Tafuta

Vatican inasema ilihuzunishwa na kusikitishwa sana na baadhi ya matukio ya Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024. Vatican inasema ilihuzunishwa na kusikitishwa sana na baadhi ya matukio ya Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024.   (AFP or licensors)

Ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris Kwa Mwaka 2024: Tamko la Vatican

Vatican inapenda kuunganisha sauti yake na sauti ambazo zimepazwa katika siku za hivi karibuni kwa kukemea kosa la kukejeli Wakristo na waamini wa dini nyingine. Hili lilikuwa ni tukio la kifahari ambapo ulimwengu wote ulikusanyika kutazama na kwamba, kwa kawaida tunu msingi za maadili hazipaswi kuwa na madokezo ambayo yanakejeli imani za kidini za watu wengine. Uhuru wa kujieleza, ambao hautiliwi shaka, unapata kikomo chake katika heshima kwa wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Vatican inasema ilihuzunishwa na kusikitishwa sana na baadhi ya matukio ya Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024. Vatican inapenda kuunganisha sauti yake na sauti ambazo zimepazwa katika siku za hivi karibuni kwa kukemea kosa la kukejeli Wakristo wengi na waamini wa dini nyingine. Hili lilikuwa ni tukio la kifahari ambapo ulimwengu wote ulikusanyika kutazama na kwamba, kwa kawaida tunu msingi za maadili hazipaswi kuwa na madokezo ambayo yanakejeli imani za kidini za watu wengine. Uhuru wa kujieleza, ambao hautiliwi shaka, unapata kikomo chake katika heshima kwa wengine. Hivi ndivyo Vatican inavyohitisha tamko lake kuhusu matukio ya kusikitisha yaliyojitokeza wakati wa Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024.

Ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 lilikuwa ni tukio la kifahari
Ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 lilikuwa ni tukio la kifahari

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa “Conférence des Evêques de France, CEF., limesema kwamba, Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024 ilikuwa ni kata na shoka, kwa kuwashirikisha wasanii maarufu kutoka ndani na nje ya Ufaransa. Gwaride la wanamichezo lilifana sana, kwa hakika ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ulifana sana, kwani ilikuwa ni siku ya kufurahi na kwamba, hii ni siku iliyobeba hisia nyingi zinazopaswa kusifiwa. Lakini kwa bahati mbaya ufunguzi huu ulichafuliwa na picha za dhihaka na kejeli dhidi ya imani ya Kikristo; jambo ambalo limechukiza kabisa na hivyo kuharibu sherehe za ufunguzi huo. Kumekuwepo na shutuma nyingi dhidi ya wasanii hao mintarafu “Karamu ya Mwisho” kama ilivyochorwa na msanii maarufu sana Leonardo da Vinci  Tukio hili lililotangazwa moja kwa moja kwenye Vituo mbalimbali vya Televisheni lilikuwa na viashiria vya ushoga. Tukio hili limewaibua viongozi mbalimbali wa dini na watu wenye mapenzi mema kuonesha mshikamano na Kanisa Katoliki nchini Ufaransa! Wakristo wengi wamesononeshwa na tukio hili na kwamba, Serikali ya Ufaransa ilipaswa kutambua kwamba, Sherehe za ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki inaenea mbali zaidi ya upendeleo wa kiitikadi kwa wasanii wachache, wanasema Maaskofu Katoliki Ufaransa.

Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote.
Uhuru wa kidini ni msingi wa uhuru mwingine wote.

Ingawa kuna watu wengi duniani wanaoendelea kuteseka kutokana na majanga pamoja na baa la njaa duniani, bado kuna wafanyabiashara wanaoendelea kutengeneza na kuuza silaha, hali inayopelekea kuchoma rasilimali fedha na hivyo kuendelea kuchochea vita kubwa na ndogo sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni kashfa ambayo Jumuiya ya Kimataifa haipaswi kuvumilia, kwani inapingana na mchakato wa ujenzi wa roho ya udugu wa kibinadamu katika Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa mwaka 2024 ambayo imefunguliwa rasmi tarehe 26 Julai 2024 na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 11 Agosti 2024. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 28 Julai 2024 wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anasema, vita ni dalili za binadamu kushindwa. Hiki ni kipindi ambacho vita sehemu mbalimbali za dunia bado inaendelea kurindima, kuna misigano na mipasuko ya kijamii katika ngazi ya Kimataifa inayoendelea.

Vatican imehuzunishwa na baadhi ya matukio ya ufunguzi wa michezo Paris
Vatican imehuzunishwa na baadhi ya matukio ya ufunguzi wa michezo Paris

Kumbe, kipindi cha Mashindano ya Olimpiki iwe ni fursa ya kusitisha vita, mapigano na kinzani hizi na muda huu uwe ni kwa ajili ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kutumia lugha ya michezo inayoeleweka na wote. Huu ni muda muafaka kwa wanamichezo Jijini Paris kujikita katika kukuza na kumwilisha tunu msingi za michezo kama vile: shauku, ujumuishaji, udugu wa kibinadamu, moyo wa timu, uaminifu, ukombozi, sadaka na majitoleo. Katika kipindi cha mazoezi, wanamichezo wanaweza kushinda changamoto na ugumu wanaokabiliana nao, huu ndio ujasiri unaoletwa katika Michezo ya Olimpiki ya Paris kwa Mwaka 2024. Michezo hii ni marathoni ya maisha inayowashirikisha wanamichezo wengi kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, kiini cha Michezo hii ni amani inayopaswa kumwilishwa wakati wote wa mashindano haya, ili kupandikiza mbegu ya matumaini kwa watu walioathirika kwa vita, watu wanaosiginwa utu, heshima na haki zao msingi kwa umaskini, ukosefu wa haki, kinzani na woga, tayari kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu kwa kusitisha vita.

Baadhi ya matukio ya ufunguzi wa michezo yameonesha fedheha
Baadhi ya matukio ya ufunguzi wa michezo yameonesha fedheha

Ni katika muktadha wa kusitisha vita na kuanza kujikita katika ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, anaungana na Baba Mtakatifu Francisko kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha vita wakati huu wa Michezo ya Olimpiki Paris, kwa mwaka 2024. Kimsingi ari na moyo wa Michezo ya Olimpiki ni amani, kwa kumfuata Kristo Yesu, chemchemi ya amani ya kudumu. Michezo hii iwe ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kusitisha vita, kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za dunia, lakini zaidi huko nchini Ukraine na Ukanda wa Gaza. Vita imekuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya watu wengi duniani. Wakristo wawe mstari wa mbele kujenga na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, hii ni changamoto ya maisha ya Wakristo!

Tamko Vatican
04 August 2024, 14:42