Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anatarajia kufanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anatarajia kufanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore.  (Vatican Media)

Hija ya 45 ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia 2-13 Septemba 2024

Papa Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Hii ni fursa kwa watu wa Mungu katika nchi hizi kuweza kuonana mubashara na Papa kwani wengi wao wanamwona kwenye luninga na mitandao ya kijamii. Hii ni fursa kwa watu wa Mungu Barani Asia kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija za Kitume za Baba Mtakatifu nje ya Vatican zinapania kuwatia shime, ari na mwamko wa kimisionari, watu watakatifu wa Mungu ili wawe tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma aweze kuwagusa na kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao, kama ilivyokuwa kwa yule mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. Hii ni changamoto ya kusikiliza kwa makini na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji. Rej. Yn 9:1-25. Ni hija zinazopania kuwaimarisha watu wa Mungu katika imani, matumaini na mapendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anatarajia kufanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Hii itakuwa ni fursa kwa watu wa Mungu katika nchi hizi kuweza kuonana mubashara na Baba Mtakatifu Francisko, kwani wengi wao wanamwona kwenye luninga na mitandao ya kijamii.

Papa Indonesia: 3 Septemba hadi tarehe 5 Septemba
Papa Indonesia: 3 Septemba hadi tarehe 5 Septemba

Hii ni fursa kwa watu wa Mungu Barani Asia kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hii pia ni nafasi kwa Baba Mtakatifu Francisko kujionea mwenyewe ari na mwamko wa kimisionari katika nchi hizi ambazo zina idadi ndogo ya Wakristo, ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine, kumbe, hii ni nafasi ya kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini sanjari na mchato wa majadiliano ya kiekumene. Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Yangon lililoko nchini Myanmar, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican anasema, Bara la Asia lina amana na utajiri mkubwa wa: tamaduni, dini na mapokeo na kwamba, Wakristo ni wachache sana katika nchini nyingi Barani Asia, isipokuwa katika Nchi za Ufilippini na Timor ya Mashariki. Kuna tofauti kubwa kati ya Wakristo wanaoishi Barani Asia, lakini haya ni maeneo ambayo yamesimikwa katika misingi ya amani na utulivu, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Asia. Haki na amani ni kati ya vipaumbele vya Kanisa Barani Asia, ili kuweza kusimama kidete kupambana na umaskini wa hali na kipato; athari za mabadiliano ya tabianchi; nyanyaso na mifumo mbalimbali ya ubaguzi.

Papa Francisko Papua New Guinea 7-9 Septemba 2024
Papa Francisko Papua New Guinea 7-9 Septemba 2024

Kardinali Charles Maung Bo anakaza kusema, amana na urithi wa imani kutoka Barani Asia unaendelea kutangazwa na kushuhudiwa mahali popote pale walipo. Imani Barani Asia bado iko hai na imara na kwamba, Makanisa yanaendelea kufurika waamini kila Dominika wanapokufanyika kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, chakula cha wasafiri. Kiu kubwa ya watu wa Mungu Barani Asia ni haki, amani na maridhiano. Kumbe, Hija hii ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni fursa ya kupyaisha na kuimarisha zawadi ya: imani, matumaini na mapendo. Huu ni mwaliko kwa wateule watakatifu wa Mungu Barani Asia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kanisa hai la Kristo Yesu. Huu ni muda muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili kufungua na kuandika ukurasa mpya wa utume wa Kanisa; kwa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na kuendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho.

Papa Francisko: Timor ya Mashariki tarehe 7 Septemba 9 Septemba
Papa Francisko: Timor ya Mashariki tarehe 7 Septemba 9 Septemba

Lengo kuu ni kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili. Mchakato wa Uinjilishaji mpya unahitaji majiundo makini na endelevu yatakayowasaidia waamini kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kwani: ushuhuda, maisha na utume wa Kanisa ni mambo msingi katika kufufua imani ndani na nje ya Bara la Asia. Waamini wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha imani katika uhalisia wa maisha yao sanjari na utamadunisho, vinginevyo, wanaweza kujikuta kwamba, imani inaelea katika ombwe pasi na kukita mizizi katika maisha, tamaduni na mila njema za watu husika. Uinjilishaji mpya unaotekelezwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo unajikita katika mchakato wa: Majadiliano ya kiekumene na kidini ili kujenga na kudumisha: utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao. Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu Injili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao. Uekumene wa damu unajikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Singapore 11 Septembahadi 13 Septemba 2024
Singapore 11 Septembahadi 13 Septemba 2024

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Baba Mtakatifu anapembua kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira, umuhimu wa wongofu wa kiekolojia na teknolojia rafiki kwa mazingira. Anazungumzia kuhusu haki ya maji safi na salama. Mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, urithi unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Utunzaji wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na uwajibikaji na wala maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasitumike kama nguvu ya kiuchumi kwa ajili ya kunyonya Mataifa mengine wala kuyatumbukiza katika utamaduni wa kifo. Watu wateule wa Mungu Barani Asia wanapaswa kuwa wadau wakuu katika mchakato wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.

Hija ya Kitume Barani Asia

 

20 August 2024, 13:26