Tafuta

Utambulisho, historia na matarajio ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbanian ni kati ya ajenda za mkutano mkuu maalum wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwa mwaka 2024. Utambulisho, historia na matarajio ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbanian ni kati ya ajenda za mkutano mkuu maalum wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwa mwaka 2024.  (Vatican Media)

Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu: Hatima ya Chuo Kikuu cha Urbaniana

Baba Mtakatifu katika hotuba yake amelishukuru Baraza kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; utambulisho na utume wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, matarajio kwa siku za usoni yanayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu na matumizi bora ya rasilimali fedha na watu, ili Chuo kikuu cha Urbaniana kiweze kuibuka kikiwa bora zaidi katika majiundo yake ya kiakili, na kimisionari katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwongozo wa Malezi ya Kipadre unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis” yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na majiundo ya kipadre ambayo yanapaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee. Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo anakabiliana na changamoto nyingi kati yake ni: Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa.

Mkutano Maalum wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, 2024
Mkutano Maalum wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, 2024

Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma kilianzishwa kunako mwaka 1627 ili kutoa majiundo makini kwa viongozi wa Makanisa mahalia, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kwa kujikita katika malezi na majiundo ya kiakili, kichungaji na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu Francisko anakazia pia wongofu wa kimisionari na shughuli za kichungaji. Utambulisho, historia na matarajio ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana ni kati ya ajenda za mkutano mkuu maalum wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, ambalo limekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 30 Agosti 2024 mjini Vatican. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amelishukuru Baraza kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi; utambulisho na utume wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, matarajio kwa siku za usoni yanayofumbatwa katika kipaji cha ubunifu na matumizi bora ya rasilimali fedha na watu, ili Chuo kikuu cha Urbaniana kiweze kuibuka kikiwa bora zaidi katika majiundo yake ya kiakili, na kimisionari katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete.

Hatima ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, 2024
Hatima ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, 2024

Baba Mtakatifu amelipongeza Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kwa kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake, kwa kushirikiana kwa karibu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilicho chini ya uongozi na usimamizi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na kwamba, Chuo hiki kina utambulisho wake maalum unaofumbatwa katika utume wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Rej. Mk 16:15. Kwa kusoma alama za nyakati chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu, kuna haja ya kufanya marekebisho makubwa si tu katika mchakato wa kurithisha ufahamu, ujuzi na maarifa, bali kuwasaidia wanafunzi kuwa na nyenzo za kiakili muhimu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwa wazi na makini katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, matarajio ya Vyuo vikuu vya Kipapa vilivyoko mjini Roma ni tema inayoshughulikiwa kwa sasa na Vatican, ili kuhakikisha kwamba, kuna matumizi bora zaidi ya rasilimali watu, fedha na maboresho ya kiuchumi.

Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete
Uinjilishaji na utamadunisho ni chanda na pete

Ni majiundo yanayopaswa kuzingatia hali ya Kikanisa na kijamii, mahitaji ya Makanisa mahalia; wito na maisha ya Kipadre na Kitawa. Huduma za kichungaji katika ufunguo wa kimisionari zinajikita katika ujasiri na ubunifu kwa kufikiria upya malengo, miundo, mitindo na njia za uinjilishaji na kwamba, Kanisa linahitaji sana kipaji cha ubunifu na ujenzi wa mtandao wa vyuo vikuu vya Kipapa mjini Roma. Rej. Evangelium gaudium, 33. Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kisijikite tu katika masomo, ufanisi na ufaulu wa mitihani. Chuo hiki kiwe na uwezo wa kuwaunda watu katika mafundisho tanzu ya Kanisa, matumizi bora na sahihi ya rasilimali watu; kwa kubana matumizi na kuondokana na mifumo ambayo kwa sasa imepitwa na wakati. Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kijipambanue katika ubora wake wa majiundo na makuzi ya kimisionari na kiakili, kwa kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete anasema Baba Mtakatifu Francisko. Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana tayari kina uzoefu mkubwa wa uundaji wa vituo vikubwa vya tafiti kijiografia na kitamaduni kama ilivyo Barani Asia na China. Kumbe, huduma hii inaweza kuboreshwa katika mazingira mbalimbali kwa Makanisa mahalia, kwa kuendelea kuvisindikiza vituo hivi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia utume mwema unaojikita katika maudhui ya Makanisa mahalia; Roho Mtakatifu awakirimie hekima na busara katika tafakari na majadiliano wakati wa mkutano huu maalum. Bikira Maria, Malkia wa utume, awalinde na kuwaombea.

Papa Chuo Kikuu
30 August 2024, 15:40