakatifu wa Mungu, na hivyo kuwahamasisha kujisikia kuwa ni sehemu hai ya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Takribani miaka 100 iliyopita, imekuwa ni kipindi muafaka cha ujenzi wa misingi ya majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, kutokana na mwingiliano wa watu kutoka katika dini, tamaduni na Mataifa mbalimbali duniani. Mama Kanisa tarehe 14 Julai 2024 aneadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari, fursa kwa Familia ya Mungu sehemu mbalimbali za dunia, kumshukuru Mungu kwa huduma na mchango mkubwa, unaotolewa na mabaharia pamoja na wavuvi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari Kwa mwaka 2024
Maadhimisho ya Dominika ya Utume wa Bahari Kwa mwaka 2024

Ni siku maalum ya kutambua na kuthamini sadaka ya watu hawa ambao wakati mwingine: haki, utu na heshima yao vinahatarishwa kutokana na changamoto mbalimbali, wanazokumbana nazo wakati wa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa jamii. Hii ni siku maalum ambayo Kanisa linatambua mchango mkubwa unaotolewa na Mabaharia pamoja na wavuvi katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika nyanja mbalimbali za maisha. Maadhimisho haya pia yana mwelekeo wa kiekumene, kwani yanawashirikisha Wakristo kutoka katika Makanisa na madhehebu mbalimbali ya Kikristo, ili kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 14 Julai 2024 amewakumbusha waamini kwamba, Mama Kanisa alikuwa anaadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2024, mwaliko kwa waamini kuwakumbuka na kuwaombea wale wote wanaochakarika usiku na mchana katika Utume wa Bahari, yaani mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao bila kuwasahau wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia kiroho na kimwili. Hili ni jeshi kubwa la mamilioni ya watu wasioonekana, lakini ni muhimu sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hawa ni watu wanaosafiri na kutumia muda mrefu wakiwa baharini, ni watu ambao: utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa. Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi baharini.

Siku ya Utume wa Bahari Ilianzishwa rasmi tarehe 4 Oktoba 1920
Siku ya Utume wa Bahari Ilianzishwa rasmi tarehe 4 Oktoba 1920

Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa uwepo na utendaji wa Mapadre washauri wa maisha ya kiroho watu wa kujitolea pamoja na waamini wa Makanisa mahalia wanaojisadaka usiku na mchana ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za mabaharia na wavuvi zinaheshimiwa na kulindwa, ili kwa pamoja kuweza kujikita katika ujenzi wa umoja, ushirikiano na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anasema, Dominika ya Utume wa Bahari ni siku maalum ya kuwashukuru na kuwaenzi mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Waamini wamwombe Bikira Maria, Nyota ya Bahari kuwasindikiza wale wote wanaofanya utume wao Baharini pamoja na familia zao kumwendea Kristo Yesu.   Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu katika ujumbe wake kwa mwaka 2024, linasema, viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja na wote wamebatizwa katika Roho mmoja na kwamba, viungo vyote vinahitajiana na kukamilishana. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa kristo, na viungo kila kimoja peke yake. Rej. 1Kor 12: 12-27. Mabaharia na wavuvi ni viungo visivyoonekana kwa urahisi, lakini ni watu wenye mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea kila mwaka ifikapo Dominika ya Pili ya Mwezi Julai. Shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Utume wa Bahari ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya maisha ya mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao. Huu ni mwaliko kwa waamini kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao.

Dominika ya Utume wa Bahari Kwa mwaka 2024
Dominika ya Utume wa Bahari Kwa mwaka 2024

Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kuwahudumia mabaharia na wavuvi hawa wanaotekeleza dhamana na utume wao wakiwa mbali na nchi pamoja na makazi yao. Wote hawa wajisikie kupendwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa. Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa aliyejisadaka kutangaza na kushuhudia Injili akitembea Baharini ni mfano bora wa ujasiri, nguvu na ari inayowatia moyo mabaharia na wavuvi kuendelea kutekeleza dhamana na nyajibu zao. Waamini wa mji wa Korintho wakabahatika kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu. Kulipotokea hali ya mgawanyiko na kutoelewana, Mtume Paulo aliwataka waamini wa Kanisa la Korintho kujikita katika hekima na kuondokana na upuuzi. “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa;” 1Kor. 1:26. Huu ni mwaliko kwa Mama Kanisa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika ili kuepuka kinzani na mipasuko mbalimbali inayoweza kujitokeza, daima waamini wawe waaminifu kwa wito waliodhaminishwa na Kristo Yesu. Habari Njema ya Wokovu imetangazwa na kushuhudiwa sehemu mbalimbali za dunia kwa njia ya Utume wa Bahari, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendeleza wito huu wa ukarimu na upendo kwa wageni wanaotua nanga katika bahari na miji mbalimbali, tayari kushirikiana kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na ujenzi wa udugu wa kibinadamu na urafiki wa kijamii. Mama Kanisa anatambua mchango kwa wale wote wanaowahudumia mabaharia na wavuvi, ili waweze kuonekana. Huu ni mwaliko wa kuendeleza Injili ya ukarimu, utamaduni wa kusikilizana pamoja na kuwahakikishia ulinzi na usalama pamoja na kuwatakia kheri wale wote wanaotamani kurejea makwao kwa amani. Mabaharia na wavuvi waendelee kujisikia kuwa wako nyumbani, kila mahali wanapokwenda. Bikira Maria, Nyota ya Bahari, awasindikize wale wote wanaotekeleza utume wao baharini na kwenye Maziwa, awe kwao ni nyota inayowaongoza kumwelekea Kristo Yesu.

Utume wa Bahari
15 July 2024, 14:15