Kumbukumbu ya Kifodini cha Yohane Mbatizaji: Shuhuda wa Mwanga wa Mataifa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifodini ni huduma, utume na zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waaminifu wa Mungu. Yohane Mbatizaji alimtambulisha Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Rej. Yn 1:29-36. Akafunga utambulisho huu kwa kufungwa gerezani na hatimaye, kukatwa kichwa. Mk 6:17-29. Katika giza na uvuli wa mauti, akamtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Mwanga wa Mataifa. Rej. Yn 1:7. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Agosti, anaadhimisha Kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji kukatwa kichwa na Mfalme Herode. Akawa ni mtangulizi wa kuzaliwa na hata kufa kwa Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu. Alikuwa ni shuhuda amini na angavu wa Neno la Mungu, kiasi hata cha kukatwa kichwa kwa ajili ya kutetea haki na ukweli. Mtakatifu Yohane Mbatizaji alikuwa ni shule ya kwanza ya Mitume wa Kristo Yesu. (Rej. Yoh. 1:35-40). Kumbukumbu hii ilianza kuadhimishwa tangu karne ya tano, kila mwaka tarehe 29 Agosti. Mfalme Herode alidhani kwamba, Yohane Mbatizaji alikuwa ni Nabii, alimwogopa, kwani alijua kuwa ni mtu wa haki, Mtakatifu wa Mungu, akamlinda na kumsikiliza kwa furaha. “Alimsweka ndani” kwa vile Yohane Mbatizaji alimshutumu kwa uzinzi, lakini hakutumia fursa hii kutubu na kumwongokea Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, tayari alikuwa amelewa madaraka na kutopea katika uzinzi. Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu umuhimu na utume wa Mtakatifu Yohane Mbatizaji anasema, tangu tumboni mwa Mama yake Elizabeth, Yohane Mbatizaji alikuwa ni mtangulizi wa Yesu, aliyeonesha kwamba, hakuna jambo lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha uhusiano wa kina kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja la Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Wengi walimfananisha Yohane Mbatizaji na Nabii Elia aliyewatakasa Waisraeli kutoka katika ibada ya kuabudu miungu na kuwarejesha tena katika imani ya kweli iliyojikita kwa Mwenyezi Mungu aliye hai, yaani Mungu wa Abramu, Isaka na Yakobo. Yohane Mbatizaji alihubiri juu ya uwepo wa Masiha ambaye atajifunua kwao. Yohane Mbatizaji aliwataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa. Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu anamshukia Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Yesu Kristo ni Masiha wa Bwana. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, tukio hili lilimshangaza sana Yohane Mbatizaji, kumwona Yesu akiwa kati kati ya kundi kubwa la wadhambi kama wao, lakini kwa ajili yao, ili aweze kubatizwa na kutekeleza haki yote sanjari na mpango wa wokovu wa Mungu. Yesu Kristo anajionesha kama Mwana kondoo wa Mungu anayeichukua na kuondoa dhambi ya ulimwengu. Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha kuwa Kristo Yesu kuwa ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu! Hawa ndio akina Simone aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, tafakari ya Neno la Mungu imekita mizizi yake katika tukio hili lisilo la kawaida kwani ni kiini cha imani na utume wa Kanisa linalohamasishwa nyakati zote kumtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Mwana Kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu! Ni Bwana na Mkombozi pekee wa ulimwengu aliyejivika taji la fadhila ya unyenyekevu akathubutu hata kusimama kati kati ya wadhambi, ili kuwakomboa na kuwapeleka kwenye uhuru kamili wa watoto wa Mungu. Kuna watu waliopelekea kukatisha maisha ya Yohane Mbatizaji: Mtu wa kwanza ni Mfalme Herode, fisadi na mtu asiye na msimamo katika maisha. Pili, ni Herodia aliyekuwa anamchukia Yohane Mbatizaji kwa sababu alimwambia ukweli! Tatu ni Salome, binti Herodia aliyecheza mbele ya Mfalme, kiasi cha kumfanya achanganyikiwe na kutoa ahadi ambazo baadaye zimemtesa sana kwa mauaji ya mtu wa Mungu. Nne, ni Yohane Mbatizaji, Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeiondoa dhambi za ulimwengu. Yohane Mbatizaji, kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, anaishia kukatwa kichwa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Yohane Mbatizaji, akauwawa kikatili, peke yake mle gerezani kama ilivyo kwa wafidia dini na waungama imani wengi! Huu ni ushuhuda wa hali ya juu wa utakatifu unaofumbatwa katika maisha ya waamini. Ni maisha yanayomiminwa na sadaka inayotolewa, mwaliko na changamoto kwa waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu wahusika wanaozungumziwa kwenye Injili mintarafu kifo chake, kama changamoto ya kumshuhudia Kristo si tu kwa maneno, bali kwa njia ya maisha yao adili na matakatifu, kama alivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji! Baba Mtakatifu Benedikto XVI aliwahi kusema kwamba jina la Yohane Mbatizaji maana yake ni kwamba, "Mungu ni mwenye huruma."