Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB katika "Hija yake ya Kitume, Ad Limina Visit" Ijumaa tarehe 30 Agosti 2024 limekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB katika "Hija yake ya Kitume, Ad Limina Visit" Ijumaa tarehe 30 Agosti 2024 limekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya Mjini Vatican: 2024

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, hija yao ya Kitume mjini Vatican imekuwa ni ya manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.” Wamejadiliana kuhusu maisha ya Sakramenti za Kanisa na changamoto zake nchini Kenya hasa kuhusu maisha ya ndoa na familia pamoja na ongezeko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa; umuhimu wa uinjilishaji na urithishaji wa imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Papa Sixtus wa V kunako mwaka 1585 alianzisha hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu Jimbo mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano, yaani “Ad Limina Apostolorum Visitatio” na kwa kifupi, “Ad Limina.” Kwa busara yake ya kichungaji akaamuru Maaskofu wote Katoliki kutembelea mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni nafasi ya kutembelea na kusali kwenye Kaburi la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na kutoa taarifa ya Maandishi kwa Baraza la Kipapa la Maaskofu kuhusu mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa katika Jimbo husika. Ni fursa pia ya kujadiliana na wakuu wa Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Hija ya Kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, 2024
Hija ya Kitume ya Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, 2024

Huu ni wakati muafaka kwa Mabaraza ya Kipapa kusikiliza kwa makini kile kinachoendelea kwenye Makanisa mahalia. Ni katika hali na mazingira kama haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, “The Kenya Conference of Catholic Bishops, KCCB” linasema, hija yao ya Kitume mjini Vatican imekuwa ni ya manufaa sana kwa ajili ya kukoleza kazi ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake sanjari na huduma kwa roho za waamini “Curam animarum.” Wamejadiliana kuhusu maisha ya Sakramenti za Kanisa na changamoto zake nchini Kenya hasa kuhusu maisha ya ndoa na familia pamoja na ongezeko la miito mitakatifu ndani ya Kanisa; umuhimu wa uinjilishaji na urithishaji wa imani unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; huduma ya kiroho na kimwili kwa wakimbizi na wahamiaji; malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya.

Papa Francisko akizungumza na Maaskofu katoliki kutoka Kenya, 30.08.2024
Papa Francisko akizungumza na Maaskofu katoliki kutoka Kenya, 30.08.2024

Kwa hakika anasema, Askofu mkuu Maurice Muhatia Makumba, wa Jimbo kuu la Kisumu ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, KCCB, kipaumbele kwa sasa ni malezi, majiundo na makuzi makini ya vijana wa kizazi kipya ili waweze kukumbatia na kuambata: Ukweli na Haki; tunu msingi za maisha ya kiroho na kijamii zinazosimikwa katika hofu ya Mungu, haki msingi za binadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Maaskofu Katoliki Kenya
30 August 2024, 13:59