Familia za Wahanga wa Mlipuko wa Bandari ya Beiruti: Haki, Ukweli na Uwajibikaji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ilikuwa ni tarehe 4 Agosti 2020 mlipuko mkubwa ulipotokea kwenye bandari ya Beirut nchini Lebanon na hivyo kusababisha watu zaidi ya 2,000 kupoteza maisha, watu 6, 500 kujeruhiwa vibaya sana pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Taarifa za awali zilionesha kwamba chanzo ni kulipuka kwa “Ammonium Nitrate” Tani 2750 iliyokuwa imehifadhiwa bandarini hapo. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa familia za wahanga wa mlipuko wa bandari ya Lebanon, tarehe 26 Agosti 2024 anasema, anamshukuru Mungu kwa kuweza kuwa pamoja nao; anawakumbuka na kuwaombea wale wote waliopoteza maisha yao katika mlipuko wa bandari ya Beiruti, anautafakari uso wa Mtoto Alexandra ambaye kwa sasa yuko mbinguni. Hao waliotangulia mbele za haki, wanatazama mahangaiko ya ndugu zao na kuwaombea, ili kipeo hiki kiweze kufikia hatima yake. Baba Mtakatifu anasema, watu wa Mungu wanataka kuona haki na ukweli vikitamalaki, ili kuwepo na uwajibikaji katika dhana ya ukweli na uwazi. Baba Mtakatifu anasikitika kuona kwamba, bado kuna watu wengi wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na kinzani na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati; Palestina na Israeli wanapambana vikali, lakini Lebanon inalipa gharama ya vita hii. Anasema, kila vita huacha makovu ulimwenguni na kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. “Vita ni kushindwa kwa siasa na ubinadamu, kujisalimisha kwa aibu, kushindwa kwa nguvu mbele ya nguvu za uovu.” Baba Mtakatifu kwa kushirikiana na watu wa Mungu nchini Lebanon anaendelea kuombea amani nchini Lebanon na Mashariki ya Kati katika ujumla wake. Lebanon inapaswa kuendelea kuwa ni sehemu ya mradi wa amani, mahali ambapo jumuiya za watu mbalimbali zinaishi kwa pamoja katika amani na utulivu; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu.
Baba Mtakatifu amezihakikishia familia za wahanga uwepo wake angavu na wa Kanisa na watambue kwamba, Kanisa nchini Lebanon liko bega kwa bega pamoja nao. Kamwe wasijisikie wapweke kwani Kanisa litaendelea kuwaonesha mshikamano, kwa njia ya sala na Injili ya upendo katika uhalisia wa maisha yao. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wingi wa imani, matumaini na ustawi kama Mwerezi wa Lebanon, utambulisho wa nchi ya Lebanon, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kuinua nyuso zao juu mbinguni kwa Mwenyezi Mungu ambaye kimsingi ni chemchemi ya matumaini ambayo kamwe hayamdanganyi mtu. Bikira Maria wa Harissa, aendelee kuwaangalia wananchi wa Lebanon kwa macho yake yenye huruma. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1991, Mtakatifu Yohane Paulo II aliitisha Siku Maalum ya Sala kwa ajili ya Lebanon na baadaye mwaka 1995 yakafuatia maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki. Viongozi hawa kwa mwaka 2021 wakasali na kumwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awakirimie watoto wake wa Lebanon amani ya kudumu. Viongozi hawa wakawasha Mshumaa wa matumaini kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro, kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Baadaye Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wageni wake wakashiriki kwenye vipindi vitatu vya majadiliano ya faragha. Baadaye, majira ya jioni, kwa pamoja wakaadhimisha Liturujia ya Kiekumene iliyoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Watu wa Mungu nchini Lebanon alioutoa wakati wa Liturujia ya Kiekumene tarehe 2 Julai 2021 kwa ajili ya kuombea amani; aliomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu kwa niaba ya viongozi wa Makanisa walioshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.
Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani. Ni wito wa Lebanon kuwa ni nchi inayokita mizizi yake katika uzoefu wa amani, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Lebanon kuzamisha mizizi yao katika ndoto ya amani, tayari kung’arisha mwanga wa matumaini. Baba Mtakatifu alianza ujumbe wake kwa kuwashukuru viongozi wote walioitikia wito wake wa kusali, kutafakari na kuombea amani Lebanon, sanjari na kufanya toba, ili kuomba msamaha na huruma ya Mungu pale waliposhindwa kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Injili ya Kristo. Lakini zaidi pale ambapo wameshindwa kutumia kikamilifu njia ya udugu wa kibinadamu, upatanisho na umoja kamili. Kwa mapungufu yote haya wanamwomba Mwenyezi Mungu msamaha wa kweli. Anasema, kamwe wasichoke kumlilia Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, ili aweze kuwakirimia waja wake amani ya kudumu. Nchi ya Lebanon ni amana na utajiri wa ustaarabu pamoja na tasaufi ambayo imekuwa ni chemchemi ya maridhiano na amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ujumbe unaosikika kwa wakati huu kutoka Mashariki ya Kati ni amani na udugu wa kibinadamu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon na huu ni mradi unaopaswa kudumu katika amani, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kumezwa na malimwengu. Wito wa Lebanon unapaswa kuwa ni nchi ya maridhiano na ya watu wengi, chemchemi ya udugu wa kibinadamu unaosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi wa kisiasa walioko madarakani, wanapaswa kujizatiti zaidi kutafuta na kudumisha amani ya kweli na kamwe wasitafute masilahi yao binafsi. Na kamwe watu wachache wasiendelee kufaidika kwa mateso na mahangaiko ya wananchi wa Lebanon na kwamba, watu wanataka kusikia ukweli wote kuhusu hatima ya maisha yao. Lebanon na Mashariki ya Kati katika ujumla wake, “lisiwe ni pango la wevi” kwa ajili ya masilahi ya watu wachache, wanaotaka faida na utajiri wa haraka haraka. Baba Mtakatifu anawakumbusha watu wa Mungu nchini Lebanon kwamba, Mwenyezi Mungu ana mawazo ya amani; anao mpango mkakati kwa ajili ya amani huko Lebanon. Umoja na tofauti zao msingi ziliwawezesha wahenga wa Lebanon kuishi kwa pamoja. Huu ni wakati wa kuzamisha mizizi kwa ajili ya ndoto ya amani, kwa kushirikiana na wengine. Wananchi wasikate tamaa bali waendelee kuwa na matumaini. Viongozi wa kisiasa kadiri ya wajibu wao watafute majibu ya matatizo na changamoto za kiuchumi kwa kujikita katika haki kama msingi wa amani. Wananchi wa diaspora kutoka Lebanon, wajifunge kibwewe kwa ajili ya kuwasaidia ndugu zao huko Lebanon. Jumuiya ya Kimataifa isaidie juhudi za kufufua uchumi nchini Lebanon; yote haya ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu anasema, ikiwa kama Lebanon inataka kujenga na kudumisha amani; wote wanapaswa kuungana na kushikamana ili kutenda katika umoja, upendo na huruma. Wakristo wanaitwa na kuchangamotishwa kuwa ni wapanzi wa amani na wajenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa kuwajibika kikamilifu sanjari na kuendelea kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika njia ya amani. Majadiliano ya kidini na kiekumene yaimarishe mchakato wa umoja na mshikamano, tayari kufanya kazi kwa pamoja kama ndugu! Katika amani hakuna mshindi wala anayeshindwa. Ni wakati wa kunogesha majadiliano, kukuza na kudumisha elimu na mshikamano wa kweli. Katika pazia la usiku wa giza nene, kuna mapambazuko ya matumaini kama walivyoonesha vijana waliowakabidhi viongozi wa kidini mishumaa inayowaka, kielelezo cha matumaini kwa sasa na kwa siku zijazo. Katika mchakato wa kufanya maamuzi, viongozi watambue na kukumbuka kwamba, watu wanataka kuona mwanga wa matumaini ukiwashwa katika safari ya maisha yao. Viongozi waongozwe na mang’amuzi yanayobubujika kutoka katika dhamiri nyofu, ili kuwashirikisha watu wa Mungu matumaini mapya. Wanawake wathaminiwe na kushirikishwa katika vikao vyote vinavyotoa maamuzi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Lebanon. Katika kipindi hiki cha kinzani, migogoro na mipasuko ya kijamii, changamoto kubwa ni wote kushikamana na kuungana ili kuwa ni kitu kimoja. Kwa njia hii wataweza kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; ili kuendeleza nia njema, ili hatimaye, kuwasha mwanga wa matumaini pale penye giza. Mwisho mwa ujumbe wake kwa watu wa Mungu nchini Lebanon, Baba Mtakatifu aliwaaminisha wote chini ya ulinzi na tunza ya Kristo Yesu, Mfalme wa amani, ili awakirimie huruma na matumaini! Usiku wa kinzani na migogoro utoweke; mapambazuko ya matumaini yaangaze, chuki na uhasama vikome, Lebanon irejee tena kuangaza nuru ya amani.