Tafuta

Wanawake na Utume wa Kanisa la Kisinodi: Majadiliano ya Wazi! Ni Kitabu kilicho tungwa na waandikishi watano, kwa kuwahusisha viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Wanawake na Utume wa Kanisa la Kisinodi: Majadiliano ya Wazi! Ni Kitabu kilicho tungwa na waandikishi watano, kwa kuwahusisha viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu.  (Vatican Media)

Wanawake na Utume wa Kanisa la Kisinodi: Majadiliano ya Wazi

Wanawake na Utume wa Kanisa la Kisinodi: Majadiliano ya Wazi! Ni Kitabu kilicho tungwa na waandishi watano, kwa kuwahusisha viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu, kufuatia mchakato wa majadiliano kati ya Makardinali washauri wakuu wa Baba Mtakatifu Francisko na dibaji yake imeandikwa na Baba Mtakatifu Francisko anayesema kwamba, mambo halisi ni muhimu kushinda fikra na kwamba, hali halisi ni kubwa kuliko fikra. Wanawake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake ili waweze kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Bila mchango wa wanawake, Kanisa litapoteza nguvu yake ya kujipyaisha tena. Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji mpya. Kumbe, Kanisa linapaswa kushikamana pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kitamaduni na kijamii kwa watoto wao. Itakumbukwa kwamba, wanaume na wanawake, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wapendane na kukamilishana; bila kuwadharau, kuwabeza na kuwanyanyasa wanawake. Wanawake washirikishwe pia katika malezi na majiundo ya Majandokasisi. Sauti ya wanawake, inapaswa kusikilizwa ndani ya Kanisa. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wanasema, wanawake ni rasilimali muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake washirikishwe katika mchakato wa kufanya maamuzi katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria awe ni mfano bora katika shule ya ufuasi wa Kristo Yesu. Vijana wawe ni nyota ya Msamaria mwema kwa njia ya huduma; nyota ya umisionari, matumaini na majadiliano ya: Kitamaduni, kidini na kiekumene. Kimsingi, Mababa wa Sinodi wanakaza kusema, dhamana na utume wa wanawake katika Kanisa hauna budi kuimarishwa, kwa kukazia zaidi makuzi, malezi na majiundo ya awali, endelevu na fungamani, ili kuondokana na mfumo dume unaowanyima wanawake haki zao msingi. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni mambo muhimu katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu.

Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa
Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna haja ya kutambua kwamba, kuna usawa na utofauti, kama kielelezo makini kinachotafuta uwiano mzuri unaojikita katika mahusiano dhidi ya utamaduni wa mfumo dume unaoendelea kumkandamiza mwanamke. Kuna haja ya kuvuka kishawishi cha kudhani kwamba, wote ni sawa sawa, kwa kushindwa kutambua tofauti, katika utambulisho wa mtu na asili yake, kwani mwanamke na mwanaume wanakamilishana. Pili, Baba Mtakatifu anasema, uwezo wa mwanamke kuzaa ni kanuni na utambulisho maalum kwa wanawake ambao wamejaliwa uwezo wa kuendeleza zawadi ya maisha, kwa kuilinda na kuidumisha. Kanisa linapenda kuwapongeza wanawake kwa mchango wao katika medani mbalimbali za maisha ya mwandamu; kwani wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu na majiundo; shughuli na mikakati mbalimbali ya kichungaji na kwamba, wanawake wanaonesha sura ya huruma ya Mungu kwa binadamu. Ni watu wanaojisadaka kwa njia ya huduma, kwa kuonesha ukarimu, kimsingi, wanawake ni sawa na tumbo la Kanisa linalopokea na kuzaa maisha. Tatu, Baba Mtakatifu Francisko anajaribu kuangalia mwili wa mwanamke kati ya tamaduni na bayolojia, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanamke mwili unaopendeza, lakini pia umesheheni madonda ambayo wakati mwingine yamesababishwa na dhuluma pamoja na nyanyaso. Mwili wa mwanamke ni kielelezo cha maisha, lakini kwa bahati mbaya, unaharibiwa hata na wale ambao walipaswa kuwalinda na kuwasindikiza katika maisha!

Wanawake wakiwezeshwa wanaweza kufanya mageuzi makubwa kijamii
Wanawake wakiwezeshwa wanaweza kufanya mageuzi makubwa kijamii

Kuna mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo, biashara ya ngono na vitendo vya ukeketaji; mambo ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuyavalia njuga, ili kusitisha vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima ya wanawake duniani, kiasi cha kuwageuza kuwa kama bidhaa inayouzwa sokoni, bila kusahau umaskini unaosababisha wanawake wengi kuishi katika mazingira magumu na hatarishi; kiasi hata cha kunyanyaswa, kielelezo cha utamaduni usiojali wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine. Nne, Baba Mtakatifu anapopembua kuhusu wanawake na dini: mwelekeo wa kutafuta ushiriki katika maisha na utume wa Kanisa anakiri kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wanawake wanashiriki kwa ukamilifu zaidi katika utekelezaji wa dira na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Kanisa. Wanawake ni wadau wakuu katika kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ni watu wenye utajiri mkubwa, wanaoweza kusaidia upatikanaji wa amani na utulivu; wito na utume maalum kwa wanawake. Ziwepo juhudi za makusudi ili kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha ya hadhara, katika medani mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa: mahali panapotolewa maamuzi na utekelezaji wa mikakati na sera mbali mbali; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha ya kifamilia. Wanawake wasaidiwe kufanya maamuzi machungu katika maisha, kwa kuwajibika barabara katika jamii na katika maisha na utume wa Kanisa.

Wanawake wakatoliki wajenzi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu
Wanawake wakatoliki wajenzi wa mafungamano ya udugu wa kibinadamu

Wanawake na Utume wa Kanisa la Kisinodi: Majadiliano ya Wazi! Ni Kitabu kilicho tungwa na waandishi watano, kwa kuwahusisha viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu, kufuatia mchakato wa majadiliano kati ya Makardinali washauri wakuu wa Baba Mtakatifu Francisko. Kitabu hiki kimechapishwa na Pauline, Milano na kina kurasa 109 na dibaji yake imeandikwa na Baba Mtakatifu Francisko anayesema kwamba, mambo halisi ni muhimu kushinda fikra na kwamba, hali halisi ni kubwa kuliko fikra. Kanuni hii inahimiza kukataa njia mbalimbali za kuficha uhalisia wa mambo. Kinachomwita mtu kwenye utendaji ni mambo halisi yaliyoangaziwa na akili inayomwezesha mtu kuangalia mambo bila ya upendeleo. Rej. Evangelii gaudium 231-232. Mjadala kuhusu wanawake na utume wa Kanisa la Kisinodi ni tema tete sana katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu mwelekeo wake wa Kitaalimungu, Kisheria na katika Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium.” Watu wengi wameteleza na kuanguka pengine hata Kanisa mintarafu uaminifu wake kwamba dhana ni muhimu zaidi kuliko kujizatiti katika hali halisi. Utume na maisha ya wanawake katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi si tema mpya. Kuna haja kwa Kanisa kufungua macho na kuangalia “janga la matumizi mabaya ya madaraka kwa wakleri: Clericalism.” Kashfa hii ni kumbakumba inaweza kuwagusa watu wote, hata waamini walei na wanawake katika ujumla wao. Huu ni mwaliko wa kukaa kitako na kusikiliza kilio na furaha ya wanawake pasi na kuathirika na maamuzi mbele.

Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa
Wanawake wanao mchango mkubwa katika maendeleo na ustawi wa Kanisa

Wanawake wengi wanateseka sana kwa kutotambuliwa utu, heshima na haki zao msingi na wakati mwingine, hawatambuliwi jinsi walivyo na wale walioko karibu nao, wenye nyajibu juu ya maisha yao; ili waweze kujiandaa tayari kujizatiti katika kushiriki ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kitabu hiki ni matunda ya tafakari zilizotolewa na wanawake watatu kwenye Mkutano wa Baraza la Makardinali Washauri. Hiki ni Kitabu kinachoanza na ukweli wa mambo pamoja na tafsiri yake ya hekima katika mang’amuzi na uzoefu wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi mintarafu mang’amuzi yake unachota dhamana na mang’amuzi yake kutoka katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ukweli na mang’amuzi yake sanjari na uaminifu wake katika ubunifu mintarafu Mapokeo ya Kanisa. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu anapenda kuuweka mchakato wa mang’amuzi ya hali ya juu kuhusu utume na wahudumu wa Kanisa la Kisinodi chini ya tunza na maombezi ya watakatifu, walioishi, wakasikiliza na kugusa kwa mikono yao, na hatimaye, kushiriki katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa kama walivyofanya: Bikira Maria, Mtakatifu Petro na Yohane; Maria Madgalena, kwa kuwataja watakatifu wachache tu bila kuwasahau watakatifu wengi wanaofahamika kwa sura na majukumu yao ndani ya Kanisa kama wafuasi na wamisionari wa wa Injili, wawasaidie kutafasiri kwa uaminifu na ubunifu mkubwa nia za Kristo Yesu.

Papa Dibaji

 

12 July 2024, 14:57