Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024   (Vatican Media)

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko Kwa Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Kwa Mwaka 2024

Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 yananogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Sala ya mkongwe “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9. Inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanagundua wakiwa wamechelewa kwamba, walishindwa kuwatendea vyema wazee; mwaliko waa kuwaonea huruma, kuwatendea wema na kuwatembelea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Siku ya Wazee Duniani itakayokuwa inaadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo Dominika ya Nne ya Mwezi Julai. Na kwa mwaka huu ni hapo Dominika tarehe 28 Julai 2024. Wazee ni amana na utajiri wa jamii; wao ni watunzaji wa mapokeo hai na wanayo mizizi ya jamii; mambo wanayopaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ni imani na mang’amuzi ya maisha. Inapendeza ikiwa kama wazee watakutana na wajukuu wao, ili kuendeleza amana na utajiri unaofumbatwa katika maisha yao! Inasikitisha kuona kwamba, mara nyingi wazee wanasahauliwa sana katika jamii. Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatakuwa yanakaribiana sana na Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. “Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote” Mt 28:20: Hii ni ahadi ya uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya na wazee, kushirikishana na hatimaye, kuwa ni wadau pia katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Siku ya Babu, Bibi na Wazee tarehe 28 Julai 2024
Siku ya Babu, Bibi na Wazee tarehe 28 Julai 2024

Siku ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ni matunda yanayobubujika kutoka katika Maadhimisho ya Mwaka wa Furaha ya Upendo Ndani ya Familia, “Famiglia Amoris Laetitia” uliozinduliwa rasmi tarehe 19 Machi 2021 na ukahitimishwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumi ya Familia Duniani hapo tarehe 26 Juni, 2022 kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Upendo wa familia: wito na njia ya utakatifu.” Siku ya Mababu, Mabibi na Wazee ni muda wa kuserebuka, kutoa faraja na kuonesha upendo kwa wazee, ili kujenga na kudumisha: Umoja, udugu, upendo na faraja tunu msingi katika maisha ya kijamii. Ni muda kwa waamini kujifunza sanaa ya kupenda na kupendwa na katika muktadha huu, wazee wanaweza kuwa magwiji kwa vijana wa kizazi kipya! Ndoto, kumbukumbu na sala ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati pamoja na waja wake. Wazee wawe ni wadau katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika maisha na utume wa Kanisa.

Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache Zab 71:9
Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache Zab 71:9

Wasaidiwe kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha ya kiroho, wahusishwe kikamilifu na uwepo wao uthaminiwe, na Kanisa liwe tayari kuchota hekima na busara kutoka kwa wazee hawa. Wazee wana mang’amuzi, ujuzi, maarifa na uzoefu wa miaka mingi, walisaidie Kanisa kupambana na changamoto mamboleo katika maisha na utume wake! Kwa hakika: babu, bibi na wazee ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 inayonogeshwa na kauli mbiu inayochota amana na utajiri wake kutoka katika Sala ya mkongwe “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 anasema, inasikitisha kuona kwamba, watu wengi wanagundua wakiwa wamechelewa kwamba, walishindwa kuwatendea vyema wazee. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanawaonea huruma wazee, kwa kuwatembelea mara kwa mara na kuwatia moyo, wale waliovunjika na kupondeka moyo na hivyo kujikatia tamaa ya maisha; tayari kuwarejeshea tena matumaini katika safari ya maisha yao!

Wazee ni amana na utajiri wa jamii
Wazee ni amana na utajiri wa jamii

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu kamwe hawatelekezi watoto wake, wala haangalii kama binadamu aangaliavyo na kwamba, kimsingi Maandiko Matakatifu ni simulizi la uaminifu wa upendo wa Mungu unaofumbatwa katika huruma katika kila hatua ya maisha hata katika uzee na kwamba, uzee kadiri ya Maandiko Matakatifu ni alama ya baraka. Maadhimisho haya yananogeshwa na kauli mbiu “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 kielelezo cha ukatili wa hali ya juu sana kutoka kwa mwanadamu kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu pale Mlimani Kalvari, kiasi cha Kristo Yesu kulia kwa sauti “Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Mt 27:46. Katika Maandiko Matakatifu, kumesheheni viashiria vya ukaribu wa Mungu katika maisha ya mwanadamu katika uzee, mateso na mahangaiko ya maisha bila kusahau upweke hasi unaowaandama hasa maskini, wazee na wazazi pweke. Upweke huu unaweza kusababishwa na vijana kuhama familia zao ili kutafuta maisha bora zaidi, vita, mila na desturi zilizopitwa na wakati. Hii inachangiwa pia na vijana kukwepa kutekeleza dhamana na majukumu yao kwa wazazi na walezi wao, mwaliko kwa vijana kupenda na kuthamini zawadi ya maisha.

Kanisa liwe tayari kuchota hekima na busara kutoka kwa wazee
Kanisa liwe tayari kuchota hekima na busara kutoka kwa wazee

Kauli mbiu: “Usinitupe wakati wa uzee, nguvu zangu zipungukapo usiniache” Zab 71:9 Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati mwingine, hii ni sera inayokita mizizi yake katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kibinafsi ambayo kamwe haitambui “dignita infinita” yaani “heshima isiyokuwa na ukomo.” Badala yake sera na mikakati kama hii inaunga mkono mchakato wa kudhibiti gharama ya maisha na wale wanaogharamia ni wazee, wanaoshutumiwa kwa kuwa ni mzigo usiobebeka na hivyo kutengwa. Kuna baadhi ya watu katika Jamii wanaamua kuishi katika hali ya upweke na inawawia vigumu kuishi na wengine. Wazee ni tabaka linalotaka kujitegemea kwa kudhani kwamba, wamekuwa mzigo kwa jamii na hivyo kutaka kujitegemea na hivyo kuwapatia vijana nafasi ya kufurahia maisha.

Vijana waoneshe upendo na mshikamano na wazee
Vijana waoneshe upendo na mshikamano na wazee

Lakini kama inavyojionesha kwenye Maandiko Matakatifu hasa katika kitabu cha Ruthu, ambapo Naomi anaamua kubaki na Ruthu kwani kama mwanamke mjane, aliona hana tena thamani mbele ya jamii, lakini Ruthu anamwonesha upendo na anahidi kutokumwacha kamwe katika uzee wake. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa Kristo Yesu, Bwana na Masiha, Imanueli, Mungu pamoja na waja wake katika hali zote. Hiki ni kielelezo cha uhuru na ujasiri unaoweza kubadili hatima ya wazee wengi, kwa kujikita katika uwepo wa karibu hata kama itabidi kutoa sadaka kubwa. Ruthu ni mfano bora wa kuigwa katika ulinzi na tunza bora kwa wazee. Ruth aliamua kukaa karibu na Naomi na kitendo hiki kikawa ni chemchemi ya baraka na neema ya kupata ndoa yenye furaha, uzao pamoja na ardhi. Kumbe, waamini kwa kukaa karibu na wazee, kwa kutambua dhamana na wajibu wao katika familia, Kanisa na jamii katika ujumla wake, wataweza kupata neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maadhimisho ya Siku ya Nne ya Babu, Bibi na Wazee Duniani, Dominika tarehe 28 Julai 2024 iwe ni fursa ya kuwafariji: babu, bibi na wazee walioko kwenye familia; iwe ni nafasi ya kuwatembelea na kuwasalimia wale wote waliovunjika na kupondeka moyo, kiasi cha kujikatia tamaa. Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi unaopelekea watu kumezwa na utamaduni wa kutupa na hivyo kuwatumbukiza watu wengi katika upweke hasi. Huu ni wito wa kuonesha moyo wa ujasiri na upendo kwa kushikamana na kutembea na babu, bibi na wazee, bila kuwageuzia kisogo hata kidogo!

Siku ya Wazee 2024
25 July 2024, 14:57