Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025: Mwaka Sala: Shule ya Sala
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 itakuwa ni fursa ya kupyaisha tena matumaini kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Katika Tamko hili, Baba Mtakatifu anakazia kuhusu Matumaini katika Neno la Mungu ili kuamini, kutumaini, kupenda na kuvumilia kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni mahujaji wa matumaini. Alama za matumaini zinazomwilishwa katika amani, kwa kujikita katika Injili ya uhai, maboresho ya magereza; huduma kwa wagonjwa, vijana, wahamiaji na wakimbizi, wazee na maskini. Wito wa matumaini kwa kujikita katika matumizi bora ya rasilimali za dunia; msamaha wa madeni ya nje kwa nchi zinazoendelea duniani.
Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanabeba ujumbe mzito wa matumaini kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo; hii ni fursa kwa watu wateule wa Mungu kujikita katika ujenzi wa tunu msingi za kibinadamu zinazosimikwa katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Lengo kuu ni kujizatiti kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ujenzi wa uchumi shirikishi sanjari na ujenzi wa urafiki wa kijamii na udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu Francisko ametangaza kwamba, Mwaka 2024 uwe ni mwaka wa Sala kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo. Mwaka huu unapania pamoja na mambo mengine: Kugundua na kupyaisha umuhimu wa maisha ya sala katika maisha ya mtu binafsi, ndani ya Kanisa na katika Ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kupyaisha matumaini baada ya watu wengi kukata na kujikatia tamaa ya maisha kutokana na hali ngumu ya maisha, vita na mipasuko ya kijamii bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mkakati wa shughuli za kichungaji unaopania kuwarejeshea tena watu wa Mungu matumaini. Huu ni mwaliko kwa kila jimbo, baada ya kusoma alama za nyakati kwa watu wake, kuandaa katekesi kuanzia wakati huu, hadi wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya mwaka 2025 hapo tarehe 24 Desemba 2024 wakati wa kufungua Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Katekesi hii ilenge kuwasaidia waamini kujiandaa kikamilifu kuingia katika Lango la Jubilei. Ni katika maadhimisho ya Mwaka wa Sala, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kuzungumza na watoto zaidi ya 200 kutoka katika Parokia ya “Santa Bernadette Soubirous” Jimbo kuu la Roma. Huu ulikuwa ni muda wa katekesi kuhusu maisha ya sala, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Katika katekesi yake amekazia umuhimu wa sala katika maisha, daima vijana wasichoke kumuulizia Mwenyezi Mungu wito wao katika maisha, tayari kujibu kwa moyo wa ukarimu na shukrani, kwani Mwenyezi Mungu ana mpango kwa kila mtu. Wawe makini, wala wasiwahukumu, wale wasioamini, lakini wajitahidi kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, Baba mwenye huruma na mapendo. Waamini watambue kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanayopaswa kuimwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Katika shida na mahangaiko mbalimbali ya maisha, watafute washauri wema na waaminifu kwani si rahisi sana kwa mtu binafsi kuvuka nyakati za shida na giza nene katika maisha. Kuna hatari kubwa kwa siku za mbeleni kutokana na kiwango cha chini kabisa cha watoto wanaozaliwa nchini Italia. Licha ya shida, magumu na changamoto za maisha ni vyema ikiwa kama vijana watawekeza katika maisha ya ndoa na familia, kwa sababu watoto ni tumaini la taifa la leo na kesho iliyo bora zaidi. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Hivi karibuni kuna Wakristo waliuwawa kikatili nchini DRC kwa kukataa kuikana imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hii ni changamoto kwa Wakristo kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kikristo! Baba Mtakatifu anawataka vijana kuthubutu katika maisha!