Askofu mkuu Noël Treanor, Balozi wa Vatican kwenye Nchi za Umoja wa Ulaya, EU amefariki dunia tarehe 11 Agosti 2024 akiwa na umri wa miaka 73. Askofu mkuu Noël Treanor, Balozi wa Vatican kwenye Nchi za Umoja wa Ulaya, EU amefariki dunia tarehe 11 Agosti 2024 akiwa na umri wa miaka 73.  

Fumbo la Kifo Katika Maisha ya Mwanadamu: Askofu mkuu Noel Treanor: 1950-2024

Askofu mkuu Noël Treanor, Balozi wa Vatican kwenye Nchi za Umoja wa Ulaya, EU amefariki dunia tarehe 11 Agosti 2024 akiwa na umri wa miaka 73. Alikuwa ni mtu wa majadiliano katika ukweli na uwazi; aliyesimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Alizaliwa kunako mwaka 1950. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre Mwaka 1976, akawekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 29 Juni 2008; Mwaka 2022 akateuliwa kuwa Askofu mkuu, cheo binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la mateso na Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi!

Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu
Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu

Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!  Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza.

Askofu mkuu Noel Treanor, Balozi wa Vatican Umoja wa Ulaya amefariki dunia
Askofu mkuu Noel Treanor, Balozi wa Vatican Umoja wa Ulaya amefariki dunia

Baba Mtakatifu anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono duniani Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo!

Askofu mkuu Noel Treanor, Balozi wa Vatican kwenye Umoja wa Ulaya
Askofu mkuu Noel Treanor, Balozi wa Vatican kwenye Umoja wa Ulaya

Askofu mkuu Noël Treanor, Balozi wa Vatican kwenye Nchi za Umoja wa Ulaya, EU amefariki dunia tarehe 11 Agosti 2024 akiwa na umri wa miaka 73. Alikuwa ni mtu wa majadiliano katika ukweli na uwazi; aliyesimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Noël Treanor, alizaliwa tarehe 25 Desemba 1950 huko Silverstream, Kitongoji cha Monaghan Tyholland, Jimbo Katoliki la Clogher, Ireland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi tarehe 13 Juni 1976 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre kwa ajili ya Jimbo Katoliki la Clogher lililoko nchini Ireland. Baba Mtakatifu Benedikto XVI tarehe 22 Februari 2008 akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Down na Connor, nchini Ireland na hatimaye, akawekwa wakfu tarehe 29 Juni 2008. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 26 Novemba 2022 akamteuwa kuwa ni Balozi wa Vatican kwenye Nchi za Umoja wa Ulaya, na hivyo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu, cheo binafsi. Tarehe 11 Agosti 2024 akafariki dunia huko Mechelen-Brussel (Malines-Brussels), nchini Ubelgiji.

Fumbo la kifo katika maisha ya binadamu
Fumbo la kifo katika maisha ya binadamu

Kwa ufupi kabisa Hayati Askofu mkuu Noël Treanor, Balozi wa Vatican kwenye Nchi za Umoja wa Ulaya, EU, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 73; amelitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 48 na kama Askofu akifundisha, ongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa muda wa miaka 16. Sasa anapumzika katika usingizi wa amani  Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linasema kwamba, limepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Askofu mkuu Noël Treanor, na kwamba, wanaungana na waamini pamoja na watu wote walioguswa na msiba huu, ili kumwombea. Ni kiongozi aliyesimamia utu, heshima na haki msingi za binadamu; umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Alipenda kuhakikisha kwamba, amana na urithi wa Kikristo vinastawi na kushamiri Barani Ulaya. Kwa hakika ni Kiongozi aliyebarikiwa kuwa na kipaji cha akili, mang’amuzi na uongozi makini.

Fumbo la Kifo

 

13 August 2024, 14:48