Tafuta

Mwenyeheri Patriaki Stefano El Douayhy aliyeliongoza Kanisa la Wamaroniti “Wamaroni” kati ya Mwaka 1670 hadi mwaka 1704 Mwenyeheri Patriaki Stefano El Douayhy aliyeliongoza Kanisa la Wamaroniti “Wamaroni” kati ya Mwaka 1670 hadi mwaka 1704   (Maronite Patriarchate)

Mwenyeheri Patriaki Stefano Douayhy :Mwalimu wa Imani Na Mchungaji Mwema!

Mwenyeheri Patriaki Stefano El Douayhy alitangaza na kushuhudia upendo wa kichungaji; akaonesha upendo wa dhati kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; akakuza na kudumisha ujenzi wa udugu wa Kikristo; mambo msingi ambayo Mwenyeheri mpya ameliachia Kanisa, changamoto kwa waamini kutambua jinsi ya kuwa Kanisa, marafiki wa Kristo na Kanisa lake na upendo kati yao kama waamini. Mfano bora wa ujenzi wa upendo wa kichungaji na udugu wa Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Marcello Semeraro Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu, Ijumaa tarehe 2 Agosti 2024 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko alimtangaza Mtumishi wa Mungu Patriaki Stefano El Douayhy kuwa ni Mwenyeheri, Ibada ya Misa Takatifu imeadhimishwa huko Bkerke, nchini Lebanon. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 4 Agosti 2024 alimtaja Mwenyeheri Patriaki Stefano Douayhy aliyeliongoza Kanisa la Wamaroniti “Wamaroni” kati ya Mwaka 1670 hadi mwaka 1704 yaani ameliongoza Kanisa kwa takribani miaka thelathini. Hiki ni kipindi kilichokuwa na changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa. Hiki kilikuwa ni kipindi cha nyanyaso, dhuluma na mateso makali kwa Wakristo. Alikuwa ni Mwalimu wa imani na mchungaji bora na makini kwa watu wa Mungu nchini Lebanon. Alikuwa ni chombo na shuhuda wa matumaini, daima alijitahidi kuambatana na watu wake.

Mlipuko wa Bandari ya Lebanon ulisababisha maafa makubwa
Mlipuko wa Bandari ya Lebanon ulisababisha maafa makubwa

Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 4 Agosti 2020 mlipuko mkubwa ulipotokea kwenye bandari ya Beirut nchini Lebanon na hivyo kusababisha watu zaidi ya 2,000 kupoteza maisha, watu 6, 500 kujeruhiwa vibaya sana pamoja na uharibifu mkubwa wa miundo mbinu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbuka waathirika wa mlipuko huo. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wahusika wataweza kuharakisha kutoa habari kuhusu: ukweli na haki kutokana na mlipuko huo. Mwenyeheri Patriaki Stefano El Douayhy awaombee watu wa Lebanon imani na matumaini. Kwa upande wake, Kardinali Marcello Semeraro Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu katika mahubiri yake amemwelezea kuwa ni mfano bora wa upendo wa kichungaji; kiongozi aliyejitahidi kujenga na kudumisha udugu wa Kikristo miongoni mwa watu wa Mungu nchini Lebanon na kwamba, Mwenye haki atastawi kama mtende, atakuwa kama Mwerezi wa Lebanon Zab 92:13.

Mwenyeri Patriaki Stefano Douayhy awaombee Walebanon.
Mwenyeri Patriaki Stefano Douayhy awaombee Walebanon.

Kardinali Marcello Semeraro ameliombea Kanisa la Lebanon ili liendelee kuishi katika Madhabahu ya Mungu; mahali ambapo watu wanaishi kwa amani na utulivu, ushuhuda wa uwepo angavu wa Mungu kati pamoja na waja wake; daima wakijitahidi kujenga na kudumisha umoja na kuendelea kuwa ni vyombo vya imani na matumaini thabiti. Waamini walei waendele kuwajibika katika masuala ya kisiasa sanjari na kujikita katika ujenzi ya Jumuiya ya waamini nchini Lebabon. Mwenyeheri Patriaki Stefano El Douayhy ameliongoza Kanisa la Maronite kwa kipindi cha miaka thelathini iliyo sheheni nyanyaso na madhulumu ya Kanisa sanjari na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Mara kwa mara ilimbidi kukimbia makazi, ili kusalimisha maisha yake. Aliishi hali hii kama sehemu ya wito wake, kama yasemavyo Maandiko Matakatifu “ili Sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, Kanisa lake.” Kol 1:24. Kutoka katika undani wa maisha yake, alijijengea utamaduni wa kusamehe na kusahau, akaendelea kujisadaka kwa ajili ya upendo wake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Huyu ndiye Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Mwenyeheri Patriaki Stefano Douayhy shuhuda wa ujenzi wa udugu
Mwenyeheri Patriaki Stefano Douayhy shuhuda wa ujenzi wa udugu

Katika maisha na utume wake, alijitahidi kumwiga Kristo Yesu mchungaji mwema aliyekuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wa Kristo Yesu. Rej Yn 10:11. Alijikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kinyume kabisa cha viongozi wengi katika ulimwengu mamboleo wanaojitafuta wenyewe na kwa ajili ya mafao binafsi. Ni kiongozi aliyekuwa mwadilifu, mwenye hekima na busara akajaliwa kipaji cha diplomasia; akajikita katika mchakato wa upendo wa kiekumene na majadiliano ya kidini na waamini wa dini nyingine. Kwa ufupi kabisa, Mwenyeheri Patriaki Stefano El Douayhy alitangaza na kushuhudia upendo wa kichungaji; akaonesha upendo wa dhati kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; akakuza na kudumisha ujenzi wa udugu wa Kikristo; mambo msingi ambayo Mwenyeheri mpya ameliachia Kanisa, changamoto kwa waamini kutambua jinsi ya kuwa Kanisa, marafiki wa Kristo Yesu na Kanisa lake na upendo kati yao kama waamini.

Lebanon

 

 

05 August 2024, 15:14