Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anatarajia kufanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anatarajia kufanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia na Oceania 2-13 Sept.2024

Papa Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija za Kitume za Baba Mtakatifu nje ya Vatican zinapania pamoja na mambo mengine: kuwatia shime, ari na mwamko wa kimisionari, watu watakatifu wa Mungu ili wawe tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma aweze kuwagusa na kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao, kama ilivyokuwa kwa yule mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. Hii ni changamoto ya kusikiliza kwa makini na kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, Kiutu na Kitamaduni katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji na kama sehemu mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete anasema Baba Mtakatifu Francisko.  Rej. Yn 9:1-25. Ni hija zinazopania kuwaimarisha watu wa Mungu katika imani, matumaini na mapendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi 13 Septemba 2024 anafanya Hija ya 45 ya Kitume Barani Asia na Oceania kwa kutembelea Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na hatimaye, Singapore. Katika hija hii, Baba Mtakatifu Francisko ni shuhuda wa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia mahususi katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu; haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kimsingi ni hujaji wa matumaini, faraja na ujirani mwema. Hii ni kati ya hija ndefu kuwahi kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Safari hii ni utekelezaji wa ndoto ya mwaka 2020 kabla ya kuibuka na hatimaye, kusambaa kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Papa Francisko alipowasili mjini Jakarta, Indonesia
Papa Francisko alipowasili mjini Jakarta, Indonesia

Huu ni mwendelezo wa hija zilizofanywa na watangulizi wake: Mtakatifu Paulo VI pamoja na Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye miaka 1970 na Miaka 1980. Kuna mabadiliko makubwa ambayo yamekwisha kufanyika tangu nyakati hizo: kukua na kukomaa kwa demokrasia; ustawi na maendeleo ya watu baada ya vita na uvamizi. Baba Mtakatifu anakwenda Barani Asia kama mjumbe wa amani, hasa nchini Indonesia ambayo kwa miaka ya hivi karibuni imekumbwa na mashambulizi pamoja na vitendo vya kigaidi, vita na machafuko. Huu ni wakati muafaka kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanasitisha vita, kinzani na mipasuko sehemu mbalimbali za dunia, kwa kujikita katika majadiliano, urafiki wa kijamii, mshikamano na maridhiano. Tofauti msingi kati ya watu hazina budi kuheshimiwa na kuthaminiwa, ili kujenga na kudumisha mafungamano na mahusiano ya kijamii, udugu wa kibinadamu; haki na mshikamano kwa ajili ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Baba Mtakatifu akiwa mjini Jakarta atapata nafasi ya kutembelea msikiti wa “Istiglal” na pamoja na Imam mkuu wataweka saini kwenye Tamko la Pamoja. Huko Papua New Guinea, bado kuna mapambano ya kikabila.

Baraza la Maaskofu kutoka Timor ya Mashariki
Baraza la Maaskofu kutoka Timor ya Mashariki

Timor ya Mashariki “Timor-Leste” bado inaendelea na vita ya kudai uhuru wao kutoka kwa Wareno; vita ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu nchini humo. Singapore ni nchi inayoonesha tofauti kubwa ya usawa wa kijamii. Baba Mtakatifu Francisko atazungumzia pia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu anatarajia kutoa hotuba 16 katika lugha ya Kihispania na Kiitalia. Tema kuu ni pamoja na: Injili ya ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu amejiandaa kikamilifu kutekeleza hija hii ya kitume, akisaidiwa na kikundi cha madaktari na wauguzi wake. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu ni kati ya viongozi wakuu kutoka Vatican wanaoshiriki katika hija hii ya Kitume Barani Asia na Oceania. Pamoja naye, wamo pia Makardinali, Maaskofu wakuu na Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali zitakazotembelewa na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 13 Septemba 2024.

Hija ya Kitume
31 August 2024, 14:47