Bikira Maria Malkia wa Amani na Faraja Ya Watu Wanaoteseka Kwa Vita na Mipasuko ya Kijamii
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni mwili na roho, Alhamisi tarehe 15 Agosti 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican aliyaelekeza mawazo na sala zake kwa watu wa Mungu huko Ukraine wanaoendelea kuuwawa kama mashuhuda; Mashariki ya Kati, Palestina, Israeli pamoja na Myanmar. Wote hawa wapate matumaini na faraja kutoka kwa Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni, ili hatimaye, waweze kuwa na amani, utulivu na usawa kwa watu wote. Baba Mtakatifu alitumia fursa hii, kumkabidhi Bikira Maria aliyepalizwa mbinguni mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na mipasuko ya kijamii pamoja na vita.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, anafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali ya kibinadamu huko Ukanda wa Gaza na kwa mara nyingine, anawaalika wahusika wa pande zote mbili kusitisha mapigano; kuwaachilia huru mateka na wafungwa wa kivita na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa sasa ijielekeze kuwasaidia watu wa Mungu wanaoteseka na kusiginwa na baa la njaa. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wahusika wa pande zote mbili kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, ili hatimaye, vita hii iweze kufikia hatima yake. Watu watambue kwamba vita ni dalili za mwanadamu kushindwa.