Maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Sala ya Rozari Takatifu kwa ajili ya kuwaombea Wakristo wanaonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia Maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Sala ya Rozari Takatifu kwa ajili ya kuwaombea Wakristo wanaonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Miaka 10 ya Rozari Takatifu Kwa Wakristo Wanaodhulumiwa Duniani

Tarehe 20 Agosti 2024 ni maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanza kwa ishara ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kuponya madonda kwa maombezi ya Bikira Maria, ili watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati waweze kuishi kwa haki, amani, upendo na udugu wa kibinadamu dhidi ya ukabila, udini, vurugu na vita; mambo ambayo kwa nyakati hizi, yamekuwa ni chanzo cha majanga huko Mashariki ya Kati. Rozari Takatifu inapania kuponya madhara haya katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Damu ya Wakristo wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika sehemu mbalimbali za dunia mambo yanayoendekezwa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani. Watu wanauwawa kinyama, Makanisa yanalipuliwa; maeneo ya kumbukumbu na hifadhi ya mambo kale yanaharibiwa na watu wanauwawa kwa misingi ya imani na kidini. Hapa, inaonekana kana kwamba, Wakristo ndio walengwa wakuu wa mauaji, nyanyaso na dhuluma mbalimbali, ingawa hata waamini wa makundi madogo madogo ya kidini nao pia wanadhulumiwa kama inavyojionesha huko Iraq.  Uchunguzi wa kina uliofanywa na kuchapishwa na “Pew Research Center kwa mwaka 2014 unaonesha kwamba, Wakristo wanaongoza kwa kuuwawa, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao, sehemu mbalimbali za dunia. Ni katika muktadha huu, Rimini pamekuwa ni mahali ambapo watu wa Mungu kwa takribani miaka kumi wamekuwa wakisali ili kusimamisha vita huko Mashariki ya Kati. Ilikuwa majira ya joto kunako mwaka 2014, wiki chache baada ya kutangazwa kwa Ukhalifa, Kikundi cha Dola ya Kiislamu ISIS kilichukua udhibiti wa eneo kubwa kati ya Siria na Iraq na usiku kati ya tarehe 6 na 7 Agosti Wakristo elfu mia moja na ishirini na tano walilazimika kuiacha ardhi na makazi yao, ili kutafuta hifadhi na usalama wa maisha yao na wengine wengi wakabaki kama wakimbizi katika eneo la Erbil na Duhok.

Rozari kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia
Rozari kwa ajili ya kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia

Hiki kilikuwa ni kipindi cha: mateso, dhuluma na unyanyasaji wa kimwili na kiuchumi dhidi ya Wakristo. Hapo ndipo jioni ya tarehe 20 Agosti 2014 huko Rimini, kwenye uwanja wa kati wa mji huo, Wakristo walipokusanyika kusali Rozari kwa ajili ya kuwaombea Wakristo waliokuwa wanateswa na kunyanyaswa huko Mashariki ya Kati na sehemu nyingine za dunia. Kuanzia usiku huo, kila tarehe 20 ya mwezi, mpango huo uliendelea sio tu katika mji wa Rimini, lakini hatua kwa hatua uliongezeka hadi miji kumi na tatu ya Italia na baadhi ya nje ya nchi, kwa kuhusisha nyumba za kitawa zipatazo ishirini na saba kutoka ndani na nje ya Italia. Tarehe 20 Agosti 2024 ni maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanza kwa ishara ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kuponya madonda kwa maombezi ya Bikira Maria, ili watu wa Mungu huko Mashariki ya Kati waweze kuishi kwa haki, amani, upendo na udugu wa kibinadamu dhidi ya ukabila, udini, vurugu na vita; mambo ambayo kwa nyakati hizi, yamekuwa ni chanzo cha majanga huko Mashariki ya Kati. Sala hii ya Rozari Takatifu inapania kuponya madhara haya katika maisha ya binadamu katika ulimwengu mamboleo.

Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea uponyaji na ujenzi wa udugu
Rozari Takatifu kwa ajili ya kuombea uponyaji na ujenzi wa udugu

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Bwana Marco Ferrini, Mratibu wa Kamati ya Nazarat kwa ajili ya Wakristo wanaodhulumiwa na kunyanyaswa anasema, anapenda kushirikisha furaha yake katika kumbukizi ya miaka kumi, tangu kuanzishwa kwa Sala ya Rozari Takatifu sehemu mbalimbali za dunia, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia. Huu ni ushuhuda wa upendo, ujirani mwema na ushirika na wale wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki, chuki na uhasama. Walimwengu wanayo kiu ya kusikia Habari Njema ya Wokovu, ikitangaza amani na kwamba, Wakristo wanaitwa na kutumwa kutangaza na kuwashirikisha wengine zawadi ya amani. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwahamasisha wale wote wanaoshiriki tukio hili wakiwa wamesheheni karama za Roho Mtakatifu, wajitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa utamaduni unaoheshimu watu wote; utamaduni unaofumbatwa katika ukarimu na udugu wa kibinadamu ambao ni shirikishi, ili watu wote waweze kushiriki katika ushirika na furaha ya mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawaalika washiriki kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Msaada, ili aweze kuwapokea na kuwahifadhi; kuwalinda na kuwatunza wakati wa majaribu. Bikira Maria awashe mwanga wa matumaini, ili amani na utulivu viweze kupatikana. Mwishoni, Baba Mtakatifu ametoa baraka zake za Kitume kwa wale wote watakaoshiriki katika kumbukizi hii ya miaka kumi tangu watu wa Mungu walipoamua kusali Rozari kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo wanaonyanyaswa na kudhulumiwa sehemu mbalimbali za dunia.

Rozari ya amani

 

16 August 2024, 15:41