Watu wa Mungu Nchini Ukraine Wana Kiu ya Haki na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Madhabahu ni mahali ambapo panapaswa kukuza na kudumisha ari na moyo wa Sala ya Kanisa, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kama sehemu ya kazi ya ukombozi. Ni mahali pa shuhuda za: imani, matumaini na mapendo, kielelezo cha Kanisa linalokesha na kusali daima! Madhabahu ni mahali pa ukimya unaopaswa kububujika kutoka katika undani wa mahujaji, tayari kuomba: baraka, neema na rehema pamoja na kudumisha upendo kwa Mungu na jirani! Madhabahu ni mahali pa kuonja huruma na upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu. Maeneo kama haya yanahitaji wakleri waliofundwa barabara, watakatifu, vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, katika madhabahu, kamwe hawatakosekana Wamisionari wa huruma, mashuhuda wa upendo wa Mungu unaokoa na kuponya! Madhabahu yawe ni mahali pa kumwilisha upendo, kielelezo cha utekelezaji wa Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani! Ni katika muktadha huu wa hija ya watu wa Mungu, Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alimteuwa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuwa ni Mwakilishi wake katika maadhimisho ya kufunga hija ya watu wa Mungu kutoka katika Madhehebu ya Kilatini kutoka sehemu mbalimbali za Ukraine, Dominika tarehe 21 Julai 2024 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli wa Berdychiv.
Kardinali Parolin, katika Ibada hii alifuatana na Padre Ruslan MYKHALKIV, Gambera wa Seminari ya Jimbo Katoliki la Kyiv-Zhytomir; pamoja na Padre Andriy LEHOVICH, Katibu muhtasi wa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lviv, nchini Ukraine. Madhabahu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli wa Berdychiv yalitambuliwa kuwa ni Madhabahu ya Kitaifa kunako mwaka 2011 na yanasimamiwa na kuendeshwa na Watawa wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli, huduma inayotekelezwa kwa ibada na uaminifu na uchaji mkuu. Uwepo wa Kardinali Parolin katika maadhimisho haya ni kielelezo cha ukaribu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa watu wa Mungu nchini Ukraine. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahubiri yaliyosomwa kwa niaba yake na Askofu Msaidizi Edward Kawa wa Jimbo la Lviv la Kanisa Katoliki la Ukraine amekazia muujiza unaotamaniwa ni amani, watu wa Mungu nchini Ukraine kama ilivyokuwa kwa Nabii Eliya wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika fadhila ya amani, kwani hakuna jambo ambalo haliwezekani kwa Mungu, waamini waendelee kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine na sehemu mbalimbali za dunia. Madhabahu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli wa Berdychiv ni eneo la sala kwa ajili ya kumshukuru, kumtukuza na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia waja wale muujiza wa amani, kama ambavyo inashuhudiwa katika Madhabahu haya kunako mwaka 1627 na mwaka 1642.
Hii inaonesha kwamba, hakuna jambo lisilowezekana mbele ya Mungu. Somo la pili linakazia kuhusu toba na wongofu wa ndani. Watu wa Mungu nchini Ukraine wanaitwa na kutumwa kutekeleza unabii wa kusali bila ya kuchoka, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaongoa wenye kiburi, wanaopandikiza mbegu ya chuki na uhasama, vita na kifo, ili waweze kusitisha vitendo hivi vinavyosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Chanzo kikuu cha vita ni watu kutaka kujimwambafai, ubadhirifu na kuonesha ufahari na matokeo yake ni mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia. Lakini, baada ya Ijumaa kuu, kuna Pasaka: Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Wakati huu, Ukraine inaishi na kutembea kwenye uvuli wa mauti na kwamba, iko siku haki na amani vitatawala na katika hija hii ya maisha, Bikira Maria wa Mlima Karmeli anawaongoza, kama ilivyokuwa Siku ile ya Ijumaa kuu, alipomfuata Mwanaye wa pekee katika njia ya Msalaba. Ndiyo maana watu wa Mungu kwa maombezi ya Bikira Maria wanapenda kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee amani nchini Ukraine. “Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” Lk 1:37. Lengo la siku hii ni kuombea amani na usalama; ili watoto waweze kuishi katika mazingira ya amani na usalama; familia ziwe ni kitovu cha upendo; wagonjwa na wazee wapate rehema na faraja; watu wa Mungu nchini Ukraine wapate ulinzi; mateka na wafungwa wa vita wapate fursa ya kurejea makwao na wale waliopoteza maisha wapate rehema kwa Mungu wapumzike kwa amani.