Tafuta

Wajumbe wa mkutano mkuu wa 19 wa Shirika la Neno la Mungu, tarehe 28 Juni 2024 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Wajumbe wa mkutano mkuu wa 19 wa Shirika la Neno la Mungu, tarehe 28 Juni 2024 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.   (Vatican Media)

Wamisionari wa Neno la Mungu: Wajenzi wa Amani na Manabii wa Matumaini

Baba Mtakatifu aliwataka wanashirika kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani na manabii wa matumaini. Katika ulimwengu uliojeruhiwa kwa vita na migogoro mbalimbali watu wa Mungu wanalilia amani mwaliko kwa wamisionari hawa kuwa ni wamisionari wa Kisinodi ndani ya Kanisa linalotoka kuinjilisha watu wa Mataifa. Mkutano mkuu ni muda muafaka wa kusali, kujadiliana, kusikilizana na hatimaye, kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu: karama na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Neno la Mungu “Society of the Divine Word; La Società del Verbo Divino”, kwa Kilatini “Societas Verbi Divini” lilianzishwa na Mtakatifu Arnold Janssen kunako tarehe 8 Septemba 1875 hadi wakati huu lina wanashirika zaidi 6, 000 wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi zaidi ya 79. Mheshimiwa Padre Paulus Budi Kleden, Mkuu wa Shirika la Neno la Mungu, tarehe 16 Juni 2024 alifungua rasmi maadhimisho ya Mkutano mkuu wa 19 wa Shirika la Neno la Mungu kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Nuru yenu na iangaze mbele ya watu” (Mt 5:16): “Wanafunzi waaminifu na wabunifu katika ulimwengu uliojeruhiwa.” Mkutano unafungwa rasmi tarehe 14 Julai 2024. Wajumbe wa mkutano mkuu wa 19 wa Shirika la Neno la Mungu, tarehe 28 Juni 2024 walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika hotuba yake Baba Mtakatifu aliwataka wanashirika kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani na manabii wa matumaini. Katika ulimwengu uliojeruhiwa kwa vita, kinzani na migogoro mbalimbali watu wa Mungu wanalilia amani, changamoto na mwaliko kwa wamisionari hawa kuwa ni wamisionari wa Kisinodi ndani ya Kanisa linalotoka kifua mbele kwenda kuinjilisha watu wa Mataifa. Mkutano mkuu ni muda muafaka wa kusali, kujadiliana, kusikilizana na hatimaye, kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu: karama na utume mintarafu mustakabali wa Shirika kwa sasa na kwa siku za usoni. Ni wakati wa kurejea katika chemchemi ya utambulisho na utume wa Shirika, ambao ni Kristo Yesu, Neno la Uzima wa milele, ufunuo wa Sura ya huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Kristo Yesu, Nuru ya Ulimwengu anawachangamotisha wafuasi wake kuhakikisha kwamba, nuru yao inaangaza mbele ya watu, kwa kujishikamanisha katika pendo lake na hatimaye, kulitolea ushuhuda.

Wamisionari wa Neno la Mungu Wajenzi wa amani na Manabii wa Matumaini
Wamisionari wa Neno la Mungu Wajenzi wa amani na Manabii wa Matumaini

Baba Mtakatifu Francisko anasema waamini wanapaswa kujifunza Maandiko Matakatifu, Neno la Mungu litajirishe katekesi na juhudi za kurithisha imani na kwamba, mchakato wa uinjilishaji unadai hali ya kulizoea Neno la Mungu, changamoto wa kulisoma na kulisali Neno la Mungu ambalo kimsingi ni hazina tukufu ya Neno lililofunuliwa. Rej. Evangelii gaudium, 175. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa kweli ni wamisionari waaminifu kwa wito walioupokea mintarafu neema ya Mungu, tayari kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa furaha ya Injili, huruma na upendo wa Mungu, tayari kuwasha moto wa mapendo unaopyaisha, takasa na kuwakirimia waamini ari na mwamko mpya, licha ya dhambi na udhaifu wa kibinadamu, lakini waamini imara, wajasiri na watu wanaojiaminisha chini ya huruma na upendo wa Mungu, tayari kupokea na kukumbatia msamaha wa dhambi, nao kwa upande wao wakiwa kweli ni vyombo vya huruma na msamaha wa Mungu. Wamisionari hawa wanapaswa kuwa ni wabunifu, wakichota neema na utajiri unaobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu na katika karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, kwa kutambua kwamba, wao ni washirika hai wa utume wa Kristo Yesu, anayetenda kazi ndani yao kwa njia ya Roho Mtakatifu. Wanapotangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, yaani uinjilishaji wajitahidi kuhakikisha kwamba, ufalme wa Mungu unasimikwa duniani kwa kuunganisha nguvu na karama binafsi, zile za kijumuiya na zile za Kanisa zima. Kumbe, kama wamisionari wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani katika dunia ambayo imejeruhiwa kutokana na vita, kinzani sanjari na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Amani ni kilio kikubwa cha watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni ile amani iliyotolewa na Kristo Mfufuka. Hii ni amani inayopaswa kuwafumbata na kuwakumbatia watu wote, lakini hasa: Maskini, wakimbizi na wahamiaji, wanawake na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, bila kuwasahau watu wanaoteseka kutokana na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo.

Jubilei ya Miaka 150: Tarehe 8 Septemba 2025
Jubilei ya Miaka 150: Tarehe 8 Septemba 2025

Wamisionari hawa wawe ni vyombo na wajenzi wa matumaini kwa kila watu na tamaduni zao; watoe matumaini na wawe kweli ni vyombo vya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Kwa njia ya Ubatizo na Karama ya Shirika lao, wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili kama ilivyokuwa kwenye ile Pentekoste ya kwanza, wote wakawa wakizungumza lugha moja ya upendo, iliyowawezesha kuelewana; waendelee kubobea katika mchakato wa utamadunisho unaohitaji kufanyiwa mang’amuzi. Baba Mtakatifu Francisko anawataka wamisionari hawa kuwa na matumizi bora zaidi ya intenet na mitandao ya kijamii, kwa kujikita katika utamaduni wa upendo na matumaini unaobubujika kutoka katika tunu msingi za maisha ya kitawa na Kipadre, huku wakiwa huru. Waendeleee kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza, ili kila mtu aweze kujisikia kwamba, anapendwa na kupokelewa jinsi alivyo. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Wamisionari wa Shirika la Neno la Mungu kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi katika medani mbalimbali za maisha na utume wao. Shirika la Neno la Mungu “Society of the Divine Word” tarehe 8 Septemba 2025 litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu Shirika hili lilipoanzishwa. Ni muda wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuwawezesha kwenda sehemu mbalimbali za dunia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kuwagawia watu wa Mungu upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; kuwahudumia maskini, kutafuta na kuambata haki na amani kwa ajili ya watu wa Mungu; kutoa elimu kwa watu watakatifu wa Mungu sanjari na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kumbe, huu utakuwa ni muda muafaka wa kushirikisha ile furaha ya Injili kama ilivyotangazwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Arnold Janssen aliyeweza kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume kwa njia ya Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa wafuasi wake leo hii kuendeleza karama hii, kwa njia ya mang’amuzi ya kijumuiya na kutenda kwa ujasiiri katika hali ya unyenyekevu kwa kuendelea kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu.

Shirika la Neno la Mungu
03 July 2024, 14:54