Papa Francisko: Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, katika maisha na utume wake, yanapaswa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika, kwa kuongozwa na kipaji cha ubunifu pamoja na ukakamavu. Papa Francisko: Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, katika maisha na utume wake, yanapaswa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika, kwa kuongozwa na kipaji cha ubunifu pamoja na ukakamavu.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa Zingatieni: Ushirika, Ubunifu na Ukakamavu Katika Uinjilishaji

PMS, katika maisha na utume wake, yanapaswa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika, kwa kuongozwa na kipaji cha ubunifu pamoja na ukakamavu, daima yakichota amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika upendo unaotolewa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuendelea kujipyaisha katika maisha na utume wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, katika maisha na utume wake, yanapaswa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika, kwa kuongozwa na kipaji cha ubunifu pamoja na ukakamavu, daima yakichota amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika upendo unaotolewa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuendelea kujipyaisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa na Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na agizo la Mungu Baba Mwenyezi. Ad gentes, 2. Utume huu wa Kanisa unafumbatwa katika kutangaza na kushuhudia kweli za kiinjili zinazofumbatwa katika upendo wa Mungu kwa waja wake; na hivyo kushuhudiwa katika maisha na utume wa Kanisa. Si dhamana wala wajibu wa Kanisa kufanya wongofu wa shuruti, bali watu watakatifu wa Mungu wavutwe na ushuhuda wa upendo, wenye mvuto na mashiko.

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa: Upyaisho ni muhimu
Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa: Upyaisho ni muhimu

Hii ni sehemu ya hotuba aliyoitoa Baba Mtakatifu Francisko kwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, ulioadhimishwa tarehe 25 Mei 2024. Huu ni mwaliko wa kukuza na kudumisha tasaufi ya ushirika wa kimisionari, msingi wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, katika ulimwengu mamboleo. Mtazamo huu mpya unapaswa kujikita katika wongofu wa kimisionari unaofumbatwa katika majiundo ya mtu binafsi na yale ya kijumuiya, ili kukuza na kudumisha ushirika wa kimisionari, utakaowawezesha watu wateule wa Mungu kuishi katika ushirika wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya waja wake na hivyo kuingia na hatimaye, kutengeneza historia ya maisha ya binadamu. Ushirika wa kimisionari unafumbatwa katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, unaowataka wabatizwa wote kutembea kwa pamoja kama ndugu wamoja; kujenga na kudumisha utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana; hata kama kuna kupishana kwa mawazo na vipaumbele, lakini yote haya anasema Baba Mtakatifu Francisko yafanyike ndani ya Jumuiya. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS yanayo dhamana ya kuendeleza maisha na utume wa Makanisa mahalia katika ujumla wake.

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa: Ubunifu ni jambo la msingi
Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa: Ubunifu ni jambo la msingi

Kipaji cha ubunifu kinachokita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kinapania pamoja na mambo mengine yote, kuyafanya yote mapya! Rej Ufu 21:5. Kipaji hiki cha ubunifu anasema Baba Mtakatifu kina uhusiano wa karibu na uhuru ambao unapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kama inavyojidhihirisha katika Kitabu cha Matendo ya Mitume, kielelezo cha utume wa Roho Mtakatifu. Huu ndio uhuru wa ubunifu wa kimisionari ambao haupaswi kupokwa kwani ni upendo peke yake unaoweza kuunda upya. Kumbe, kipaji cha ubunifu wa kimisionari kinapata chimbuko lake katika upendo wa Kimungu, mwanzo na hatima ya shughuli zote za kimisionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Ubunifu huu si tu kwa ajili ya kupanga sera na mikakati ya kukusanya fedha ya mshikamano na nchi za kimisionari, ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu sanjari na ukuaji wa Kanisa mahalia. Kumbe, kila mwamini anao wajibu wa kuhakikisha kwamba, anachangia kwa hali na mali katika mchakato wa ustawi, maendeleo na ukuaji wa Kanisa la Kristo. Ushirika huu, unawahusu waamini binafsi, vyama na mashirika ya kitume, kama kielelezo cha moyo wa shukrani kwa mema mengi ambayo Kristo Yesu anawakirimia waja wake, kila kukicha.

Huduma kwa Mashirika ya Utoto Mtakatifu ni muhimu sana
Huduma kwa Mashirika ya Utoto Mtakatifu ni muhimu sana

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Ukakamavu ni sehemu ya mchakato wa kudumu katika kutenda kazi mintarafu upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwaliko kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanajibidiisha kujenga ushirika wa watu wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa ataendelea kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo hadi miisho ya dunia, licha ya matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazoendelea kujtokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu alitumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza baadhi ya waamini kutoka Kivu Kaskazini, nchini DRC waliouwawa kikatili kwa sababu tu walikataa kuongokea dini nyingine na kuamua kubaki kuwa Wakristo. Tukio hili ni kama lile lilitokea nchini Libya, takribani miaka mitano iliyopita, Wakristo wa Kanisa la Kikoptiki walipouwawa kikatili. Kumbe, Kanisa kakamavu, litazidi kusonga mbele katika maisha na utume wake, kama ushuhuda wa kifodini. Huu ni ushuhuda unatolewa na Kanisa sehemu mbalimbali za dunia. Katika shida, magumu na changamoto za maisha na utume wa Kanisa; waendelee kuwa wavumilivu, daima wakijitahidi kutenda wema. Uvumilivu uwawezeshe kuendelea na maisha na utume wao hata katikati ya magumu na changamoto za maisha. Wawe tayari kuinama na kuwainua wale wote walioteleza na kuanguka. Mwishoni, Baba Mtakatifu aliwapongeza na kuwashukuru Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, kwa sadaka na majitoleo yao; kwa kuwajibika kimisionari hasa kwa huduma ya Utoto Mtakatifu!

Mashirika ya Kimisionari
19 August 2024, 11:45