Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko mintarafu Shirika la Oblati wa Mtakatifu Yosefu katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Kujificha, Ubaba na Upendeleo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Baba Mtakatifu Francisko mintarafu Shirika la Oblati wa Mtakatifu Yosefu katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Kujificha, Ubaba na Upendeleo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mkutano Mkuu wa 28 wa Oblati wa Mtakatifu Yosefu: Kujificha, Ubaba na Maskini

Baba Mtakatifu Francisko mintarafu maisha yao ya kitawa na huduma yao kwa Kanisa, katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Kujificha, Ubaba na Upendeleo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mtakatifu Giuseppe Marello (1844-1895), anakazia umuhimu wa kuzamisha mizizi katika imani na maisha ya kitawa, tayari kuishi pamoja na Kristo Yesu. Wanashirika wanahimizwa kujenga mahusiano na Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mikutano mikuu ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume inayoadhimishwa wakati huu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni muhimu sana katika maisha na utume wa kila Shirika ili kulinda, kutunza na kuendeleza karama za waanzilishi wa Mashirika haya. Huu ni muda muafaka wa kujenga utamaduni wa kusikilizana; kuchunguza na kusoma ishara za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili, ili kubaini masuala yenye uzito zaidi katika ulimwengu mamboleo. Rej, Gaudium et spes, 4. Ni wakati wa kufanya tafakari ya kina kuhusu: mang’amuzi, majiundo na Injili ya upendo. Huu ni muda uliokubalika kwa kila mwanashirika kujikita katika mchakato wa upyaisho wa maisha yake binafsi na ule wa kijumuiya, tayari kuzama katika maendeleo ya Shirika kwa sasa na kwa siku usoni. Tangu mwanzo wa Kanisa wamekuwepo watu kwa kutekeleza mashauri ya Injili walinuia kumfuasa Kristo Yesu kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu ambao unapata chimbuko lake katika Sakramenti ya Ubatizo, na unaojitoa na kujisadaka kabisa kwa Mungu na kwa msukumo wa Roho Mtakatifu, wanaamua kumfuata Kristo Yesu kwa karibu zaidi kwa kujisadaka na kuonesha upendo kwa Mungu, anayepaswa kupendwa kuliko vitu vyote. Rej. Perfectae caritatis, 1 na KKK, 916.

Shirika la Wa Oblate wa Mtakatifu Yosefu: Mkutano mkuu wa 28.
Shirika la Wa Oblate wa Mtakatifu Yosefu: Mkutano mkuu wa 28.

Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume ni kipindi maalum cha watawa kukutana katika: Sala, tafakari na mang’amuzi ya kina mintarafu amana na utajiri wa mashirika na wanashirika wenyewe. Ni wakati muafaka kwa wanashirika kufanya upembuzi yakinifu kuhusu maisha na utume wa mashirika yao, kwa kuangalia changamoto, matatizo na fursa zilizopo kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni wakati muafaka wa kusoma alama za nyakati na kuangalia wapi ambapo Roho Mtakatifu anawataka kwenda baada ya mikutano yao mikuu. Lengo kuu ni kuhakikisha kwamba, watawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili kwa kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu kama chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake tayari kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.

Wa Oblate wa Mtakatifu Yosefu: Kujificha, Ubaba na Maskini
Wa Oblate wa Mtakatifu Yosefu: Kujificha, Ubaba na Maskini

Shirika la Oblati wa Mtakatifu Yosefu “Oblati di San Giuseppe” kwa Kilatini: Congregatio Oblatorum S. Ioseph, Astae Pompejae), O.S.I., lilianzishwa tarehe 14 Machi 1878 na Padre Giuseppe Marello (1844-1895), alitangazwa kuwa ni Mwenyeheri tarehe 26 Septemba 1993 huko Asti na hatimaye, Mtakatifu Yohane Paulo II akamtangaza kuwa ni Mtakatifu tarehe 25 Novemba 2001. Shirika la Oblati wa Mtakatifu Yosefu lilitambuliwa rasmi na Vatican na kupewa hadhi ya kuwa ni Shirika la Kipapa tarehe 11 Aprili 1909 na Vatican kupitisha Katiba ya Shirika tarehe 1 Desemba 1929. Shirika hili chini ya uongozi wa Padre Jan Pelczarski aliyechaguliwa hivi karibuni kuongoza Shirika, ikiwa ni awamu yake ya pili, Jumatatu, tarehe 26 Agosti 2024 akiwa ameambatana na wajumbe wa Mkutano mkuu wa 28 wa Shirika, walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican.

Muasisi wa Shirika: Mt. Giuseppe Marello 1844-1895
Muasisi wa Shirika: Mt. Giuseppe Marello 1844-1895

Mkutano huu mkuu unanogeshwa na kauli mbiu “Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.” 2Tim 1:6. Haya ni maneno yenye kuwajibisha kwa kutambua utakatifu wa maisha ya Mwanzilishi wa Shirika, Karama na Historia ya Shirika, changamoto na mwaliko wa kulinda na kuhakikisha kwamba, karama na mapaji ya wanashirika yanatumiwa kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani mintarafu maisha na utume wa Mtakatifu Yosefu, Mlinzi wa Familia Takatifu, ambaye ni kielelezo, Muhamasishaji, Mlinzi na Mwombezi wa Shirika lao. Baba Mtakatifu Francisko mintarafu maisha yao ya kitawa na huduma yao kwa Kanisa, katika hotuba yake amekazia mambo makuu matatu: Kujificha, Ubaba na Upendeleo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mtakatifu Giuseppe Marello (1844-1895), anakazia umuhimu wa kuzamisha mizizi katika imani na maisha ya kitawa, tayari kuishi pamoja na Kristo Yesu. Wanashirika wanahimizwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Ushiriki mkamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Tafakari ya kina ya Neno la Mungu pamoja na kujitahidi kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Wajenge utamaduni wa Kuabudu Ekaristi Takatifu kama mtu binafsi na katika maisha ya kijumuiya.

Mafungamano na Yesu: Sala, Neno, Sakramenti za Kanisa na Kuabudu Ekaristi
Mafungamano na Yesu: Sala, Neno, Sakramenti za Kanisa na Kuabudu Ekaristi

Mtakatifu Yosefu katika maisha na utume wake, alijifunza kumsikiliza Kristo Yesu na kumshirikisha Injili ya maisha na kwamba, bila Kristo Yesu ni vigumu watawa kuweza kusimama kwa miguu yao wenyewe. Yote haya ni muhimu katika maisha yao hasa wanapotekeleza utume wao miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Kipaumbele kiwe ni ukomavu wa kiimani. Wawe na nyoyo zinazojielekeza katika Injili ya upendo na furaha ya milele, daima wakiwa tayari kushirikishana mang’amuzi ya Shirika lao; mambo yatakayowawezesha kumkaribisha Kristo Yesu katika maisha. Wanashirika watunze Ubaba kwa ajili ya huduma kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watu wanaosiginwa kwa umaskini. Wawe na moyo wa Kibaba anayeteseka pamoja na vijana wake wanaoathirika kutokana na mifumo mbalimbali ya ubaguzi, kielelezo cha ulimwengu unaoyumba. Vijana wanahitaji kuendelezwa kwa kujengewa uwezo, kwa kuongozwa na watu wenye busara, wavumilivu na wakarimu. Ili ni jukumu linalopaswa kutekelezwa kwa kushirikiana na kuwaambata wazazi walezi wao. Baba Mtakatifu anawataka wanashirika kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini; kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Huu ndio upendo unaosimikwa katika ukarimu; kwa kutambua uwepo angavu wa Mwenyezi Mungu miongoni mwa maskini, katika hali ya unyenyekevu. Mwenyezi Mungu amejifanya maskini kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Giuseppe Marello, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa vijana wa kizazi kipya, lakini zaidi kwa ajili ya umaskini wa vijana wa kizazi kipya.

Oblate wa Mt. Yosefu
26 August 2024, 14:32